*Kupeperusha bendera nusu mlingoni
*Maandalizi ya mazishi yaendelea K’njaro
Na Waandishi Wetu, Dar/K’njaro
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kimepoteza mpiganaji na shujaa ambaye alikuwa mstari wa mbele kutetea haki za wanyonge.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vicent Mashinji alisema marehemu Philemon Ndesamburo hakuwa mtu hata kidogo.
Kutokana na hali hiyo, Dk. Mashinji alisema kuwa kuanzia leo chama chao kinapeperusha bendera yake nusu mlingoti nchi nzima kuanzia ngazi ya tawi hadi taifa hadi marehemu atakapozikwa.
Dk. Mashinji alisema tangu kuanzishwa mfumo wa vyama vingi, Ndesamburo alikuwa akipigania demokrasia kupitia chama chake na alitanguliza mno uzalendo.
Alisema ili kuwapo na demokrasia, Ndesamburo alibariki kuanzishwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na Operesheni Ukuta, ambayo Serikali iliizuia katika hatua za mwisho.
“Licha ya kujitahidi kuleta demokrasia kipindi kirefu, katika awamu ya tano, demokrasia imeshindwa kufikiwa kutokana na kuminywa kwa kuzuiwa kufanyika mikutano ya vyama vya siasa na mambo mengine ambayo Ndesamburo aliyapigania,” alisema Dk. Mashinji.
Aliwaomba Watanzania kuendelea kumuenzi Ndesamburo katika mambo yake mema aliyoyafanya ili kumuenzi.
Dk. Mashinji alisema Ndesamburo alitumia uwezo wake wa kifedha na akili kuhakikisha Chadema inakuwa katika nafasi nzuri iliyopo sasa.
KIMESERA
Mwanasiasa mkongwe na mwasisi wa Chadema, Victor Kimesera, alisema akiwa na Ndesamburo walihakikisha chama kinasimama imara.
Kimesera alisema anamfahamu Ndesamburo tangu mfumo wa vyama vingi ulipoingia nchini mwaka 1992, walipitia maisha magumu na yenye shida hadi kufanikiwa.
Alisema Ndesamburo alikuwa mwanzilishi pekee na mfanyabiashara ambaye hakuogopa wala hakuwa tegemezi.
“Tunahangaika kujenga chama wakati huo tukiwa na magari mawili, yote aliyatoa Ndesamburo. Tulizunguka huko na kule pamoja na mikoa ya Morogoro, Arusha, Kiteto na Tabora kujuenga chama. Chama hakikuwa na chochote, alituunganisha kwa wafanyabiashara wengine ambao tuliwafanya kuwa siri hadi leo,” alisema Kimesera.
MAZISHI
Taarifa kutoka mkoani Kilimanjaro, zinasema maandalizi ya mazishi ya marehemu Ndesamburo yameanza, baada ya jana kutwa nzima familia kushinda kwenye vikao.
Mazishi hayo yatafanyika kwa kushirikisha familia, viongozi wa Chadema na Serikali.
Msemaji wa familia ambaye ni mtoto mkubwa wa marehemu, Sindato Ndesamburo, alisema baba yake anatarajia kuzikwa Jumanne ijayo katika makaburi ya KDC Kiboriloni.
“Tumekubaliana baba atazikwa Jumanne ijayo, maandalizi yanaendelea vizuri… kama unavyojua msiba huu ni wa taifa, tunamsubiri Freeman Mbowe (mwenyekiti) afike kutoka Dar es Salaam ili tupate utaratibu kamili,” alisema.
Sindato alisema wanatarajia kupata wageni wengi wa kitaifa na kimataifa ambao watahudhuria mazishi hayo.
Alisema siku hiyo mwili utapelekwa kwenye Uwanja wa Mashujaa ambako wananchi watapata nafasi ya kutoa heshima za mwisho na ibada itafanya hapo hapo.
Jana kutwa nzima, mamia ya waombolezaji wakiwamo wanasiasa waliendelea kumiminika nyumbani kwa marehemu kuwafariji wafiwa.
Ndesamburo aliyeshikilia kiti cha ubunge katika Jimbo la Moshi Mjini kwa miaka 15, pia alikuwa mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Kilimanjaro.
Nyumbani kwake eneo la KDC, Kata ya Kiboriloni mamia ya waombolezaji wakubwa kwa wadogo walionekana misururu mirefu, huku magari mengi yakienda kwake.
Wabunge wa Chadema, Joseph Selasini (Rombo), Godbless Lema (Arusha Mjini) na Grace Kiwelu (Viti Maalumu), jana walifika nyumbani hapo wakiwa wameambatana na mtoto wa marehemu, Lucy Owenya.
SALIM MWALIMU
Naibu Katibu Mkuu Chadema Zanzibar, Salim Mwalimu, alisema kuwa alianza kumfahamu marehemu wakati anasoma Kilimanjaro.
Alisema kitendo cha umauti kumkuta akiwa anasaini hundi ya rambirambi kusaidia familia za wanafunzi wa Shule ya Lucky Vincent waliofariki katika ajali ya gari, kinadhihirisha alikuwa ni mtu wa watu.
KUBENEA
“Namfahamu Ndesamburo kwa miaka mingi na mara ya mwisho nimekutana naye Jumamosi iliyopita alipokuja hapa Dodoma kwenye mkutano wa Baraza Kuu la chama, namfahamu kama mtu jasiri na anayejiamini.
“Kuna matukio ambayo nayakumbuka wakati nikiwa mwandishi wa habari aliyoyasimamia, miongoni mwake ni lile la mwaka 2008 la kesi ya Yusuf Manji na Mwenyekiti wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi.
“Katika kesi hiyo mzee Ndesamburo alijiondoa Kamati ya Maadili baada ya kuwepo madai ya rushwa, kwamba wabunge walihongwa na mmoja wa wanaovutana katika shauri hilo,” alisema Kubenea ambaye ni mbunge wa Ubungo.
Alisema katika kamati ya maadili taarifa zake zilikuwa za siri, lakini Ndesamburo alizitoa kwenye hadhira ya watu kwa kusema kuwa imehongwa, hakujali kamati hizo zinahusu majadiliano ya Bunge, hakujali usiri, vitisho. Kwa ujasiri wake alizungumza na waandishi wa habari.
Pia alisema anamkumbuka kutokana na kushiriki kikamilifu kumwingizia aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa hadi kugombea urais akishirikiana
na wenyeviti wa vyama vinne vya siasa.
“Wakati kulianza kuwa na sintofahamu ya kumwingiza Lowassa Chadema, Ndesamburo akiwa Kenya alirudi ghafla na kuendeleza mazungumzo kwa viongozi nyumbani kwake hadi hapo walipofanikiwa,” alisema.
Lakini pia alisema anasikitishwa na anaumia na kifo hicho kwa kuwa aliwahi kukutana naye Moshi akamwonyesha miradi mbalimbali anayoisimamia na pia alimwahidi kumsaidia kujenga mradi wa wafanyabiashara ndogo ndogo Ubungo utakaogharimu Sh bilioni 1.2.
SELASINI
Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini, alisema chama chao kimepoteza mtu makini na nguzo muhimu katika medani za siasa.
Alisema Ndesamburo alionyesha ushujaa wa hali ya juu kwa miaka mingi, hata kabla ya kuanzishwa mfumo wa vyama vingi nchini, baada ya kuamua kuacha kazi serikalini ili kushiriki mageuzi.
Alisema yeye akiwa ni mbunge na kada wa Chadema, atakuwa mnafiki asipoziishi kauli za marehemu Ndesamburo na misingi aliyojiwekea ya kufanya siasa kwa amani na utulivu.
Diwani wa Kata ya Mawenzi, Hawa Mushi alisema alikuwa ni zaidi ya kiongozi kwake.
Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, John Makundi alisema marehemu alikuwa mtu asiyependa kuendesha siasa za chuki, ubabe na makundi jambo ambalo limekuwa ni funzo kwa wanasiasia wengine wa mkoa huo.
Ndesamburo alifariki dunia juzi akiwa ofisini kwake akiendelea na majukumu, baada ya kupata mshtuko wa ghafla.
Mwili wake umehifadhiwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC.