NA CHRISTOPHER MSEKENA
TUKIWA tunasubiri kusikia shangwe, nderemo, vifijo na mbwembwe za mafataki yakipigwa hewani kwa furaha ya kuukaribisha mwaka 2017, naingia Instagram na kuiona picha mbaya ya Chid Benz.
Ni picha moja iliyogawanywa mara mbili na kuonyesha akiwa kwenye mikao miwili tofauti. Inanishtua sababu sikuwahi kufikiria kama Chid anaweza kufika kwenye hatua mbaya kiasi kile hadi asiwe na muda wa kukata nywele.
Afya yake imedhoofika, mkono wa kulia ana bandeji, amevaa fulana kuu-kuu yenye bendera ya Jamaika pamoja na jinsi modo iliyochanika huku miguuni akitembelea yebo yebo.
Kumbukumbu inanirudisha mwaka 2009 ambapo umaarufu wake ulikua mara dufu. Kila msanii alitamani kufanya kolabo na Chid Benz, hakuna rapa aliyeweza kuvunja rekodi ya kushirikishwa mara nyingi zaidi kama alivyofanya Rashid.
Enzi hizo alikuwa na mwili mkubwa wenye nguvu ya kulitikisa jukwaa kwa saa kadhaa akitumbuiza mubashara na vyombo vya muziki. Sauti nzito iliyobeba vionjo kama ‘Ilalaaaa’ ilinogesha maonyesho yake na kufanya achukue tuzo ya KTMA kama Msanii Bora wa hip hop 2010.
Mwaka 2016 umekuwa mbaya kwa rapa huyu. Mwezi Machi baada ya kuonekana kwenye kipindi cha D’weekend Chat Show ya Clouds Tv, meneja wa Diamond Platnumz, Babu Tale, aliingiwa na huruma na kuamua kulivaa jukumu la kumpeleka Rehab, kwa ajili ya matibabu ya kuacha utumiaji wa dawa za kulevya.
Matibabu yale yalizaa matunda, afya ya Chid Benz ikaanza kurejea. Akawa karibu sana na lebo ya WCB mpaka akafanya wimbo na Ray vanny unaoitwa Chuma, mashabiki wakajua jembe limerudi shambani.
Kimemkuta nini Chid Benz mpaka amerudi kwenye utumiaji wa dawa za kulevya. Ushirikiano alioupata awali kwa kina Babu Tale na Kalapina haupati tena, ameachwa mpweke akipigania uhai wake mtaani.
Anadhalilika licha ya kuwa na historia nzuri kwenye Bongo Fleva. Ina maana imeshindikana kabisa kutumia njia mbadala ili aweze kutoka kwenye shimo hilo refu ambalo wengi wetu tunadhani ni rahisi kwake kutoka.
Wizara yenye dhamana na sanaa na wadau wengine hili la Chid Benz tulibebe kama letu sote. Mwaka 2016 imeshindikana kumsaidia basi tusiache kuendelea kujaribu kuokoa maisha ya mkali huyu wa kufoka foka katika mwaka huo mpya.