Safina Sarwatt, Moshi
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi, amewaonya viongozi wa chama hicho kuachana tabia kuwa na wagombea mifukoni katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa.
Boisafi ameyasema hayo leo Ijumaa mjini Moshi, wakati wa maadhimisho ya miaka 42 ya CCM ambapo chama hicho kilishiriki kufanya usafi katika Hospitali ya Mawenzi na kupanda miti pamoja na kusikiliza kero za wagonjwa na wauguzi wa afya.
“Yapo mambo ya msingi ambayo chama kinapaswa kuyafanya ili kiendelee kushika dola kuanzia ngazi za vijiji na kata, ni wakati wa viongozi wa chama kuachana na kuwa wagombea wa mifukoni ambao hawakubaliki kwa wananchi.
“Tunaelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa ndugu zangu viongozi, jengeni dhana ya upendo, simamieni haki kwa wanachama wote ambao wana sifa ya kugombea wapeni nafasi, hizi ni zama za ukweli na uwazi msifanye mambo kwa kificho,” amesema.
Pamoja na mambo mengine, mwenyekiti huyo amesema yeye binafsi hana mtu mfukoni ambapo ametaka kila mmoja apate haki na siyo kuvaa mashati ya kijani lakini wanafanya mambo ambayo hayaendani na dhana halisi ya CCM huku akisisitiza kanuni na sheria na taratibu za chama ziko wazi.