*Wasema hoja zake hazina mshiko
Na Ashura Kazinja, Morogoro
Katibu wa Siasa, Uenazi na Mafunzo Mkoa wa Morogoro, Zangina Shanang amejibu hoja tano zilizotolewa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu na wenzake katika mkutano wa hadhara uliofanyika Aprili 30, mwaka huu mkoani Morogoro na kusema kuwa hoja hizo ni za upotoshaji.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Morogoro Mei 8,2024 Shangina amesema hoja ya Tundu Lissu na wenzake kuhusu uwepo wa Serikali ya tatu ya Tanganyika ambayo ni TAMISEMI kwa kuwa ni Taasisi isiyo na muungano, haina mashiko kutokana na TAMISEMI kuwa wizara kama zilivyo wizara nyingine nchini.
“Ajenda hii ya serikali ya tatu ya Tanganyika inalazimishwa ionekane ni hitaji la wananchi ilihali ni mpango wa Chadema wa kuongeza utitiri wa madaraka na kuitumia kujiimarisha kisiasa na kisha wauvunje muungano kwa kuwa wamejawa na roho ya kuibagua Zanzibar. Chadema waache utoto wa kulazimisha serikali ya Tanganyika itakayoongeza mzigo kwa Watanzania,” amesema Shanang.
Amesema hoja ya pili ya Tundu Lissu na wenzake inayohusu ardhi na fursa za kazi za Zanzibar kupewa kipaumbele Wazanzibari kupitia katiba na sheria za Zanzibar zinalenga kupotosha umma.
“Tanzania Bara tupo milioni 61.7 kiidadi huku Zanzibar ikiwa na watu miilioni 1.8 na fursa zao za kazi bado ni chache, hivyo sisi wabara tukipeleka ushindani wa kuzitaka ajira chache za watu mil ilioni 1 itakuwa ni ubakaji wa fursa hizo chache.
“Upande wa ardhi bara tuna kilometa za mraba 945,000 ilhali Zanzibar kuna kilometa za mraba 1,650, kwa takwimu hizo ni wazi unapata picha watu wa bara tukienda kuivamia ardhi ya Zanzibar kwa idadi yetu kubwa itakuwa ni ubakaji wa ardhi ya Zanzibar,” amesema.
Aidha, amesema hoja ya Lissu na wenzake inayohusu migogoro ya ardhi kuchochewa na uondoaji wa wafugaji kwenye hifadhi za wanyama haina maana kutokana na migogoro hiyo kuongezeka kadri watu na mifugo wanavyoongezeka, hivyo kiwango cha uvamizi wa maeneo ya malisho na makazi kimeongezeka.
Pia akijibu hoja ya nne ya kwamba Chadema wanaandamana ili kushinikiza katiba mpya haraka iwezekanavyo kabla ya kuingia kwenye chaguzi, amesema jambo hilo siyo la kukurupuka kwani lazima mchakato wake ufanywe kwa utulivu mkubwa na umakini uliotukuka, ikiwemo wananchi kupewa elimu ili wajue namna ya kuwasilisha wanachokitaka ili kiingie kwenye katiba mpya.
“Hoja ya tano ya Lissu na wenzake inayodai kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kagoma kutekeleza maridhiano ya vyama vya upinzani, hili nalo siyo kweli kwani baada ya vikao na vyama vya siasa, Rais Samia alifungulia vyombo vya habari vilivyokuwa vimefungwa, alirejesha amani ya kisiasa na hata kuimarisha ulinzi na amani.
“Pia amekomesha tabia za kuenguliwa kwa wagombea wa upinzani na swala la kupita bila kupingwa na amefungulia na kuruhusu mikutano ya kisiasa ambayo ilikuwa imezuiwa,” amesema Shanang.