Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam
MBUNGE wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM), ameiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutoa zuio la kudumu kwa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Baraza la Maadili ya Viongozi kuendelea kushughulikia lalamiko lolote la kimaadili dhidi yake linalotokana na ripoti ya CAG na PAC.
Malalamiko yaliyowasilishwa katika baraza hilo ni tuhuma za kupokea fedha kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa imefunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Chenge kupitia mawakili wake John Nyange na Michael Ngaro waliwasilisha maombi hayo dhidi ya Tume ya Maadili ya Viongozi, Baraza la Maadili ya Viongozi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mbunge huyo anaomba mahakama itangaze kwamba Spika wa Bunge, Waziri Mkuu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali walishindwa kutimiza wajibu wao kisheria na kikatiba na kuheshimu utawala wa sheria ambao umevunjwa.
“Maazimio ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na PAC kuhusu Chenge si sahihi kwani yalifikiwa bila kusikilizwa.
“Mahakama itamke pia mwenendo wa Bunge na maazimio yake ni batili, haki ya kikatiba ilivunjwa na malalamiko yaliyopelekwa na Tume ya Maadili ya viongozi katika Baraza la Maadili ya viongozi ni batili,” ilisema hati hiyo ya maombi.
Chenge anadai ameiomba mahakama itoe amri hizo kwa sababu 13 ikiwemo malalamiko yaliyosilishwa katika Baraza yamegubikwa na ukiukwaji mkubwa wa sheria kwa vile unatokana na masuala yaliyozungumzwa hadharani bungeni na katika vyombo vya habari.
Pia malalamiko hayo yalifunguliwa na kuendeshwa wakati kuna amri ya mahakama iliyotolewa Novemba 25, mwaka jana ikitaka hali iliyokuwepo iendelee kama ilivyo lakini ripoti zilijadiliwa pamoja na amri hiyo.
Sababu nyingine ni kwamba Tume ya Maadili na Baraza zinatakiwa kuheshimu amri ya mahakama pamoja na kwamba hawakutajwa kuwa sehemu ya wahusika katika shauri hilo.
Spika wa Bunge na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wangetii amri ya mahakama wasingejaribu wala kuthubutu kutekeleza maazimio nane ya Bunge, na kitendo cha kutangaza mwenendo wa Bunge hadharani, kurudiwa rudiwa katika vyombo vya habari kinamuhukumu Chenge wakati hakuwahi kusikilizwa na hivyo kinakiuka haki yake ya msingi ya kusikilizwa.
Ripoti ya CAG na PAC zilimtaja Chenge kuwa miongoni mwa viongozi waliopokea fedha kutoka katika Akaunti ya tegeta Escrow kupitia Kampuni ya VIP Engeneering.
Baada ya kuwasilishwa kwa ripoti hiyo Bunge lililofikia maazimio nane yakiwemo ya wote waliopokea fedha hizo washughulikiwe na vitengo vya Serikali ikiwemo tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Maombi hayo yamepangwa kusikilizwa mbele ya Jopo la majaji watatu, Augustino Mwarija, Dk. Fauz Twaib na Stellah Mgasha.
Jopo hilo limepanga kuanza kuyasikiliza Mei 21, mwaka huu, walalamikiwa watajibu Mei nane, mwaka huu na kama kuna majibu ya nyongeza yatawasilishwa Mei 15, mwaka huu.