22.1 C
Dar es Salaam
Monday, July 22, 2024

Contact us: [email protected]

Chui avamia kijiji aua na kujeruhi watu nane

Na Allan Vicent, Tabora

WAKAZI wa Kijiji cha Kakulungu kata ya Milambo-Itobo wilayani Nzega mkoani Tabora wamekumbwa na taharuki kubwa baada ya Chui kuvamia Kijijini hapo na kuua mtoto wa miaka 11 na kujeruhi wananchi wengine nane .  

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani hapa, ACP Richard Abwao amethibitisha kutokea tukio hilo na kubainisha mtoto aliyeuawa kuwa ni Maganga Myete (11) msukuma mkazi wa Kijiji hicho.

Amesema Chui huyo ambaye alitokea kwenye hifadhi ya msitu wa Ipala na kuvamia makazi ya watu majira ya saa 2 usiku, alimshambulia katika maeneo mbalimbali ya mwili ikiwemo kumng’ata shingoni ambapo alitokwa na damu nyingi na kupoteza maisha kabla ya kufikishwa hospitalini.

Ameongeza kuwa baada ya kumshambulia aliendelea kujeruhi watu wengine katika maeneo mbalimbali na kuwasababishia maumivu makali kabla ya kutoweka.

Ameeleza kuwa baada ya kutoweka walifanya msako mkali kwa kushirikiana na wananchi na Maofisa Wanyamapori na kufanikiwa kumwua.

Kamanda Abwao alitaja watu wengine waliojeruhiwa kuwa ni Peter Ziloba (55), Juma Seleman (78), Jumanne Yona (29), Hadija Mrisho (20) na mwanafunzi wa darasa la 3 katika shule ya msingi Kahurungu Buhere Emanuel (11) wote ni wanyamwezi, wakazi wa Kijiji cha Magengati.

Wengine waliojeruhiwa ni Lusia Ilumba (70), Mateo Lubigiri (60) na mtoto Mwashi Bundala (10) wasukuma, wakulima wanaoishi katika Kijiji cha Milambo-Itobo.

Aliongeza kuwa majeruhi wote wamepelekwa katika hospitali ya Ndala wilayani humo kwa ajili ya matibabu zaidi na afya zao zilikuwa zinaendelea vizuri.  

Alitoa wito kwa wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya misitu ya hifadhi kujihadhari na wanyama wakali ikiwemo kutoacha watoto pekee yao nyumbani na wanapowaona wanyama katika makazi yao watoe taarifa haraka.  

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles