25.8 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

CCM YA MAGUFULI KUFUNGA MKANDA UKAZE NA KAMBA

magufuliccm

NA EVANS MAGEGE

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), chini ya uongozi wa Rais John Magufuli kinajidhihirisha sasa kuingia kwenye mlengo mgumu zaidi dhidi ya maisha ya mazoea ambayo yametawala fikra za Wana-CCM kwa muda mrefu.

Inawezekana ugumu huo unaweza  ukatafsirika kama ni historia mpya inakwenda kuandikwa tangu kuzaliwa kwa chama hicho mwaka 1977.

Mtazamo wa ugumu huo unatokana na uhalisia wa mabadiliko ya hivi karibuni ambayo Mwenyekiti wa chama hicho, Rais John Magufuli, kayaleta akiwa na kusudio la kuboresha mifumo na kukata mizizi ya makandokando ya fitina ambayo kwa nyakati fulani yalitoa kiashirio cha kukidhoofisha kisiasa machoni mwa Watanzania.

Kwa mabadiliko ambayo ameyafanya Rais ndani ya CCM , kwa lugha nyepesi unaweza kusema kwamba amefumua muundo wa chama hicho.

Hoja hiyo inajijenga katika mabadiliko ya kupunguza idadi ya wajumbe wa vikao vya juu pamoja na kupunguza idadi ya vikao ndani ya chama.

Ni dhahiri kwamba uamuzi huo wa Mwenyekiti wa kufanya mabadiliko umetiwa baraka Jumanne ya wiki hii na wajumbe wa kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho(NEC), kilichoketi Ikulu ya Magogoni jijini Dar es Salaam.

Iko bayana kwamba Rais ameweka utaratibu huo ikiwa ni hatua mojawapo ya mabadiliko makubwa ambayo amedhamiria kukifanyia chama hicho ndani ya uongozi wake.

Pia, mtazamo huo unaishibisha hoja ya kuongeza ufanisi wa utendaji wa chama kwa maana ya kuongeza muda wa viongozi kufanya kazi za chama kwa umma, badala ya kutumia muda mwingi vikaoni.

Kwa tafsiri ya kawaida mabadiliko hayo ni sehemu ya matamanio makubwa ambayo Rais anataka kuyaona ndani  ya CCM mpya anayoiongoza hadi mwaka 2022.

Kimantiki mabadiliko hayo makubwa ambayo baadhi yanahusisha kanuni na miongozo, yameanza mara moja na yale yanayohusisha Katiba ya CCM yatapata idhini ya Mkutano Mkuu  wa chama hicho utakaoitishwa Februari mwakani.

Na kwa uhalisia sehemu ya mabadiliko hayo imegusa wana-CCM katika mtazamo chanya na hasi. Kwa mfano kitendo cha kupunguzwa kwa wajumbe wa NEC  kutoka 388 hadi 158 kitakuwa kimewaangusha wengi hasa wale waliokuwa wanajipanga kwa ajili ya uchaguzi wa ndani ya chama hicho unaofanyika mwakani.

Si hivyo tu, hata uamuzi wa kupunguzwa kwa wajumbe wa Kamati Kuu (CC) kutoka 34 hadi 24, wajumbe wa kamati za siasa za mikoa wamepunguzwa watatu wakati wilayani wameondolewa wanne pamoja na kufutwa kwa vyeo vya makatibu wasaidizi wa wilaya, mikoa na mchumi wa wilaya na mkoa nao ni pigo kwa Wana-CCM .

Muktadha wa mabadiliko hayo unaleta muundo mpya ndani ya vikao vya juu vya chama, kwamba NEC itakuwa na wajumbe 158 tu, kutoka wajumbe 388 ambao tumezoea kuwaona. Ndani ya idadi hiyo nafasi za wabunge zitakuwa tano badala ya 10 zilizozoeleka.

Dalili za mambo zinatanabaisha kwamba mabadiliko hayo yamezingatia hesabu na uzito wa kutoa maamuzi ya ngazi za juu ndani ya chama.

Kwamba si lazima sana kuwa na idadi kubwa ya wajumbe wa maamuzi kama mkutano wa hadhara kwa sababu hata idadi ndogo inaweza kutoa maamuzi ya msingi na yenye kukipeleka mbele chama.

Pamoja na maumivu ya mabadiliko, lakini ukweli unabaki palepale kwamba kuifumua CCM, kulikuwa hakuepukiki kwa sababu mazingira ya kulaumiana, kupigana fitina, usaliti, tuhuma za ufisadi na kuendeleza makundi ya urais kumechangia kwa kiasi kikubwa kupausha siasa za chama hicho.

Ni tumaini la wengi  kwamba baada ya NEC kubariki mabadiliko magumu na yenye uchungu kwa baadhi ya wanachama, dira mpya ya mwelekeo wa CCM anayoitaka Rais Magufuli inaweza kukita kwenye mstari wa mwanzo wa mwisho wa siasa za majitaka ambazo zimekigharimu chama ndani ya miaka ya hivi karibuni.

Pia, tafsiri ya dhamira ya mabadiliko ya Rais Magufuli ndani ya CCM ni dhahiri kwamba ni magumu kuzoeleka ingawa ni lazima yakubalike kwa afya ya chama hicho ambacho tathimini ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana inaonyesha wazi kwamba kilishuka vibaya kwa kuambulia asilimia 58 ya kura zilizopigwa.

Mazingira na matokeo ya uchaguzi huo yanakilazimu chama hicho kijifunza mengi na magumu kiliyoyapata wakati wa mchakato na kampeni na urais, ubunge na udiwani.

Hivyo CCM mpya iliyo chini ya Rais Magufuli ilikuwa lazima ifanye mabadiliko makubwa, na huu ni ujumbe kwa wana-CCM kwamba usipoyakubali mabadiliko ndani ya uenyekiti wa Magufuli ni bora urudi utotoni ujifunze kutembea, na kama ukishindwa kutembea basi utasaidiwa kubebwa mgongoni.

Na kama utakuwa mbishi mithili ya  kuota pembe kama mnyama basi sitashangaa kuiona CCM hii mpya ya Magufuli ikikuwekea mkia ili ujulikane kwa uwazi kuwa kimwili upo CCM lakini nafsi yako upinzani.

Kama utakubali mabadiliko kuhimili mikikimikiki ya dira mpya ambayo Rais amedhamiria kuitumia katika kuipeleka CCM mbele ni bora ufunge mkanda mapema na ukaze na kamba maana picha iliyowazi CCM ya Magufuli itakuwa ngumu kuitumikia kama huna uadilifu.

Mazingira hayo yanazaliwa kwa picha ya vipaumbele 10 ambavyo Rais aliviwasilisha mbele ya wajumbe wa NEC. Hoja zinazojenga vipengele hivyo zinajikita katika kuwaambia wana –CCM  ukweli mchungu wenye nia ya kukiponya chama ili kiendelee kumudu ushindani wa siasa za vyama vingi nchini.

Vipaumbele hivyo ambavyo alivinadi kama  sehemu tu ya mambo mengi ambayo amedhamiri kuyatekeleza kwa maendeleo ya chama, kwa kiasi kikubwa vinatoa tafsiri ya shubiri maisha ya mazoea ambayo yaliwanufaisha baadhi ya wana CCM na si chama.

Kipaumbele cha kuimarisha chama katika ngazi zote pamoja na jumuya zake. Muktadha wa kipaumbele hicho unaleta picha ya kuijenga CCM  yenye uwezo wa kuisimamia serikali na kutetea wanyonge.

Pia hoja kama za kukiondoa chama katika mtazamo wa chama legelege cha walalamikaji kwamba kisimame kama chama tawala chenye kuiwajibisha serikali iliyopo madarakani.

Inawezekana Rais anania njema ya ufanisi wa serikali yake kupitia nguvu ya CCM, lakini ni kweli Wana-CCM wako tayari kuisimamia Serikali?

Swali hilo linajengwa kwa mtazamo wa picha  ya kwamba unafiki ambao umekuwa ukiwaficha kichakani  Wana-CCM kwa kushindwa kusema ukweli au kukemea madudu na badala yake hugeuka bubu na wakali wanapokosolewa.

Kwa kuwa Rais ameonyesha nia katika hoja hiyo, labda mabadiliko ya kifikra yatawaamsha wanachama na kuamua kuisimamia serikali kwa dhati.

Kipaumbele cha kuongeza idadi ya wanachama. Kinaashiria ushindani na nguvu mpya ya kisiasa katika siasa za nchi hii. Pia Rais Magufuli amedhamiria kwamba chama kiwe na wanachama hai wengi kutoka kundi la vijana.

Aidha, tafsiri nyingine ya hoja hiyo ni kukomesha tabia ya kuingiza wanachama hewa ndani ya chama nyakati za changuzi.

Rushwa ndani ya chama ni kipaumbele kingine ambacho Rais amenuia kupambana nayo ndani ya CCM. Kupitia hoja hiyo atakuwa na kazi ya kuhakikisha chama kinapata wananachama waadilifu na wenye uzalendo na chama kuliko wachumia tumbo.

Kuhusu kipaumbele cha CCM kujitegemea kiuchumi. Inawezekana Rais atakuwa na jukumu la makusudi la kufuatilia kwa ukaribu mali na chama.

Na kama atafanikiwa katika hilo, ni hakika atakiondoa chama katika mtindo wa kusubiri ruzuku ya serikali na kutegemea watu binafsi ambao kwa namna moja au nyingine hupenyeza maslahi yao ndani ya chama na kuipa wakati mgumu serikali kuwabana pindi wanapokuwa na makosa.

Inawezekana hoja hii ikawa chungu kwa wengi ambao walizoea kujinufaisha kupitia mali za chama. Rais ameweka wazi nia yake ya usimamizi wa vyanzo vya uchumi wa chama.

Kimaumbele kingine ambacho Rais Magufuli anaonyesha kwenda kuwanyosha wana-CCM ni kile cha usaliti na makundi  ambapo amedhamiria kukomesha tabia hizo ndani ya uongozi wake.

Kupitia hoja hiyo Rais anaamini kunabaadhi ya wanachama hukisaliti chama hasa nyakati za uchaguzi na wengine huendeleza makundi hata  kama uchaguzi umepita. Anaamini tabia hizo zinakidhoofisha CCM.

Kipaumbele kingine ni kuimarisha chama kwa wanachama wa chini. Dhamira ya Rais kufanya hivyo ni kuondoa muundo wa chama kuboresha mfumo wa uongozi wa juu na kutumia fedha nyingi kwa viongozi hao badala ya fedha hizo kupelekwa chini kuimarisha wanachama wengi.

Kipaumbele kingine ni uzingatiaji wa kanuni za uchaguzi hasa kumfanya kiongozi kutumikia cheo kimoja badala ya viwili.

Viongozi wa chama na wanachama wawe wanazingatia katiba ya chama, kuondoa vyeo ambavyo havijatamkwa kwenye Katiba .

Kipaumbele  cha kutaka CCM kuongozwa na wanachama badala ya mwanachama aongoze chama kina kishindo kikubwa cha kuwaangusha watu wenye tamaa za madaraka.

Hoja hiyo kama ikifanikiwa itakiondoa chama katika viganja vya mafisadi, wala rushwa ambao fedha zao zilikuwa zinaashiria kukiongoza chama kama fimbo. Badala ya chama kuongozwa kwa mawazo huru ya wanachama.

Mantiki ya chama hufuatwa na wanachama badala ya chama kufuata wanachama, ni dhahiri hoja hii ikisimamiwa ipasavyo itazika maisha ya unafiki na fikra za kutegemea makundi ndani ya chama kujinufaisha.

Kwa maoni

-0718814926

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles