24.5 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

…Kura za wajumbe kukusanywa kwa mtandao

Samuel Sitta
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba ambaye pia ni Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta

NA MAREGESI PAUL, DODOMA

BUNGE Maalumu la Katiba limelazimika kubadili kanuni ili kuwaruhusu wajumbe walio nje ya Bunge hilo kupiga kura za kupitisha rasimu ya Katiba.

Pia, Bunge hilo limebadili kanuni ya 36 inayoagiza mjumbe apige kura ibara kwa ibara ili kuruhusu mjumbe apigie kura ibara zote zilizoko katika sura moja au zaidi ili kupunguza muda wa wajumbe kupiga kura.

Uamuzi huo ulifikiwa jana baada ya mjumbe wa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge Maalumu, Amon Mpaju kuwasilisha mapendekezo ya kubadili kanuni za Bunge hilo kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Pandu Ameir Kificho.

Kutokana na mabadiliko hayo, wajumbe watakaokuwa nje ya Bunge wakati wa kupiga kura Septemba 29 hadi Oktoba 2, wakiwamo walioko nje ya nchi kwa kibali maalumu cha Mwenyekiti wa Bunge hilo, watapigia kura katika ofisi za mabalozi wa Tanzania walioko katika nchi hizo.

Akisoma mapendekezo hayo na kuzungumzia kanuni ya 38 inayoeleza utaratibu wa kupiga kura, Mpanju alisema Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge ililazimika kuifanyia marekebisho kanuni hiyo ili kuwaruhusu wajumbe wote watakaokuwa nje ya nchi waweze kupiga kura kwa kuwa ni haki yao kisheria.

Kwa mujibu wa Mpanju, kanuni ya 38 haielezi jinsi wajumbe watakaokuwa nje ya Bunge watakavyopiga kura ingawa wana haki ya kufanya hivyo.

“Mambo ya msingi yaliyopelekea kufanya mabadiliko ya kanuni zetu ni kuweka utaratibu wa kumwezesha aliye nje ya maeneo ya Bunge kwa ruhusa yako kupiga kura mahali popote alipo.

“Katika kufanikisha suala hili, utawekwa utaratibu wa kupiga kura utakaotumia muda ulioainishwa kwenye kanuni za Bunge Maalumu.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, ni haki ya kila mjumbe wa Bunge hili kujadili Rasimu ya Katiba na hatimaye kupiga kura ili kupitisha ibara za sura za rasimu ya Katiba zilizoandikwa upya na rasimu ya mwisho ya Katiba.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, kanuni ya 38 imeweka utaratibu wa kupiga kura utakaotumiwa na wajumbe waliomo ndani ya Ukumbi wa Bunge Maalumu peke yake.

“Kanuni hii haijaweka utaratibu utakaotumiwa na mjumbe ambaye hayumo ndani ya ukumbi kupiga kura, hivyo inamnyang’anya mjumbe huyo haki yake ya kupiga kura.

“Kwa msingi huo, kanuni zinafanyiwa marekebisho ili kumwezesha mjumbe huyo kupata haki yake ya kupiga kura na mapendekezo haya yanamwezesha apige kura ya siri au ya wazi kwa njia ya nukushi, mtandao au njia nyingine itakayoelekezwa na Katibu wa Bunge baada ya kushauriana na mwenyekiti,” alisema Mpanju.

Akizungumzia uamuzi huo ambao ulikubaliwa na idadi kubwa ya wajumbe, Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, alisema hana mamlaka ya kumzuia mjumbe aliye nje ya Bunge asipige kura kwa kuwa ni haki yake ya msingi.

“Kuna mjumbe yuko India anaumwa, ameomba ufanyike utaratibu wa kumwezesha kupiga kura, sasa mnataka mimi nisimruhusu?

“Mwingine naye amekwenda Hija kwa mara ya sita mwaka huu, naye ameomba apewe fursa ya kupiga kura, hatuwezi kuwanyima watu fursa ya kufanya hivyo, lazima wapige kura,” alisema Sitta.

Kauli ya Sitta ilitokana na kauli za baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo waliopinga utaratibu huo kwa kuwa sheria za nchi haziruhusu.

Naye Kificho alipokuwa akitoa ufafanuzi wa njia itakayotumika kwa wapiga kura walioko nje ya nchi, alisema umeandaliwa utaratibu mzuri ili kuwatambua wapiga kura halali ambao ni wajumbe wa Bunge hilo.

Chini ya utaratibu huo, alisema wajumbe hao watawasilisha hati zao za kusafiria kwa ofisa wa ubalozi wa Tanzania aliye katika nchi husika, ambaye atawaelekeza utaratibu wa kupiga kura za wazi na za siri kisha kura hizo zitafikishwa kwa Katibu wa Bunge hilo mjini hapa.

- Advertisement -

Related Articles

3 COMMENTS

  1. Kura kwa njia ya mtandao(email) ni batili kwani hakuna sheria inayahusi matumizi ya intaneti kwani mtu yeyote anaweza kupiga kura na kujifanya kuwa ni mhusika kumbe ni uongo.Kuna watu wenye super password anaweza kutengeneza mail address ya mmbunge yoyote na kupiga kura kama mmbunge mhusika kumbe ni feki na jinsi ya kumnasa siyo rahisi na kama uchunguzi ukifanyika kwa utalaam wa juu itachukua muda mrefu.Kwa hiyo bunge la Katiba waache kujidhalilisha na hasa mwenyikit wa Bunge Maalum la Katiba! Tanzania kuna wataalam wengi na wazuri wa mambo ya Tehama ni vema waombwe ushauri wa kitaalam na kisheria, hasa sheria ya Tanzania kuhusi TEHEMA.

  2. uchakachuzi Mpya kupitia mtandao embu niambie NANI atathibitisha kuwa anayepiga kura ni mjumbe husika lakini idadi ya wajumbe si inafAamika.kama kura zikizidi idadi ya wajumbe itafahamika tu.

  3. UTARATIBU HUU UNAONGEZA MATATIZO NA USUMBUFU KATIKA KUTEKELEZA AZMA YA UPATIKANAJI WA KATIBA MPYA. NAAMINI KABISA HAO WATAKAOKUWA NJE YA NCHI WAKATI WA UPIGAJI KURA HAWATAZIDI ZAIDI YA KUMI. A PEANUT! RASIMU YA PILI HAIKUONA UMUHIMU HUO, NA WALA HAUPO KWA SASA. BABA YETU MWENYEKITI WA RASIMU YA KATIBA ANAHANGAIKIA NINI? BABA YETU RAIS ALISHAONA KWAMBA KATIBA MPYA HAIWEZEKANIKI. KWA NINI ASIHESHIMU ALIYOTAKA RAIS WETU MTIIFU WA NCHI!

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles