27.5 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

WAPO NA WENGINE SI DANGOTE TU

Aliko Dangote, President and CEO of Nigeria's Dangote Group speaks during the final session of the World Economic Forum

Na Markus Mpangala

NAANDIKA safu hii nikiwa safarini mkoani Ruvuma katika Kijiji cha Amanimakolo kilichopo Wilaya ya Mbinga.

Eneo la Amanimakolo ndicho kiini cha makusanyo ya makaa ya Mawe chini ya mwekezaji wa Kampuni ya Uchimbaji wa Makaa ya Mawe ya TANCOAL, eneo hilo kuna malori mengi yanayochukua makaa ya mawe kwa ajili ya usafirishaji.

Nimeshuhudia takribani malori 30 yakiwa yameegeshwa na mizigo ya makaa ya mawe huku mengine yakiwa yanafanyiwa matengenezo.

Baadhi ya malori yalikuwa yakiingia kijiji humo na mengine yakiwa yanatoka eneo la machimbo katika vijiji kikiwamo Ruanda na Liyombo.

Nilichokiona ndicho kimenipa maswali lukuki.

Mosi; Hivi kiburi tunachoonyesha kwa rasilimali zetu dhidi ya wawekezaji kinawasaidia vipi wao na sisi kama wamiliki? Mfano, katika Kijiji cha Amanimakolo ndipo ilipo kambi ya usafirishaji kuna hali ni mbaya. Barabara inayotegemewa mbovu sana hata malori yanapishana kwa shida.

Nimejiuliza ni kwanini serikali haitoi kipaumbele kwa maeneo kama hayo kuweka miundombinu yenye tija na kurahisisha usafirishaji wa makaa hayo?.

Ndiyo kusema wakati serikali na Watanzania tumejaa kiburi kwa rasilimali zetu lakini hatuweki mkazo katika ujenzi wa barabara.

Barabara ya Amanimakolo ipo katika kiwango duni naamini inarudisha nyuma shughuli za uwekezaji. Mwekezaji gani atavumilia barabara mbovu kama hizi? Katika maeneo hayo barabara huharibika zaidi pale mvua za masika zinaposhika kasi.

Wakati tukipita eneo hilo tulilazimika kusota kwa muda wa saa moja ili kusubiri lori la TANCOAL liweze kunasuliwa kwenye tope. lori hilo lilinasa kutokana na mvua ndogo zilizonyesha na kusababisha utelezi na matope barabara nzima.

Matokeo yake kulikuwa na malori 6 ambayo yalikuwa yakiondoka eneo hilo lakini yalikwama kutokana na hali mbaya ya barabara. Malori mengine yalikuwa yakiingia kijijini hapo baada ya kusafirisha makaa hayo, yalilazimika kusubiri unasuaji.

Aidha, kulikuwa na mabasi ya abiria matatu yaliyokuwa yakielekea Mji wa Lituhi wilayani Nyasa, nayo yalisota eneo hilo kusubiri unasuaji wa malori.

Mwandishi wa safu hii ameona kasoro nyingi za miundombinu hali isiyoweza kuvumilika.

Tunafahamu kuwa serikali inapiga mbiu ya kukaribisha wawekezaji katika rasilimali zetu. Tunafahamu zipo juhudi za kuhakikisha rasilimali hizo zinawanufaisha Watanzania kote nchini.

Licha ya kuyafahamu hayo tunatakiwa kujisikia aibu pale wawekezaji wanapofanya shughuli zao katika mazingira magumu.

Ni jambo la fedheha unapokutana na wafanyakazi wa malori hayo wanavuja jasho na kuhangaishwa kwa ajili ya ubovu wa barabara. Ilitarajiwa kuona kuwa serikali inajenga barabara zote zinazopita kwenye machimbo kama haya.

Pia serikali ingerahisisha shughuli za wawekezaji ili kuongeza ufanisi pamoja na kuvumbua fursa mpya zinazotokana na makaa ya mawe.

Bahati mbaya kama ilivyo kasumba zetu, tunajionea ubovu wa barabara hizo kama santuri ya muziki itoayo burudani na kuishia kutabasamu. Ninaamini kabisa TANCOAL hawajatendewa haki.

Kwa mfano, kama tunakubaliana na bilionea wa Naigeria ambaye ni mmiliki wa Kiwanda cha Saruji, Aliko Dangote kupewa eneo la kujenga bandari, viweje tushindwe kutoa kipaumbele kwa wawekezaji wengine kwenye miundombuni? Ikumbukwe Kijiji cha Amaninakolo hakina umeme.

Hakijapata mradi wa umeme vijijini (REA),  wakazi wa eneo hilo wanaishia kuzitazama nguzo zilizosimikwa katika Kijiji cha Kitai, huku wakiwa wamebaki na matumaini labda ipo siku watapatiwa umeme.

Nilitarajia kuona maeneo ya wawekezaji kama hayo yanapewa umuhimu wa kutosha ikiwemo kupatiwa nishati ya umeme.

Ipo desturi kuwa maeneo yenye nguvu kiuchumi huletewa huduma za nishati za umeme haraka mno. Lakini mazingira yaliyopo katika kijiji hicho hayasadifu kuwa kuna mipango ya haraka uliopewa kipaumbele cha ujenzi wa nishati ya umeme.

Uhakika nilionao ni kwamba utengenezwaji wa Barabara ya Mbinga (kuanzia eneo la Kitao) kwenda Lituhi itachangia mabadiliko makubwa ya huduma na kuchochea uchumi.

Ikumbukwe maeneo yote yaliyopitiwa na barabara hiyo yana fursa za misitu, uchimbaji wa madini na shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Ninafahamu Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira , January Makamba amepata kufanya ziara katika maeneo hayo.

Suala nyeti aliloshuhudia ni barabara mbovu inayodhoofisha shughuli za uchumi na ufanisi wa TANCOAL pamoja na wananchi wa pembezoni ambao wamebakiwa na matumaini ya maisha bora pasipo uhalisi.

Nihitimishe kwa kuuliza tena, hivi kiburi chetu dhidi ya wawekezaji kina maana gani ikiwa hata kuwatekelezea mambo muhimu kunatupiga chenga?

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles