24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

JKCI yapunguza wagonjwa wa moyo wanaotibiwa nje

VERONICA ROMWALD -DAR ES SALAAM

KUIMARIKA kwa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kumewezesha wagonjwa wote kutibiwa nchini na hakuna aliyepewa rufaa kwenda kutibiwa nje ya nchi.

Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam juzi na Mkurugenzi wa Idara ya Magonjwa ya Moyo wa JKCI ambaye pia ni Bingwa wa Magonjwa ya Moyo, Dk. Peter Kisenge.

Alisema hayo ni mafanikio makubwa kwa taasisi hiyo kwa sababu imesaidia kuokoa fedha nyingi za Serikali ambazo hutumika kugharamia matibabu kwa wagonjwa wanaopelekwa nje ya nchi.

Dk. Kisenge alisema mafanikio hayo yamefikiwa kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa katika taasisi, hasa kuwekewa vifaa vya kutosha vya kisasa vinavyohitajika kwa matibabu ya moyo pamoja na wataalamu.

“Wagonjwa waliokuwa wakipelekwa nje ya nchi kwa matibabu kwa gharama za Serikali wamekuwa wakipungua mwaka hadi mwaka tangu kuanzishwa kwa taasisi hii,” alisema.

Pia alisema kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017 wagonjwa wa moyo waliopelekwa nje ya nchi walikuwa 17 tu na kila mmoja aliigharimu Serikali zaidi ya Sh milioni 30 za matibabu.

Alisema kwa sasa taasisi hiyo imekuwa na jina kubwa kutokana na matibabu ya kibingwa yanatolewa na wamekuwa wakitibu wagonjwa wa ndani na nje ya nchi.

“Tunaaminika Afrika, hasa ukanda wa Mashariki na Kati, tunapokea wagonjwa kutoka nje ya nchi, hii ina maana kwamba wana imani na huduma zinazotolewa.

 “Jana (juzi) tu nimemuona mgonjwa kutoka Misri, hata kama hakutoka huko kuja hapa nchini kwa matibabu, pengine ameugua akiwa hapa, hii inatupa picha kwamba hayo mataifa yana imani na sisi,” alisema.

Alisema taasisi hiyo hivi sasa inapokea wagonjwa wa nje (out patients) 300 kwa siku, wagonjwa 10 hadi 15 ni wa rufaa na wagonjwa wawili kati ya hao ni kutoka nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Pia alisema JKCI inatoa mafunzo kwa madaktari mbalimbali na kwa mwaka madaktari wapatao 20 wanapata mafunzo katika taasisi hiyo.

Dk. Kisenge alisema hakuna mgonjwa anayefika na asipatiwe huduma, na wagonjwa wote wanatibiwa bila kujali hali zao kifedha.

 “Gharama zetu ni za kawaida, lakini hakuna mgonjwa atakosa huduma, tuna wale ambao hawawezi kugharamia matibabu, lakini nao tunawahudumia,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles