BEIJING, CHINA
SERIKALI ya China imeapa italipa kisasi dhidi ya Marekani baada ya Rais Donald Trump kutangaza kiwango cha ushuru cha ziada cha cha dola bilioni 200 kwa bidhaa zake zinazoingizwa Marekani.
Kiwango hicho kilichotangazwa na Rais Trump kinatarajiwa kuanza kutekeleza wiki ijayo.
Pamoja na hatua hiyo ametangaza pia kuzifanyia ukaguzi bidhaa zote za China, zinazoingizwa Marekani.
Katika taarifa yake ya juzi Jumatatu Trump amenukuliwa akisema “Kwa miezi kadhaa, tumeitaka China kuifanyika marekebisho hii hali ya kibiashara isiyo ya haki na kuzitendea haki kampuni za Kimarekani.”
Katika taarifa hiyo, Trump aliendelea kusema kuwa China haioneshi nia ya kutaka kubadili mwenendo wake, ukiwemo wa wizi na kuhamisha teknolojia.
Utozaji ushuru wa sasa wa asilimia 10 wa Marekani kwa bidhaa za China ambao unadumu hadi mwishoni mwa mwaka huu, viwango vyake vinatarajiwa kuongezeka hadi kufikia asilimia 25.
Lakini Chen Fayi, mwanajeshi mstaafu nchini China anasema “Nadhani Trump atabadilika, Hana muda mrefu wa kuendelea. Sasa amefikia mwisho wake”
Katika taarifa ya hivi punde ya Wizara ya Biashara ya China, imesema ili kulinda haki na maslahi na utaratibu wa haki wa kibiashara wa kimataifa, China haina la kukwepa isipokuwa kupima hatua za kuchukua kwa lengo la kuendana na hali ya sasa kibiashara.
Taarifa hiyo haijataja kitisho cha awali cha Serikali ya China cha kutangaza kodi kwenye kadhaa za Marekani za thamani ya karibu dola bilioni 60, endapo Marekani itaendelea na kuendeleza na wimbi lake la nyongeza za kodi.
Katika utaratibu wake wa kawaida wa taarifa kwa umma Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa China, Geng Shuang amesema watatangaza hatua madhubuti watakazochukua kwa wakati muafaka.
Aliongeza kuwa hatua za upande mmoja zinazochukiwa na Marekani kwa lengo la kujikinga kibiashara hazikubaliki kwa upande wa China.
Hata hivyo, tayari Trump alikwishasema iwapo China itachukua hatua za kulipiza kisasi dhidi ya wakulima wao au hata viwanda vingine vyovyote, mara moja watakeleza awamu nyingine ya tatu, ambayo viwango vyake vya ushuru vinakadiriwa kufikia dola bilioni 267 kwa bidhaa wanazopokea kutoka China.