27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

CHOMBO KUNUSURU LOLIONDO

Na MWANDISHI MAALUM-DODOMA


WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amemaliza mgogoro wa matumizi ya pori tengefu la Loliondo ambao umedumu kwa takriban miaka 26.

Hatma hiyo ilifikiwa jana  kwenye kikao kilichoitishwa  Dodoma  kutoa mrejesho uliofikiwa na Serikali kuhusu utatuzi wa mgogoro huo baada ya kupokea taarifa ya Kamati ya Uchunguzi.

Majaliwa alisema Serikali imekubali mapendekezo ya kuunda chombo maalum kitakachosimamia eneo la Loliondo  kunusuru ikolojia ya Hifadhi ya Serengeti na kulinda mazingira na eneo mahsusi la mazalia ya wanyamapori, mapito na vyanzo vya maji.

“Baada ya kupitia mifumo mbalimbali, timu ya wataalam ilipendekeza kuwa utumike mfumo maalum utakaounda chombo maalum.

“Kwa kuwa una maslahi mapana kwa pande zote husika na unalenga kuleta amani na kufikia lengo la kuwa na uhifadhi endelevu katika eneo la Loliondo,” alisema.

Waziri Mkuu aliiagiza Wizara ya Maliasili iandae muswada wa  sheria mahsusi ya kuwa na chombo maalum au mamlaka ya kusimamia eneo la Loliondo.

Alisema lengo liwe ni kunusuru ikolojia ya Hifadhi ya Serengeti  na kulinda mazingira na eneo mahsusi la mazalia ya wanyamapori, mapito na vyanzo vya maji kwa ajili ya ustawi wa hifadhi muhimu zenye maliasili na rasilimali za Taifa kwa manufaa ya wananchi wenyewe na Taifa kwa ujumla.

“Sheria itakayotungwa ihakikishe inawekewa masharti yanayozingatia maslahi ya jamii iliyopo katika eneo la Loliondo, mila zao na desturi zao   na uhusiano wao na matumizi ya ardhi,” alisisitiza Waziri Mkuu na kushangiliwa na wajumbe zaidi ya 60 kwenye kikao hicho.

Vilevile, Waziri Mkuu aliiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii iandae waraka maalum utakaowasilishwa serikalini kupitia Baraza la Mawaziri kuhusu umuhimu wa kutunga sheria mahsusi ya eneo la Loliondo.

Alisema kuna ulazima wa kushirikisha wadau wote  baada ya rasimu ya kwanza kukamilika   wadau waipitie kwanza.

Majaliwa alisisitiza rasimu ya pili iwe imefanyiwa mapitio na kukamilika ifikapo Februari au Machi, 2018 ili mahitaji ya fedha yaingizwe kwenye mchakato wa Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2018/2019.

Aliwataka mawaziri na makatibu wakuu wizara za sekta zinazohusika na mgogoro wa matumizi ya ardhi ya Pori Tengefu la Loliondo watembelee eneo hilo   wawe na uelewa mpana kuhusu changamoto za sekta zilizopo katika eneo husika.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Mawaziri wa Maliasili na Utalii, TAMISEMI,  Ardhi na Maendeleo na Makazi; Naibu Mawaziri wa Kilimo, Maji, Mifugo na Uvuvi na Elimu na Mafuzo.

Pia kilihudhuriwa na wakuu wa taasisi za Serikali, wawekezaji walioko Loliondo, uongozi wa Mkoa wa Arusha, madiwani na wananchi kutoka Loliondo.

Desemba 2016, Waziri Mkuu alifanya ziara   wilayani Ngorongoro ambako alipokea taarifa ya   mgogoro wa matumizi ya ardhi katika Pori Tengefu la Loliondo.

Januari 2017, aliunda Kamati ya Uchunguzi iliyokuwa na wajumbe 27 ambayo iliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.

Akichangia kwa niaba ya NGOs, Mkurugenzi wa taasisi isiyo ya Kiserikali ya Pastoralist Women Council, Manda Neritiko aliishukuru Serikali kwa kuwashirikisha wananchi kutafuta suluhu ya mgogoro huo, hatua ambayo alisema haijawahi kufanyika miaka yote iliyopita.

Kwa   wawekezaji, Scott Tineja Mollel kutoka kampuni ya AndBeyond Tanzania, alisema wao kama wawekezaji wanataka kuhakikishiwa kuwapo  utalii wa kesho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles