25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Ndumbaro mgeni rasmi Siku ya upandaji miti na misitu Kitaifa

Na Clara Matimo, Mwanza

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk.Damas Ndumbaro, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya  siku ya upandaji miti  na misitu duniani kitaifa yatakayofanyika Wilaya ya Magu mkoani Mwanza Machi 21, mwaka huu.

Hayo yamebainishwa jijini hapa Machi 19, na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu maadhimisho hayo ambayo lengo ni kuwambusha na kuwahamasisha wananchi umuhimu wa upandaji na utunzaji wa miti kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa bidhaa na huduma za misitu nchini, umuhimu wa kuendelea kutunza na kuhifadhi misitu kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel.

Mhandisi Gabriel amewataka wananchi, taasisi za Serikali, binafsi na wadau wa misitu mkoani Mwanza kushiriki kikamilifu kwenye maadhimisho hayo ili wapate elimu juu ya faida ya misitu, uhifadhi na upandaji miti pia waendelee na juhudi za upandaji miti, uhifadhi wa misitu ili kuiwezesha jamii kunufaika na bidhaa pamoja na hudama za misitu endelevu maana misitu ni uchumi.

Amesema katika kuadhimisha siku hiyo, shughuli mbalimbali zitafanyika Wilayani Magu ikiwemo upandaji miti katika Shule ya Msingi Sagani iliyopo Kata ya Kandawe Tarafa ya Itumbili, maonesho ya bidhaa na huduma za misitu, chakula cha pamoja cha kimisitu ,michezo na kuwasilisha picha za misitu katika tovuti yaShirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa( FAO).

“Nawasihi wananchi, taasisi za serikali, binafsi na wadau wote wa misitu wa Mkoa wa Mwanza wafike Wilaya ya Magu Machi 21, mwaka huu ili tusherekee kwa pamoja siku hii muhimu kwa ustawi wa taifa letu, tutapanda miti shule ya Msingi Sagani kuanzia saa moja na nusu hadi saa mbili na nusu asubuhi baada ya hapo viongozi na wananchi wote tutaelekea uwanja wa Sabasaba ambako shughuli za maadhimisho zitafanyika,” amesema.

Amesema mkoa huo ulizindua kampeni ya upandaji miti Desemba 9, 2021 katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza ambapo kilele ilikuwa ni  Februari mwaka huu Manispaa ya Ilemela huku akibainisha kwamba jumla ya miti 3,237,871 ilipandwa kati ya hiyo miti 2,816,948 ilistawi sawa na asilimia 87 na miti 420, 923 sawa na asilia 13 ilikufa kutokana na changamoto mbali mbali ikiwemo ukame, mifugo, wadudu waharibifu, magonjwa na elimu ndogo ya umuhimu wa misitu kwa wananchi.

Amefafanua kwamba Tanzania ilianza kuadhimisha  siku ya upandaji miti kitaifa Januari Mosi mwaka 2000 ambapo aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awamu ya tatu, Hayati Benjamin Mkapa, alipanda mti wa milenia katika Kijiji cha Changanyikeni kilichopo karibu na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, hata hivyo serikali kupitia Waraka wa Ofisi ya Waziri Mkuu namba moja wa mwaka 2009 maadhimisho hayo yalibadilishwa na kuwa Aprili Mosi kila mwaka.

Maadhimisho ya siku ya misitu duniani yanatokana na Azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la mwaka 2012 ambapo liliagiza nchi wanachama kuadhimisha siku ya misitu duniani Machi 21 kila mwaka madhumuni yakiwa ni  pamoja na kusherekea,  kujenga uelewa juu ya umuhimu wa misitu ya aina yote kwa nchi husika na kuendesha midahalo yenye maudhui ya misitu na  mijadala kuhusu masoko ya bidhaa na huduma za misitu.

 Kauli mbiu ya maadhimisho hayo  mwaka huu ni ‘mti wangu, taifa langu mazingira yangu kazi iendelee na uzalishaji na matumizi endelevu ya misitu’.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles