Na Theresia Gasper -Dar -es-salaam
MSHAMBULIAJI wa Azam FC, Obrey Chirwa, amesema timu hiyo itahakikisha inatetea ubingwa wa Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu Kombe la Kagame.
Michuano ya Kombe la Kagame, itafanyika kuanzia Julai 7 hadi 21 mwaka huu nchini Rwanda.
Azam ndio bingwa mtetezi wa michuano hiyo, baada ya kutwaa taji hilo mwaka jana, ilipoifunga Simba mabao 2-1, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ikiwa ni mara ya pili mfululizo, baada ya kufanikiwa kutwaa pia mwaka 2015.
Chirwa ameongeza mkataba wa mwaka mmoja wa kuendelea kuitumikia Azam, baada ya ule wa awali kumaliza msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Baraa ulipofika tamati.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Chirwa alisema amejiandaa kupambana ili kuhakikisha anaisaidia timu yake hiyo kutwaa ubingwa huo.
“Nimeshaongeza mkataba baada ya kufanya mazungumzo na kuelewana na viongozi wangu, kwa sasa tunajiandaa na michuano ya Kagame, binafsi nimejipanga kutoa mchango utakaowezesha kutwaa kutetea ubingwa,” alisema.
Akizungumzia ujio wa kocha Etienne Ndayiragije klabu kwake alisema yupo tayari kufanya kazi na kocha yeyote.
“Mimi kama mchezaji kazi yangu ni kucheza na si kuchagua kocha, nipo tayari kufanya kazi naye kuhakikisha tunatwaa mataji,”alisema.