29.8 C
Dar es Salaam
Monday, October 7, 2024

Contact us: [email protected]

WASICHANA: TAMAA, VISHWAWISHI VINATUPONZA KUBEBA MIMBA KABLA YA UMRI

 

Na GABRIEL MUSHI


“SIWEZI kufanya kazi ya kusomesha wazazi. Hata kama ni mtoto wangu, siwezi kumfundisha. Hilo haliwezi kutokea ndani ya utawala wangu. Sikumpeleka mtoto shule ili apate mimba. Ninatoa elimu ya bure kwa wanafunzi ambao wameamua kusoma.” Hiyo ni kauli aliyoitoa Rais John Magufuli Julai mwaka huu mkoani Pwani.

Licha ya kauli hiyo kuzua mjadala kutoka kwa wadau mbalimbali wa elimu na afya nchini, inabainisha mojawapo ya madhara ya ndoa na mimba za utotoni kuwa ni kukosa haki ya kuendelea kupata elimu kwa wakati sahihi.

Mimba na ndoa za utotoni ni wakati msichana anapopata mimba au kuolewa kabla ya umri wa miaka 18. Mara nyingi kuna matokeo mabaya ya kimwili na kiakili kwa mama na mtoto wakati wa ujauzito, ambayo yanaweza kuepukwa kama msichana atusubiri mpaka atakapofikia umri sahihi.

Tatizo la ndoa na mimba za utotoni limekuwa likiongezeka kila mwaka na kutajwa kusababisha umaskini mkubwa katika familia na mataifa mengi katika Bara la Afrika.

Tatizo hili hili pia limekuwa likichangia vifo vya mabinti wengi katika jamii zetu.

Kwa mujibu wa Shirika la Idadi ya Watu katika Umoja wa Mataifa (UNFPA), kila mwaka watoto milioni 7.3 wa kike chini ya miaka 18 hushika mimba. Huku katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, Tanzania na Uganda ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa changamoto za mimba za utotoni.

Pia takwimu za utafiti wa demografia ya afya (TDHS) wa mwaka jana, zinaonesha kuwa asilimia 36 ya wasichana wenye umri kati ya miaka 20-24 waliolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka 18.

Tatizo limekuwa kubwa vijijini japokuwa hata mijini lipo kwa kiwango kidogo. Takwimu zinaonesha kuwa kasi ya ufungaji wa ndoa hizo kwa Mkoa wa Shinyanga ni asilimia 59, Tabora asilimia 58, Mara asilimia 55, Dar es Salaaam asilimia 17 na Iringa asilimia nane.

 

Tatizo ni nini?

Mratibu wa masuala ya uelimishaji wasichana kutoka Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), Amina Ally anasema moja ya visababishi vya mimba na ndoa za utotoni ni kiwango kidogo cha elimu ya afya ya uzazi.

Anasema wazazi wamekuwa waoga kuzungumza moja kwa moja na watoto wao kuhusiana na masuala ya uzazi, hivyo mtoto anapoanza kupata mabadiliko ya mwili wazazi hawana nafasi kuongea nao.

“Pia baadhi ya mambo yanayochangia mimba na ndoa za utotoni ni umaskini, tamaa, kufanya ngono zembe, shinikizo rika na utamaduni.

“Kutokana na hali hiyo, CDF tumeanzisha mradi wa kuelimisha jamii katika Kata ya Kitunda iliyopo jijini Dar es Salaam ili kuhakikisha kukomesha vitendo hivi.

“Mradi huu uliofadhiliwa na ubalozi wa Uholanzi unatekelezwa katika Mkoa wa Dar es Salaam kwa sababu unakabiliwa na tatizo hili kwa asilimia 19 na Kitunda ni eneo ambalo wakazi wengi ni watu wenye tamaduni na desturi za mikoa ya kanda ya ziwa inayoongoza kwa kuwaozesha watoto wao mapema,” anasema.

 

Wasichana wafunguka

Wakizungumza na MTANZANIA baadhi ya wasichana wanaoishi katika kata hiyo, wanasema mbali ya utandawazi pia tamaa ya kuolewa imekuwa mojawapo ya chanzo cha mimba za utotoni.

Mmoja wa wasichana hao, Adela Anthony (17), anasema mabadiliko ya teknolojia, mfumo wa maisha na mila zimewaathiri.

“Mtoto wa miaka 16 anaolewa. Kama mzazi anamuoza, mtoto huyo atapata mimba wakati sheria zetu zinasema msichana mwenye umri chini ya miaka 18 bado ni mtoto.

Naye Josephina Damian (19) ambaye amemaliza kidato cha nne mwaka jana anasema mimba za utotoni zimesababisha marafiki zake watatu kushindwa kuhitimu elimu ya sekondari.

“Marafiki zangu watatu tulikuwa tunasoma wote waliishia kidato cha tatu baada ya kupata mimba, hali hii inatokana tamaa ya fedha na wazazi kutowapatia elimu ya uzazi ili wajitambue miili yao.

Aidha, Julieth Paulo anasema baadhi ya wasichana huingia kwenye uhusiano kwa tamaa ya kutaka kuolewa ili hali hawajatimiza umri sahihi.

“Tunaona utandawazi umeathiri, mabadiliko ya teknolojia tunayatumia vibaya, mtoto wa miaka 10 anamiliki simu ya kijanja (smart phone) anangaalia picha na video za ngono na mambo mengine, vile vitu anavyoviona anaanza kwenda kuvifanya kwa vitendo, laiti wazazi wangekuwa na uwezo wa kuelimisha watoto wao wasingewapa nafasi ya kutumia simu hizo,” anasema.

 

Madhara ya tatizo

Amina kutoka CDF anafafanua kuwa yapo madhara yanayoweza kumpata msichama pindi anapopata mimba chini ya umri wa miaka 18.

Anasema wasichana wanaoolewa au kupata mimba za utotoni hupoteza fursa na haki ya elimu. Wengi wao hufukuzwa shuleni au wazazi wao kupoteza imani kwao kiasi kwamba husita kuwaendeleza kimaisha hata baada ya kujifungua, hali hii hufungua mlango kwa msichana kuingia katika umaskini na kuzaa ovyo bila mpangilio.

“Pia hupata madhara kimwili kwa kuwa hawajawa tayari kuyakabili majukumu ya uzazi na unyumba kwa sababu nyonga za wasichana wanaoendelea kukua mara nyingi huwa changa na finyu kiasi kwamba husababisha matatizo mengi ya uzazi wakati wa kujifungua kwa njia ya kawaida.

“Wasichana wengi huchelewa kujifungua au uchungu huchukuwa saa nyingi kabla ya kujifungua, hali hii inaweza kusababisha kifo cha mama au mtoto au wote wawili kama matibabu ya dharura ya upasuaji kwa ajili ya uzazi hayakufanyika. Idadi kubwa ya akina mama wanaojifungua kwa njia ya upasuji ni wale walio na umri mdogo.
“Wasichana wanaopata ujauzito na kujifungua katika umri mdogo wengi wao pia hupata tatizo la fisitula, ambayo husababisha msichana kutokwa na haja ndogo au kubwa bila kujizuia. Uambukizo wa bakteria katika njia ya kizazi pamoja na kupata kifafa cha mimba. Huzaa watoto wenye uzito pungufu au njiti. Pia wasichana wanaozaa katika umri mdogo hupata hali ya aibu na hisia ya kudharauliwa.

 

Jitihada za Serikali

Kumekuwapo na jitihada mbalimbali za kuokoa watoto wa kike kutumbukia katika mimba na ndoa za utotoni.

Hatua ambazo zimechukuliwa, kutunga sheria ya mitandao, inayozuia watu kutumiana picha za ngono, pia nchi za Afrika Mashariki baadhi zimeridhia hatua hizo lengo ni kujaribu kutengeneza maadili ya watoto.

Naye Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu  anasema: “Tunataka Tanzania kuwa nchi ya viwanda, lakini hatutaweza kuwa na nchi yenye viwanda wakati watoto 36 katika kila watoto 100 nchini wanaolewa kabla ya kufikia umri wa miaka 18 na watoto 27 wa Kitanzania wanapata mimba kabla ya umri huo, hili ni tatizo kubwa ambalo athari zake zitaonekana baadae.”

Akizindua ripoti ya utafiti kuhusu athari za mimba na ndoa za utotoni ambao ulifanywa kwa ushirikiano kati ya CDF na wizara yake katika kuhakikisha ndoa hizo zinakoma, ameanza kutumia marekebisho ya Sheria ya Elimu yaliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Juni mwaka jana, ambayo yanakataza mtu yeyote kumuoa mwanafunzi wa elimu ya msingi au sekondari kwa kuwa ni kosa la jinai lenye adhabu ya miaka 30 jela.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles