Na PETER FABIAN,
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza kimewavua uanachama na kuwafukuza makada wake 100 akiwamo aliyewahi kuwa Meya wa Jiji la Mwanza, Leonard Bihondo na mkewe Veronica Bihondo.
Watu hao wanadaiwa kukisaliti na kuhujumu chama katika uchaguzi mkuu uliopita.
Hatua hiyo ilitangazwa juzi katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Mwanza baada ya vikao ngazi ya chini pia kufikia uamuzi huo.
Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM wa Mkoa, Saimon Mangelepa, alisema uamuzi wa kuwavua uanachama na kuwafukuza kwenye chama ulianza kujadiliwa na kutolewa uamuzi kuanzia ngazi ya matawi, kata, wilaya na mkoa.
“Kwa mujibu wa Katiba ya CCM ya mwaka 1977 na toleo la mwaka 2012 Ibara ya 93 (14)- (15) leo wajumbe wametoa baraka zote na kuazimia kutekelezwa adhabu hiyo kwa baadhi ya wanachama waliobainika kukisaliti chama kwenye uchaguzi mkuu 2015,”alisema.
Mangelepa alisema makada na wanachama waliovuliwa na kufukuzwa ni pamoja na Meya wa zamani wa Jiji la Mwanza, Bihondo ambaye anatoka Kata ya Isamilo, Wilaya ya Nyamagana.
Aliwania kugombea udiwani na kushindwa kwenye kura ya maoni ndani ya chama lakini anadaiwa alihusika kumsaidia mgombea wa upinzani na kuishinda CCM.