29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Chispi chakula hatari kwa afya

chipc*Sahani moja ya chips kavu ina mafuta ujazo wa Milimita 250

*Wafanyabiashara huwa wanapikia mafuta zaidi ya Mara mbili

Na Veronica Romwald, Dar es Salaam

ULAJI wa Chipsi umetajwa kuwa hatari kwa afya ya binadamu, kwani husababisha maradhi mengi yasiyo ya kuambukiza hasa figo, moyo, shinikizo la damu, kisukari na saratani za aina zote.

Imeelezwa kuwa, sahani moja ya chipsi kavu huwa na mafuta yanayokaribia nusu kikombe cha chai ambayo ni sawa na ujazo wa mililita 250.

Hayo yalisemwa jana na Mtaalamu wa Masuala ya Chakula na Lishe wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Ulumbi Kilimba, alipokuwa akizungumza na gazeti hili  ambapo alisema walaji wengi wa chipsi wapo katika hatari ya kutengeneza sumu kwenye miili yao bila kujua.

“Chipsi ni chakula hatari, sahani moja ya chips kavu ina mafuta ujazo wa mililita 250, na kwa jinsi ilivyo watu wengi hupendelea kula chipsi mayai, kuku, soseji au hata kwa mishikaki maana yake ni kwamba kiwango hicho cha mafuta huzidi kwa sababu na vyenyewe huwa vimekaangwa,” alisema.

Alisema jambo la kusikitisha ni kwamba wafanyabiashara wengi wamekuwa hawazingatii umuhimu wa kutumia mafuta mara moja katika kukaanga vitu hivyo.

“Kwa hali halisi jinsi ilivyo huko mitaani wafanyabiashara huwa wanapikia mafuta kwa zaidi ya mara mbili na hivyo kuzidisha hatari zaidi.

“Wanazidisha hatari kwa sababu… kawaida mafuta yanapaswa kupikiwa mara moja. Kadri unavyounguza mafuta ndivyo ambavyo ule mfumo wa mafuta masafi ambayo yanatakiwa kwa mwili wa mwanadamu unabadilika na kuwa machafu, maana yake ni kwamba unapopikia mafuta zaidi ya mara mbili tayari yanakuwa yametengeneza sumu ambayo haitakiwi mwilini,” alisema.

Mtaalamu huyo alisema mafuta ambayo yanakuwa yametumika kukaangia vyakula zaidi ya mara mbili hubadilika na kutengeneza utando mweupe ambao huweza kuonekana iwapo mtu atayatazama kwa macho yake.

“Ule utando mweupe utakaouona unatoa ishara kwamba mafuta hayo hayafai kwa matumizi ya binadamu, lakini watu wanataka kufanya biashara hivyo huendelea kuyatumia bila kujali au pengine kutokujua kwamba wanaziweka afya za walaji katika hatari ya kupata magonjwa hayo,” alisema.

Ulumbi alisema pamoja na kiwango hicho cha mafuta ambacho huingia mwili kwa ulaji wa sahani moja pekee ya chipsi kavu, mlaji hula chumvi nyingi iliyopo ndani ya nyanya maalumu iliyosagwa (tomato).

“Ile ‘tomato sauce’ jinsi ilivyotengenezwa ina chumvi nyingi, sasa umekula mafuta mengi jumlisha na hiyo chumvi nyingi na ninavyofahamu walaji wengi wa chipsi hupendelea kushushia na kinywaji chenye sukari nyingi maana yake unakuwa umetengeneza sumu ndani ya mwili wako kwa mara moja,” alisema.

Alisema takwimu zinaonesha kuwa idadi ya wagonjwa wanaougua magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza nchini inaongezeka, hata hivyo hali hiyo inaweza kuepukwa iwapo watu watazingatia ulaji unaofaa.

“Wengi hatuzingatii ulaji wa chakula bora, tunakula mradi tule na hatuzingatii kupima afya zetu hili ni tatizo. Wakati umefika tubadilike kwa sababu wagonjwa wanaongezeka,” alisema.

Mtaalamu huyo wa lishe, alisema utafiti uliowahi kufanyika nchini hivi karibuni unaonesha kuwa kati ya watu 100 wenye umri wa kati ya miaka 25 na kuendelea tisa kati yao tayari wanaugua ugonjwa wa kisukari huku wawili wakiwa hawajijui kuwa wana maradhi hayo.

“Kila mwaka duniani watu milioni 12 hugundulika kuwa wana saratani na asilimia 60 ya magonjwa ya saratani yanasababishwa na mfumo mbovu wa maisha hasa ulaji usiofaa.

“Wenzetu wazungu ni wajanja si kwamba hawali chipsi, wanakula lakini wanazingatia ‘menu’ ya sahani yao, kwamba inakuwa na viazi kidogo, mboga mboga nyingi lakini sisi kwetu ni kinyume watu wanapenda tomato kwa wingi,” alisema.

Alisema ulaji wa mbogamboga ni jambo la msingi kwani huenda kusaidia kurahisisha mfumo wa umeng’enywaji wa chakula tumboni.

Utafiti wa Marekani

Ulaji wa mara kwa mara wa chips inaelezwa kuwa unaweza kuongeza uwezekano wa mwanamke kuwa katika hatari ya kupata maradhi ya kisukari wakati wa ujauzito. Wameeleza watafiti wa Marekani.

Sababu wanga uliomo katika viazi unaweza kusababisha kuongezeka kwa viwango vya sukari zaidi, wanasema. Utafiti wao ulihusisha wanawake wajawazito zaidi ya 21,000.

Lakini watafiti wa Uingereza wanasema ushahidi huo una upungufu na kuongeza kuwa watu wengi wanahitaji kula zaidi vyakula vya wanga ili kupata nyuzi nyuzi, pamoja na matunda na mboga.

Hata hivyo inashauriwa kuwa ni vema kubadilisha ulaji chipsi  kwa wiki kwa kula mbogamboga nyingine kunaweza kuzuia hatari hiyo.

Wataalamu wa masuala ya lishe nchini Uingereza wanasema vyakula vyenye wanga ama vya kuongeza nguvu na joto mwilini kama vile viazi, vinapaswa kuwa theluthi moja ya vyakula vinavyoliwa na watu.

Utafiti huo unatarajia kuchunguza nini chanzo cha maradhi ya kisukari yanayowapata baadhi ya wanawake wajawazito .

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles