31 C
Dar es Salaam
Thursday, December 19, 2024

Contact us: [email protected]

CHEGE, NANDY WALIAMSHA DUDE FIESTA KAHAMA

Na MWANDISHI WETU

WASANII wa muziki wa Bongo Fleva, Chege Chigunda na Nandy, walikuwa kivutio katika tamasha la burudani la Tigo Fiesta, lililofanyika juzi usiku katika Uwanja wa Taifa, mjini Kahama, kutokana na kulimudu vema jukwaa baada ya kuimba wimbo wa Kelele za Chura.

Mashabiki waliofurika katika uwanja huo, walianza kuimba wimbo huo pamoja na wasanii hao na kuzidisha shangwe zaidi.

Pia msanii wa singeli, Dulla Makabila, naye hakuwa nyuma katika kuwapagawisha wakazi wa Kahama, kutokana na kuimba wimbo wa Demu Wako Namba Ngapi, Sitaki Kuoa, Kabila gani na nyinginezo na kusababisha vumbi kubwa kutimka kutokana na mashabiki waliokuwa wakicheza nyimbo zake.

Wasanii wengine waliotoa burudani katika tamasha hilo ni pamoja na Ditto, Ben Pol, Jux,

Saida Karoli, Joh Makini, Darassa, Roma Mkatoliki, Mr.Blue, Fid Q na Stamina, Shilole, Adam Mchomvu, Coyo na Future JNL.

Akizungumzia tamasha hilo, Meneja wa Tigo Kanda ya Ziwa, Gwamaka Mwakilembe, alisema Tigo imeamua kudhamini tamasha hilo ili kuendeleza na kukuza vipaji vya wasanii na pia kuwaletea wateja wao burudani.

“Ni heshima kubwa kwa wateja wetu kuwaletea burudani hii ya Tigo Fiesta na pia kukuza na kuendeleza vipaji vya wasanii wetu, kwa hakika tunawajali wasanii wetu na wateja wetu pia na hii ni kurudisha kwa jamii kile ambacho sisi tumekipata.

“Tutawaletea wasanii wenye hadhi kulingana na mapendekezo ya mashabiki husika wa mkoa huo, tena wale waliojizolea sifa ndani na nje ya nchi,” alisema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tigo Fiesta, Sebastian Maganga, alisema tamasha hilo ni burudani ya kipekee katika Ukanda wa Afrika Mashariki na kwamba mashabiki wanafurahia muziki wa wasanii wawapendao lakini wataendelea kufurahia zaidi katika mikoa mingine.

“Tunachokifanya ni kukata kiu ya mashabiki wa burudani kwa kuwaletea wasanii wanaowapenda, hivyo tunawaahidi kuwaletea burudani zaidi zenye mguso.

“Tigo Fiesta mwaka huu kama ilivyo kauli mbiu yake ya ‘Tumekusoma’, tunawapelekea mashabiki wa mikoa husika wasanii wanaowakubali kutokana na kufanya vizuri katika nyimbo zao,” alisema.

Baada ya tamasha hilo kupagawisha wapenzi wa burudani wa Kahama, uhondo wa tukio hilo kubwa kabisa la burudani, utahamia jijini Mwanza Jumamosi katika Uwanja wa CCM Kirumba.

Maeneo mengine yatakayofikiwa na burudani hiyo ya Tigo Fiesta ni Iringa, Songea, Njombe, Sumbawanga, Morogoro, Tanga, Kilimanjaro, Mtwara na kuhitimishwa jijini Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles