27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

CCM ‘yalia’ kutoshirikishwa miradi ya maendeleo

Na Clara Matimo, Sengerema

Licha ya kwamba Chama cCha Mapinduzi (CCM) ndicho chenye Ilani inayotekelezwa na Serikali lakini kimedai kutoshirikishwa kwenye utekelezaji wa baadhi ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali katika Mkoa wa Mwanza.

Hayo yameelezwa Machi 18, mwaka huu na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT),  Mkoa wa Mwanza, Ellen Bogohe, kwa niaba ya Mwenyekiti wa chama hicho mkoani humo, Antony Diallo, wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa  ya Mkoa huo ilipotembelea mradi wa ujenzi wa ghala kwa ajili ya kudhibiti uchafuzi wa sumu kuvu kwenye mazao ya mahindi na karanga katika Kijiji cha Majengo Kata ya Nyakasungwa Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema.

Kikundi cha wachapakazi kikiendelea na shughuli za ujenzi wa jengo la huduma za dharura linalojengwa  katika Hospitali ya Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza kwa gharama ya Sh milioni 44.95. Picha na Clara Matimo.

Akizungumza katika eneo la mradi huo, Bogohe amesema licha ya mradi kugharimu kiasi cha zaidi ya Sh bilioni 1.01 ikiwa umefikia asilimia 56 ya ujenzi na unatarajia kukamilika Aprili mwaka huu licha ya Wakandarasi kuomba kuongezewa muda hadi Julai 2022, chama hicho hakikushirikishwa tangu hatua za awali katika utekelezaji wake.

Bogohe ametoa kauli hiyo kufuatia malalamiko yaliyotolewa na Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Sengerema, Mark Augustine, ambaye alidai kwamba yeye, katibu wake na wajumbe wa kamati ya siasa wilaya ambao ndiyo wenye jukumu la kuisimamia serikali katika kuitekeleza ilani ya chama chao hawafahamu uwepo wa mradi huo.

“Kinachotekelezwa hapa ni ilani ya CCM, tuliahidi tutaleta huduma kwa wananchi huduma zenyewe ndiyo hizi wenye ilani yao lazima wazijue ili wazisemee kwa wanachi ambao walituamini na kutuchagua tuwaongoze, mwenyekiti wa CCM wa wilaya hajui kama kuna mradi unajengwa eneo hili, sisi tunatoka mkoani ndiyo wanapata nafasi ya kujua na kuuona inamaana kama tusingekuja ungekamilika bila wenye ilani yao kujua? Alihoji na kuongeza:

“Huu ni mnyororo ambao umeanzia wilayani kutokuwashirikisha wenye ilani yao kwa kweli mheshimiwa DC (Mkuu wa wilaya) hii haikubaliki kabisa shughuli zozote zinazofanyika kwa manufaa ya wananchi lazima chama kijue pamoja na fedha zinazotolewa ni za serikali ya CCM ambao ndiyo wanaotekeleza ilani yao, mradi huu ni mkubwa sana wa kimkakati, hebu fikiria halmashauri ziko ngapi nchi hii ni zaidi ya 180 miradi 12 tu ya namna hii inatekelezwa nchini mmoja wapo ndiyo huu lakini Mwenyekiti wake hajui nimesikitika sana.

“Tunapongeza serikali ya CCM inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuona kwamba wananchi wa Buchosa wanastahili kupata mradi huu, rais anahangaika sana kutafuta fedha ili kuja kusaidia wananchi wake, naomba sana  wanaopata zabuni za kujenga miradi wahakikishe inakamilika kwa wakati na serikali ihakikishe wananchi na wenye ilani yao wanashirikishwa, miradi yote itekelezwe kwa uwazi,” alisema Bogohe Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Mwanza.

Awali, Mratibu wa mradi huo, Peter Ntoba, akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi kwa mgeni rasmi, alisema umelenga kuongeza pato kwa wakulima, thamani ya mazao, ajira kwa vijana, kuboresha afya za wananchi na kupunguza vifo vitokanavyo na sumu kuvu ambapo zaidi ya wananchi 3,200 wanaojishughulisha na shughuli za kilimo na usindikaji wa bidhaa zitokanazo na mazao ya kilimo watanufaika.

Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Senyi Ngaga, alisema wamepokea maelekezo yote waliyopewa na kamati hiyo ambapo aliahidi kuyatekeleza kwa kushirikiana na watendaji wake.

Alisema mradi huo ulianza kutekelezwa Agosti 10, 2021 na Kampuni ya White City JV Skyline kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika(AfDB) chini ya Wizara ya Kilimo, nakwamba Mkandarasi alipaswa kukabidhi mradi huo Aprili 4, mwaka huu.

Msimamizi wa mradi huo, Mhandisi Anord Rutakyamirwa, aliwaambia wajumbe hao wa kamati ya siasa mkoani humo kwamba changamoto iliyosababisha usikamilike kwa wakati ni kuchelewa kwa msamaha wa kodi kutoka Wizara ya Kilimo.

 “Sababu kubwa iliyosababisha tuchelewe kumaliza mradi ni kuchelewa kwa msamaha wa kodi kutoka Wizara ya Kilimo wakati tunasaini mkataba msahaha kutoka wizarani ukawa haujatoka  ikabidi tusubiri zaidi ya miezi miwili lakini  tukawa tayari tumeishaingia mkataba wa ujenzi hiyo ndiyo sababu kubwa iliyotufanya tuchelewe kumaliza mradi kwa wakati,” alisema Mhandisi Rutakyamirwa.

Mbali ya mradi huo katika Halmashauri ya Buchosa kamati hiyo pia ilitembelea na kukagua mradi wa maji uliojengwa Kijiji cha Kamisa kwa gharama ya Sh milioni 220 ambao umekamilika kwa asilimia 100,  ambao utawanufaisha wananchi 4,000.

Mradi mwingine ni ujenzi wa barabara ya Bukokwa- Sukuma na Nyashana kwa kiwango cha changarawe utakaogharimu zaidi ya Sh milioni 373 unaotarajiwa kukamilika Mei 10, mwaka huu.

Katika Wilaya ya Sengerema kamati hiyo ilitembelea na kukagua ujenzi wa miundombinu shule tarajali za Sekondari ya Ibondo utakaogharimu zaidi ya Sh milioni 140 unaotarajiwa kukamilika Mei 13, mwaka huu.  ujenzi wa jengo la huduma za dharura linalojengwa Hospitali ya wilaya hiyo kwa gharama ya Sh milioni 44.95 ujenzi wa kituo cha Afya Ngomamtimba kilichopo Kata ya Kafunfu kitakachogharimu Sh milioni 250 ambapo wanufaika ni wakazi 32, 804.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles