NA CHRISTINA GAULUHANGA-KISUTU
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imeshindwa kuendelea na kesi ya aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, marehemu Dk. Sengondo Mvungi hadi hapo upande wa mashtaka utakapoleta cheti cha kifo cha mshtakiwa wa kwanza, Chibago Chiugati (33), anayedaiwa kufa akiwa gerezani.
Uamuzi huo umetolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba ambaye aliuagiza upande wa mashtaka kuhakikisha unapeleka cheti cha kifo ili mahakama hiyo iweze kukiangalia na kujiridhisha ili kuondoa jina la mshtakiwa katika orodha ya washtakiwa.
“Hakuna namna nyingine ya kuliondoa jina la mshtakiwa Chiugati… nawaomba upande wa mashtaka mhakikishe cheti hicho kinapatikana mapema kwa sababu wenzetu wa magereza walileta taarifa mapema, hatuwezi kukubali kirahisi hadi cheti kitakapoonekana ndipo tutaliondoa jina lake,” alisema Hakimu Simba.
Katika kesi hiyo, kulikuwa na washtakiwa kumi ambapo wanne kati yao, waliachiwa huru baada ya kuonekana hawana hatia ambao ni Ahmad Kitabu (30), Zacharia Msese (33), Masunga Makenza (40) na John Mayunga (56).
Wakili wa Serikali, Pamela Shinyambala, alidai hivi karibuni kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), alisema hana nia ya kuendelea na kesi kwa washtakiwa hao kwa mujibu wa kifungu 91 (1) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai.
Wakili Shinyambala, alidai DPP ataendelea na mashtaka kwa washtakiwa sita waliobaki ambao ni Juma Kangungu (29), Paulo Mdonondo (30), Mianda Mlewa (40), Msungwa Matonya (30) na Longishu Losingo aliyewahi kuwa mlinzi wa marehemu Dk. Mvungi.