29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Chadema ngangari, IGP Mangu aonya

Dk. Wilbrod Slaa
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa

NA WAANDISHI WETU, DAR NA MIKOANI

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeendelea kuwa ngangari kwa kusisitiza kuwa maandamano yake yako palepale.

Chadema kimesema kuwa watajilinda wenyewe katika mikutano yao kwa sababu wana vijana waliopata mafunzo ya ulinzi na usalama.

Chama hicho jana kilitangaza kuanza kutekeleza maazimio ya mkutano wake mkuu kwa ajili ya kufanya maandamano na migomo isiyo na ukomo nchi nzima.

Wakati Chadema wakisisitiza hivyo, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu amesema hawatambui maandamano hayo na kwamba hawatatoa ulinzi.

“Tulishatoa kauli tangu mwanzo na haijabadilika, hivyo maandamano yoyote yatakayofanywa ni batili,” alisema IGP Mangu alipozungumza na gazeti hili jana.

Wakati IGP Mangu akisema hatambui maandamano hayo, Chadema imesema inafanya hivyo kwa mujibu wa sheria na siyo lazima IGP ayatambue.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkurugenzi wa Oganaizesheni wa chama hicho, Benson Kigaila, alisema wamepeleka taarifa kwa mujibu wa sheria ili waruhusiwe.

“Sheria inasema chama cha siasa kinatakiwa kimtaarifu kamanda wa polisi wa eneo husika na kama anao ulinzi au hana ataeleza hilo.

“Kama hawana ulinzi sisi tunaweza kujilinda wenyewe na hakuna kitakachoharibika kwa sababu tunao vijana tuliowapa mafunzo ya ulinzi na usalama,” alisema Kigaila.

Akizungumzia kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuhusu Bunge Maalumu la Katiba, Kigaila alisema hata wao wanatambua Bunge hilo liko kwa mujibu wa sheria, lakini mambo yanayotendeka ndiyo yanakwenda kinyume na sheria.

MWANZA

Jeshi la Polisi mkoani Mwanza limeonya wafuasi na makada wa chama hicho kutojaribu kuandamana na atakayefanya hivyo atakamatwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mulowola, alisema askari wamejipanga kudhibiti waandamanaji siku na saa yoyote watakapotokea.

SIMIYU

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Venance Kimario, naye amewaonya wafuasi wa Chadema kutoandamana kwa vile maandamano hayo yamepigwa marufuku.

Alisema viongozi wa chama hicho walipeleka barua kuomba ulinzi kufanya maandamano, lakini polisi walikataa ombi hilo.

Kiongozi wa Chadema wa Operesheni Kanda ya Ziwa Magharibi, Tungaraza Njugu, alisema maandamano katika mikoa ya Mwanza, Geita na Kagera yatakuwa ya siku moja na muda wowote ambao hakuutaja.

Mwenyekiti wa Chadema mkoani Simiyu, Mshuda Wilson, alisema  maandamano hayo yatakuwa ya amani na kulitaka Jeshi la Polisi kutotumia nguvu.

SHINYANGA

Mkoani Shinyanga maandamano yaliyotangazwa kufanyika jana hayakufanyika.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Mussa Athumani, alisema ole wake mfuasi wa chama atakayeandamana atakumbana na mkono wa dola.

Maandamano hayo yalitarajiwa kufanyika kuanzia saa 2 asubuhi yakianzia ofisi za chama hicho mjini Shinyanga kulekea viwanja vya Shycom.

Katika hali ya kushangaza, hakuna kiongozi hata mmoja wa chama hicho aliyejitokeza na muda wote ofisi ya chama hicho ilionekana imefungwa, polisi wakiwa wametapakaa katika mitaa mbalimbali mjini Shinyanga.

DK. KIGWANGALA

Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Dk. Khamis Kigwangala (CCM), amelitaka Jeshi la Polisi kuacha kuyazuia maandamano ya Chadema kwa kuwa hayana wafuasi.

Dk. Kigwangala ambaye pia ni Mbunge wa Nzega, alitoa kauli hiyo bungeni jana wakati akichangia mjadala wa mabadiliko ya kanuni za Bunge hilo.

Alisema maandamano ya Chadema hayana athari zozote kwa kuwa hakuna watu watakaojitokeza kuandamana, hivyo alilitaka Jeshi la Polisi kuyapuuza kwa kutoyazuia.

Kauli ya Dk. Kigwangala iliungwa mkono na mjumbe mwingine, Dk. Charles Tizeba aliyetaka maandamano hayo yapuuzwe.

Habari hii imeandikwa na Nora Damian (Dar), Benjamin Masese (Mwanza), Samwel Mwanga (Simiyu), Debora Sanja (Dodoma) na Kadama Malunde (Shinyanga).

- Advertisement -

Related Articles

2 COMMENTS

  1. Jeshi la Polisi linajivunia kwa kuvunja sheria za nchi. Maandamano siyo kosa la jinai kwa mujibu wa sheria zetu. Kama jeshi hili aliwezi kuwashitaki viongozi wa CHADEMA wanaoitisha maandamano wao wakategeme kuua watu tu. Askari polisi wajue kuwa wanaofanya kitendo cha kusitisha maisha ya watu wanamfanyia kosa MWENYEZI MUNGU na katika hili wanaziweka familia zao kuwa na laana ya umwagaji damu. Ni bora kama kuna askari polisi walio na elimu waache kazi hiyo na kisha kujiunga na kazi zingine ambazo hazina mazingira ya kulinda maslahi mfu ya viongozi.

  2. Hivsi, hawa police hawakifunzi kwa katibu wa umoja wa mataifa alivyo tanya maandamano ya amani kupinga uchafuzi mazingira.SWALI LA MSINGI JE HAO POLICE WANAONA RAHA KWA HAO WABUNGE KUENDELEA KUJINEEMESHA NA MAKATO YA MISHAHARA YAO?.IPO SIKU WATAJUA HAKI YAO NA WATAWAUNGA CHADEMA MKONO NA KUANDAMANA PAMOJA NAO ASANTENI NINYI MLIO ONA TAIFA LINAVYO ANGAMIA.Mfano sahihi Mkuu wa yuko ugenini busy mwezi je unafikiri ni sh zitatumika kwa huo muda wote huko mashuleni hakuna madawati mishahara midogo kwa watumishi secta elimu na afya pembejeo kwa wakulima nk.police achem

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles