23.4 C
Dar es Salaam
Friday, June 21, 2024

Contact us: [email protected]

Chadema yakwaa kisiki tena kortini

Freeman MboweNa Judith Nyange, Mwanza

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Mwanza imekubali pingamizi la awali la Mwanasheria Mkuu wa Serikali, na kutupilia mbali maombi ya kibali cha mahakama cha kufungua na kusikilizwa kesi ya msingi, yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe.

Mawakili wa Mbowe, Gasper Mwanaliela na John Malya waliwasilisha maombi madogo ya kuomba kibali cha kufungua na kusikilizwa shauri la msingi  la kuiomba mahakama kubatilisha amri iliyotolewa na polisi kuzuia mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa nchini.

Maombi hayo yaliwekewa pingamizi la awali na Wakili wa Serikali, Robert Kidando anayemwakilisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Kidando aliiomba mahakama iyatupilie mbali maombi hayo akidai mleta maombi (Mbowe) aliyawasilisha kwa kutumia   kifungu cha sheria ambacho si sahihi.

Alisema maombi hayo yaliwasilishwa kwa kutumia kifungu namba 5 (3) cha Sheria ya ‘Fatal Accidents and  Miscellaneous Provision’ ya mwaka 1991 badala ya kifungu  namba 5 (1&2), ambacho ndicho sahihi kwa kuwasilisha  maombi ya aina hiyo.

Akisoma uamuzi wa mahakama jana, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Mohameid Gwae, alisema kwa kawaida maombi ni lazima yawasilishwe kwa kutumia kifungu cha sheria ambacho kitatoa mwelekeo kwa mahakama.

Jaji Gwae alisema maombi hayo yana kasoro katika sheria na mahakama haiwezi kutoa nafuu yoyote inayoombwa kwa sababu hakikutumiwa kifungu sahihi cha sheria.

“Kwa mujibu wa Sheria ya Mashauri ya Madai ya mwaka 2010, mleta maombi alipaswa kutumia kifungu 5 (1) na (2) cha Sheria ya ‘Fatal Accidents and Miscellaneous Provision’ ya mwaka 1991 badala ya kifungu 5 (3) kwenye Chamber Summons (maombi ya ofisini kwa Jaji)  na si kwenye kiapo wala maelezo. Walipaswa kufuata taratibu zilizopo kwa mujibu wa sheria.

“Kawaida maombi ni lazima yaambatanishwe na kiapo na maelezo ya mleta maombi, lakini havipaswi kuungwa mkono au kuwekwa vifungu vya sheria.

“Maombi haya yameletwa kwa kutumia kifungu 5 (3) cha sheria ambacho si sahihi, hivyo maombi haya ni batili na mahakama inayatupilia mbali,” alisema Jaji Gwae.

Nje ya mahakama, Wakili Malya anayemtetea Mbowe, alisema uamuzi wa kutupiliwa mbali maombi yao ya kibali hayajafuta kesi yao ya msingi ya kutafuta haki ya kufanya mikutano ya siasa.

Alisema mambo hayo yameondolewa kwa kuwa tu wamekosea taratibu za  kuyawasilisha mahakamani.

“Maombi yetu ya kibali yameondolewa tu kwa sababu tulikosea taratibu za kuja mahakamani.

“Tunakwenda kuyarekebisha na kuongeza vifungu vya sheria ambavyo jaji ameona ni muhimu vikawapo katika maombi yetu. Haki ya msingi ya kupigania demokrasia itapiganiwa hadi mwisho,” alisema Malya.

Naye Wakili wa Serikali, Obadia Kajungu, alisema amefurahishwa na uamuzi wa mahakama kwa kuwa imetenda haki.

Alisema upande wa waombaji walikosea utaratibu wa kwenda mahakamani kwa kutumia kifungu cha sheria ambacho si sahihi.

“Uamuzi wa mahakama umeangalia vitu viwili, haki na sheria… waombaji walikosea sheria.

“Sisi tunatetea sheria isibadilishwe na taratibu zifuatwe, kama watafuata taratibu na kuamua kurudi mahakamani watasikilizwa na haki itatendeka,” alisema Kajungu.

Mtatiro

Akizungumzia kesi hiyo kupitia ukurasa wake wa Facebook, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro, alisema itazaa hukumu kama ile ya mita mia mbili.

“Hii kesi ya kutaka mahakama iamue juu ya vyama vya siasa kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara itazaa hukumu kama ile ya mita mia mbili!

“Na kwa wanaotizama mbali wanajua kuwa ‘tuna set- Precedent’, mbaya zaidi tukiwaruhusu watawala waungwe mkono na mahakama, kwamba wanayo mamlaka ya kuzuia mikutano ya kidemokrasia kila watakapohisi ipo hali ya hatari.
“I guess Jaji atakimbilia kwenye usalama na kusahau kuwa kesi inahusu demokrasia pana na baada ya hukumu atapata ‘promotion’… nawaza tu jamani! ‘Just count on me’.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles