|Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kitafanya uteuzi wa wagombea ubunge katika majimbo ya Monduli, Korogwe na Ukonga Agosti 15 mwaka huu.
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema amesema hayo leo Alhamisi Agosti 9, wakati akizungumza na Mtanzania Digital kwa njia ya simu.
“Wameanza kuchukua fomu za uteuzi ila sisi uteuzi ni Agosti 15, ndiyo vikao vitakaa na kuteua,” amesema Mrema.
Wakati chama hicho kikijipanga kufanya uteuzi huo, tayari Chama cha Mapinduzi (CCM), katika Jimbo la Monduli kimempitisha aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo aliyejiuzulu wiki iliyopita, Julius Kalanga kuwa mgombea pekee.
Kadhalika hali ikiwa hivyo katika Jimbo la Monduli, tayari aliyekuwa Mbunge wa Ukonga aliyejiuzulu na kuhamia CCM, Mwita Waitara anadaiwa kuchukua fomu kupitia chama hicho akiomba kuteuliwa kugombea tena jimbo hilo huku katika Jimbo la Korogwe wakitarajia kufanya uchaguzi leo.
Wiki iliyopita, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ilitangaza Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika majimbo matatu na wa udiwani katika kata mbili za Tanzania Bara utakaofanyika Septemba 16, mwaka huu ambapo fomu za uteuzi wa wagombea wa majimbo hayo zitatolewa kuanzia Agosti 13 hadi 20, mwaka huu.