Theresia Gasper -Dar es salaam
KIUNGO wa timu ya Simba, Clatous Chama, raia wa Zambia, amesema endapo Yanga itakuwa makini zaidi katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zesco United, itaweza kupata ushindi na kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo.
Yanga inakabiliwa na mchezo huo wa marudiano, unaotarajiwa kuchezwa Septemba 28 mwaka huu, mjini Ndola Zambia. Timu hizo zilipoumana katika mchezo wa kwanza, Uwanja wa Taifa jijini hapa, zilitoka sare ya bao 1-1.
Kutokana na hali hiyo ya kuruhusu bao la nyumbani, Yanga inatakiwa kusaka ushindi katika mechi hiyo ya ugenini kuanzia bao moja na kuendelea ili iweze kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Chama alisema timu zote ni bora na zenye uzoefu katika michuano ya kimataifa hivyo yoyote anaweza kushinda.
“Mechi ya kwanza ilionekana kuwa ni ya ushindani na sasa zinaenda kurudiana huku kila mmoja akiwa amemsoma mwenzake, lakini timu yoyote itakayokuwa bora zaidi inaweza kuibuka na ushindi,” alisema.
Kiungo huyo aliongeza kuwa timu zote zina wachezaji wazuri hivyo umakini, kujituma na kutofanya makosa ndiyo kutafanya mmoja apate ushindi.
Yanga inatarajiwa kuondoka nchini kuelekea Zambia, Septemba 23 mwaka huu, kwa ajili ya mchezo huo wa marudiano dhidi ya Zesco.