27.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 27, 2024

Contact us: [email protected]

Chadema, ACT, MOAT wamvaa Nape

b16Na Veronica Romwald, Dar es Salaam

VYAMA vya Chadema na ACT-Wazalendo vimelaani vikali hatua ya Serikali kusitisha Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) kurusha matangazo ya moja kwa moja katika vikao vya Bunge vinavyoendelea mjini Dodoma.

Vimesema hatua hiyo ya Serikali inaonyesha wazi kuwa imedhamiria kuendesha nchi kidikteta.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema (Taifa), Salum Mwalimu alisema hoja zilizotolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye za kusitisha matangazo hayo hazina mashiko na hazina uhalisia na kitaaluma.

Alisema tamko hilo la Waziri Nape limekiuka Katiba ambayo inaeleza wazi kuwa kila mwananchi ana haki ya kupata habari.

Mwalimu alisema Chadema pia wanamtaka Waziri Nape alete uchambuzi namna ambavyo Sh bilioni 4.2 zinatumika kutokana na vipindi hivyo vya Bunge.

“Nimefanya kazi kwenye vituo vya televisheni, lakini kila nikichambua sioni uhalisia wa gharama hizo, hivyo ni lazima atuchambulie zinatumikaje,” alisema.

Alisema pia wanamtaka ataje utafiti aliousoma unaodhihirisha kwamba muda wa saa nne usiku unafaa kurushwa kwa matangazo hayo yatakayokuwa yamerekodiwa ili wananchi waweze kuyafuatilia.

“Awali itakumbukwa kwamba wakiwa mkoani Lindi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Waziri Nape walipiga marufuku mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa kwa maelezo kwamba waachwe wale walioshinda katika uchaguzi mkuu wafanye kazi huku ni kukiuka sheria ambayo inaruhusu vyama kufanya mikutano ya hadhara.

“Lakini kama hiyo haitoshi, baadaye Jeshi la Polisi nalo lilitoa tamko lao ambalo lilikazia tamko lile lililotolewa na Serikali la kupiga marufuku mikutano ya hadhara,” alisema.

Alisema wakitazama hata namna ambavyo kamati za Bunge zilivyoundwa zinaonyesha wazi nia ya Serikali kutaka kujilinda dhidi ya maovu yake. “Kama tatizo ni fedha za kuwalipa TBC watueleze, watupe na hizo gharama zinazohitajika, tupo tayari kuhamasisha wananchi kwa kufungua akaunti maalumu ili wasaidie kuchangia kupatikana kwa fedha hizo za kulipia matangazo.

Kwa upande wake, Chama cha ACT-Wazalendo kuputia taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Samson Mwigamba jana, kilisema uamuzi huo wa Serikali ni aibu na ni hatari kwa ustawi wa nchi inayoendeshwa kidemokrasia.

“Tunalaani tukio la aibu katika nchi yetu pale Serikali ilipofanya jaribio la hatari la kuzuia wananchi kuona na kusikia kinachoendelea bungeni.

“Kitendo cha Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuzuia kuonyeshwa moja kwa moja vipindi vya Bunge katika televisheni ya Taifa ni cha kijima na sisi ACT-Wazalendo tunakilaani kwa nguvu zetu zote,” alisema Mwigamba katika taarifa hiyo.

Alisema wanakitafsiri kitendo hicho  cha Serikali kama mwendelezo wa hatua na juhudi za Rais Dk. John Magufuli za kuminya demokrasia na kusimika utawala wa kiimla.

 

KAULI YA MOAT

Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), Henry Muhanika akizungumzia na MTANZANIA juu ya hatua ya Serikali kusitisha matangazo ya TBC, alisema hatua hiyo imewashtua wadau wa habari nchini.

“Ukweli ni kwamba hatua hiyo imetushtua na kamwe haijatufurahisha kwa sababu matangazo ya moja kwa moja yana umuhimu wake katika kufikisha ujumbe kwa wananchi.

“Ukiondoa kipindi cha maswali na majibu, kuna kipindi kingine ambacho huenda matangazo yake yatahaririwa na wakati mwingine yatatoa picha nyingine tofauti na vile ambavyo watu wangeshuhudia moja kwa moja,” alisema.

Muhanika alisema inasikitisha kuona kwamba hatua hiyo imekuja hivi sasa wakati ambao unaandaliwa muswada wa habari kwa ajili ya watu kupata haki ya kupata habari.

“Hii inapunguza lengo na hatujaelewa kwa nini imekuwa hivi kwa sababu utaratibu huu unakuja wakati huu na hatuna uhakika nini kitatokea baada ya hapo. Tunajiuliza ikiwa TBC imeshindwa kurusha moja kwa moja kwa kuwa inategemea kodi za wananchi je, vyombo vingine vitaruhusiwa? Jambo hili linatutia wasiwasi juu ya uhuru wa habari nchini,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles