25.5 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

CCM, wapinzani kupimana ubavu kata tatu

LEONARD MANG’OHA, DAR ES SALAAM

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kinatarajiwa kupata upinzani katika kata tatu kati ya 48 zitakazofanya uchaguzi mdogo Januari 19, mwakani.

Kata ambazo vyama vya upinzani vimeonesha nia ya kushiriki uchaguzi huo wa marudio ni Mwanahina, Wilaya ya Meatu mkoani9 Simiyu, Biturana, Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma na Kata ya Magomeni, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili juzi, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dk. Athumani Kihamia, alisema awali katika Kata ya Magomeni mgombea wa CCM, Shaweji Mkumbura alipita bila kupingwa baada ya mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF), Athumani Yusuf kuwekewa pingamizi kuwa si raia wa Tanzania.

Katika Kata ya Mwanahina mgombea wa CCM, Nawinda Jibunge, atachuana na mgombea wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Ng’wigulu Anthony, Sosi Mbonane (TLP) na Simike Magida (ACT-Wazalendo).

Katika kata ya Biturana, mgombea wa CCM, Barnabas Baranzila atakabiliana na Jeremiah Makere (Chaumma) na Vedasto Kamhanda (CUF).

“Tangu tulipotoka katika Uchaguzi Mkuu 2015, tumefanya chaguzi nyingi ndogo, kumekuwa na malalamiko, mara nyingi watu huamini rufaa za wapinzani hazisikilizwi.

“Hata ukiangalia katika uchaguzi huu utakaofanyika Januari 19 wagombea wengi wa CCM wamepita bila kupingwa isipokuwa mmoja wa Kinondoni (Kata ya Magomeni) ambaye alikata rufaa na lile pingamizi alilokuwa amewekewa likatenguliwa na tumemrudisha kwenye mchakato,” alisema Dk. Kihamia.

Alisema pamoja na malalamiko mengi yanayotolewa na viongozi wa vyama vya upinzani kuwa hawatendewi haki, wengi wao hawakati rufaa ama kutoa taarifa sehemu husika.

Dk. Kihamia alisema licha ya kuwapo kwa malalamiko mengi kuhusu tume hiyo kutokuwa huru, wamekuwa wakipata sifa nyingi wanapohudhuria mikutano mbalimbali ya kamisheni za uchaguzi barani Afrika.

“Ibara ya 74 ya Katiba ya mwaka 1977, imeitaja tume hii kama tume huru, hata sasa hivi Waziri Mkuu hawezi kuniita na kuniambia tunataka ufanye hivi, labda kama na mimi mwenyewe nina ukada wangu.

“Ndiyo maana hata wenzetu wa mataifa mengine ya Afrika wanakiri kuwa Katiba yetu haijaacha kitu katika maandishi,” alisema Dk. Kihamia.

Taarifa ya Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Semistocles Kaijage iliyotolewa hivi karibuni, ilieleza kuwa kata 46 kutoka halmashauri 28 na mikoa 14 ya Tanzania Bara zinatarajia kushiriki uchaguzi huo.

Kata hizo ni Sale, Misigyo, Malambo, Orgosorok, Olorien/Magaiduru, Kimnyak (Arusha), Kiranjeranje, Kikole, Pande Mikona, Kichonda, Mlembwe (Lindi), Dareda, Magara, Makame, Loiborsiret, Ruvu Remit na Naberera (Manyara).

Mkoani Mwanza ni Kwimba, Walla na Nyampulukano, mkoani Morogoro ni Msogezi, Mtibwa, Tchenzema, Mangae na  Magomeni wilayani Kilosa.

Nyingine ni Keko, Magomeni (Dar es Salaam), Kitanga Kigondo, Msambara na Mnyegera (Kigoma), Buhendangabo, Nyakato, Kikomelo, Kanyigo na Nyamiaga (Kagera).

Pia zipo kata za Utiri, Mpitimbi, Ilolo, Hasanga na Ihanda (Ruvuma), Nanhyanga na Namikupa (Mtwara), Makulu (Dodoma ), Geitasamo (Serengeti Mara) na Nkundwabiye na Nyangokolwa (Simiyu).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles