26.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

Chenge: Escrow ikijadiliwa nitakaa pembeni

chengeNa Elias Msuya, Dodoma

BUNGE limepitisha wenyeviti wake watatu, huku wabunge wa upinzani wakihoji kuhusu uadilifu wa Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM).

Wabunge wengine waliopitishwa kuwa wenyeviti ni wabunge wa viti maalumu, Dk. Mary Mwanjelwa na Najma Giga wote kutoka CCM.

Wenyeviti  hao walipitishwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uongozi iliyokutana Januari 24 mwaka huu.

Chenge maarufu kama ‘Mzee wa vijisenti’ amekuwa akitajwa katika kashfa mbalimbali za ufisadi ikiwamo ya ununuzi wa rada mwaka 2008.

Chenge aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika utawala wa awamu ya tatu na Waziri wa Miundombinu katika awamu ya nne, alitajwa pia kuhusika katika kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow iliyovuma kipindi cha mwisho cha uongozi wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete.

Kupitishwa kwa Chenge anayejulikana pia kama ‘Nyoka wa Makengeza’ kugombea uenyekiti wa Bunge jana, kulizua mtafaruku hasa kwa wabunge wa upinzani wakihoji kuhusu uadilifu wake.

Spika wa Bunge, Job Ndugai alilazimika kumkingia kifua kutokana na baadhi ya maswali yaliyoulizwa na wabunge hao.

Akihoji uhalali wa Chenge kugombea nafasi hiyo, Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe (Chadema), alisema kama Bunge likijadili suala la Escrow mwenyekiti huyo atafanyaje.

“Katika Bunge lililopita uliwajibishwa kwa kashfa ya Escrow, Je, siku kashfa hiyo ikiibuka bungeni utakuwa tayari kuisimamia?” alihoji Mwambe.

Hata hivyo, Spika Ndugai licha ya kuruhusu swali hilo kujibiwa alisema hilo siyo swali.

Akijibu swali hilo, Chenge alisema ikitokea suala la Escrow litajadiliwa bungeni atalazmika kukaa pembeni  kuondoa makandokando.

“Bunge letu linaongozwa na kanuni… ikitokea kuna jambo linalokuhusu, unafuata kanuni, unakaa pembeni  kuondoa makandokando katika Bunge,” alisema Chenge.

Swali jingine lililohusu kashfa ya Escrow liliulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Latifa Chande (Chadema), lakini akikuta akigonga mwamba baada ya Spika Ndugai kulikataa.

“Tunajua wewe ulitajwa katika kashfa ya Escrow na uliwajibishwa, sasa utawezaje kushika nafasi ya uenyekiti wa Bunge…” alisema Chande huku akikatishwa na kelele za wabunge wa CCM waliopinga swali hilo kuulizwa.

Kwa upande mwingine wabunge wa CCM nao waliinuka na kutaka kumhoji Chenge huku wakiepuka kugusa swali la Escrow, akiwamo Mbunge wa Nsimbo, Richard Mbogo (CCM), aliyeuliza kuhusu Kanuni ya 64 inayokataza lugha za kuudhi bungeni.

“Kanuni ya 64 inayokataza watu kusema lugha za kuudhi au matusi imekuwa ikikiukwa   na baadhi ya wabunge, utafanyaje  kuisimamia?” aliuliza Mbogo.

Akijibu swali hilo, Chenge aliwataka wabunge kusema ukweli kwa kila watakayoyatoa.

Mbali na Chenge, Spika Ndugai pia alionekana kumbeba Najma Giga dhidi ya swali la Mbunge wa Babati Mjini, Paulina Gekul (Chadema), aliyeuliza kuhusu kanuni inayokwaza wabunge kuchangia mijadala ya bajeti.

Spika Ndugai aliingilia swali hilo baada ya Giga kuonyesha kusita kulijibu akisema kanuni zote zitasimamiwa kwa usawa.

Dk. Mary Mwanjelwa ambaye ni mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Mbeya ndiye aliyekuwa wa kwanza kujieleza na kuulizwa maswali akifuatiwa na Chenge kicha akafuatia Giga.

Baada ya kujieleza, Spika Ndugai aliwahoji wabunge kama wanaafiki na kusema walioafiki ni wengi hivyo wakapitishwa.

 

HOTUBA YA RAIS

Wakati wa kujadili hotuba ya Rais John Magufuli, baadhi ya wabunge wa CCM waliomba mwongozo wa hatua zitakazochukuliwa na uongozi kwa wabunge wa upinzani waliosusia hotuba hiyo.

Hoja hiyo ilianzishwa na Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia (CCM), aliyemuuliza Chenge hatua atakayoichukua kwa wabunge wa upinzani waliosusia hotuba ya Rais John Magufuli wakati wa ufunguzi wa Bunge mwishoni mwa mwaka jana.

Lakini swali hilo lilijibiwa na Spika Ndugai akisema kuwa wabunge wote wana haki ya kuchangia mjadala huo bila kubaguliwa.

Baadhi ya wabunge walihoji tena suala hilo wakati Spika Ndugai alipompisha Naibu Spika Dk. Tulia Ackson, lakini alisisitiza kuwa msimamo ulikwisha kutolewa na Spika kuwa wabunge wote watachangia mjadala huo kwa usawa.

Wakijadili hotuba ya Rais Magufuli, baadhi ya wabunge waligusia mgogoro wa Zanzibar na kumtaka Rais John Magufuli, kuingilia kati na kumtangaza aliyeshinda urais wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea (CUF), alisema kitendo cha Rais Magufuli kuuacha mgogoro kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na vyama vya CCM na CUF ni kukwepa jukumu lake.

“Kuhusu usalama, katika ukurasa wa 10 wa hotuba ya Rais John Magufuli amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, CCM na CUF vimeshafanya juhudi. Hapo Rais Magufuli amekwepa jukumu lake.

“Utaiachiaje SMZ mgogoro kama huo? Hebu mtangaze aliyeshinda uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana,” alisema Mtolea.

Mtolea pia alizungumzia suala la afya akisema hospitali za Amana, Mwananyamala na Temeke, Dar es Salaam,  zilizopandishwa hadi na kuwa hospitali za mkoa hazina huduma hizo hivyo kuwapa mazingira magumu wagonjwa wanaofika kutibiwa.

Mbunge wa Mbozi, Pascal Haonga(Chadema), alimkosoa Rais Magufuli na kusema   uchaguzi mkuu uliopita ulighubikwa na vurugu hasa katika jimbo hilo.

“Rais amezungumzia suala la amani na utulivu akisema uchaguzi ulikwenda vizuri, nadhani aliteleza tu. Kuna maeneo mengi watu walipigwa, walibambikwa kesi na polisi na wengine wamekimbia makazi yao…Hata kule Zanzibar hali bado siyo shwari,” alisema Haonga.

Mbunge wa Mbinga mjini, Sixtus Mapunda (CCM), aliwapinga wabunge wa upinzani wanaolalamikia suala  la amani akisema Jeshi la Polisi lina lengo la kuleta amani katika operesheni zake.

Awali akitoa hoja ya kujadiliwa   hotuba ya Rais John Magufuli, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema hotuba hiyo ilitoa mwelekeo wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa miaka mitano.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles