JOSEPH HIZA
MTAWALA wa Kike wa Cornwall nchini Uingereza, Camilla Parker Bowles amekuwa haishiwi na kashfa hasa zinazomtazama kama mwanamke mbinafsi mwenye roho ya korosho, chuki, wivu na husda.
Analaumiwa si tu kuisambaratisha ndoa ya kwanza ya mumewe, Prince Charles na aliyekuwa kipenzi cha wengi, Princess Diana bali pia kifo cha mtawala huyo wa kike wa Wales mwaka 1997.
Uhusiano wake na Prince Charles ulianza tangu mwaka 1972 na uliendelea kwa siri hata pale walipoingia ndoa na watu tofauti; Camilla akiwa na mjeshi mmoja hivi, Charles na Diana.
Licha ya kufanikiwa kumpata Prince Charles aliendeleza chuki kwa mke wa mwanae wa kambo Prince Williams, Mtawala wa Kike wa Cambridge, Kate Middleton, tangu alipomtupia jicho kwa mara ya kwanza miaka 15 iliyopita.
Wakati Parker Bowles (68), alipokutana mara ya kwanza na Middleton (36) wakati urafiki wake na Prince Williams wakati wa enzi zao katika Chuo Kikuu cha St. Andrews, alimpa uzito maalumu.
Middleton alishukuru kwa wema na ukarimu aliofanyiwa naye na alimsimulia mama yake Carole namna alivyokirimiwa na Camilla katika moja ya shughuli za ukoo wa kifalme.
“Ni mcheshi mno na aina ya mama mwema,” Middleton anasemekana kuwaambia wazazi wake, pasipo kujua nini kinaendelea moyoni mwa Camilla.
Ndivyo ilivyokuwa, kwani nyuma ya pazia, Parker Bowles alikuwa anakula njama za kuwatenganisha na kumchagulia mwanae huyo aina ya mwanamke kama alivyodai ‘mrembo na wa hadhi zaidi’.
Hivyo, tangu hapo Camilla alifuatilia kwa karibu nyendo za penzi hilo changa ikiwamo kutuma mashushushu kufuatilia na hata kuangalia uwezekano wa kuingiza sumu kulivuruga.
Alitoa sababu kadhaa za kumkataa Middleton, mbali ya malezi kutoka familia ya kawaida, hakupendezwa na tabia ya mama yake, Carole ya uvutaji sigara na nyinginezo.
Kuhusu haiba ya Middleton alikiri yu ‘mzuri’ lakini ‘aliyefifia’ au kutokuwa ‘mwanamke wa maarifa,” anaripotiwa kumtoa dosari.
Lakini ukweli ni kwamba yote hayo ni chuki tu zinazotokana na wivu. Camilla hakutaka awepo ‘mtu baki’ ampiku umaarufu na hata uwezekano kuchuana naye katika kiti cha umalkia.
Na hivyo haikushangaza alipompiga marufuku Middleton kuhudhuria arusi yake na Prince Charles mwaka 2005, kwa mujibu wa habari za ndani.
Baada ya kufanikiwa kuingia katika ndoa na kipenzi chake hicho cha tangu ujanani, ukizingatia wote walishatengana na wenzi wao wa awali, Camilla aliongeza mashambulizi kuhakikisha Kate haingii katika ukoo wao huo.
Kama mama wa kambo, anatuhumiwa kumshawishi William kumtosa rafikiye huyo aliyedumu naye miaka sita mwaka 2007 akiukosoa ukoo wake kutoendana na wa kifalme.
Wakati kashfa ya familia ya akina Middleton ilipovuja— mjomba wake Gary akituhumiwa kutumia dawa za kulevya — Parker Bowles alipata nguvu zaidi na kumshikia sikio mumewe Charles.
Ikumbukwe Charles hakuwa na sauti mbele ya mkewe huyo na wakati huo huo hakuona ubaya wa uhusiano baina ya mwanae na akina Middletons.
Lakini kutokana na ushawishi wa mkewe, Charles alitimiza matakwa ya mkewe na hivyo William akatengana na Kate mwaka 2007.
Haikuchukua muda baada ya mtengano huo, magazeti ya udaku yakajaa na picha na habari chafu kumhusu Kate, nyingine zikimwonesha akicheza katika vilabu vya usiku akiwa na dada yake Pippa huku wakiwa wamevaa viwalo kama vile sketi fupi na za kubana.
Inasemekana Camilla alikuwa nyuma ya mikakati yote hiyo na vyombo hivyo vya habari.
Lakini katika kuonesha kuwa walishibana, wiki sita baadaye Will na Kate wakarudiana na umma wa Uingereza ukavutiwa na msichana huyo kutoka familia ya kawaida.
Wakati huo huo, Camilla aliendelea kutumia saa nyingi kufanya mikakati huku akivujisha taarifa za kweli na uongo kwa vyombo vya habari.
Licha ya hayo, Camilla si tu hakufanikiwa katika azma yake hiyo bali pia amebakia kutopendwa na watu wa kawaida pamoja na Malkia Elizabeth II mwenyewe hadi leo hii.
Prince William akamuoa Middleton April 29, 2011 na sasa wawili hao wana watoto wawili: Prince George (miaka 2) na Princess Charlotte, miezi 11.
Licha ya roho mbaya Camilla aliyomfanyia Kate, yeye mwenyewe alipambana mno kuweza kuolewa na Charles kutokana na kupingwa kwa nguvu si tu na umma wa Waingereza bali pia ukoo wa kifalme kutokana na nyendo zake zisizofurahisha, kukosa mvuto na ‘alichomfanyia’ si tu Prince Diana bali pia mumewe wa kwanza.
Ukoo wa kifalme ulikuwa ukimshinikiza Charles kutomuoa Camilla, ambaye ameweza kujipenyeza katika ukoo huo kutokana na uhusiano wa nyuma wa babu yake na ukoo huo.
Iliwahi kufikia hatua ya kuwapiga marufuku watoto wa Camilla wapenda matanuzi Laura Lopes na Tom Parker Bowles kumkaribia kijana Prince William kwa hofu ya ‘kumwambukiza’ tabia mbaya.
Lakini mwishowe, malkia akasalimu amri kutokana na msimamo wa mwanae. Ilikuwaje?
Ili kuhakikisha ndoto yake ya kumuoa Camilla inatimia, Charles alimuahidi mama yake kuwa Camilla hatokuwa malkia wakati atakapotawazwa ufalme. Hilo la umalkia lilikuwa moja ya hofu iliyoujaa ukoo huo.
“Camilla hana mpango wala nia ya kuwa Mtawala wa Kike wa Wales sasa wala kuwa malkia hapo baadaye, Charles alisisitiza. “Wote mimi na Camilla tunahisi kuwa ni vyema nitakapokuwa mfalme, yeye abaki kama mtawala wa kike mfariji tu,” alimwambia mama yake.
Hivyo ukoo wa Kifalme ukatangaza kuwa licha ya ndoa hiyo, Camilla hatakuwa malkia. Hivyo wawili hao wakaoana mwaka 2005
Iwapo kweli Princes Charles atabakia na ahadi hiyo ya kutomfanya mkewe kuwa malkia, ni kitu cha kusubiri na kuona ukizingatia udhaifu wake kwa mkewe pamoja na nyendo zinavyojionesha sasa.
Camilla amekuwa akionesha kujipamba hadharani kama mke na mtumishi mwema, akionekana katika matukio yasiyo na idadi ya hisani na kuvaa mithili ya malkia. Na anapoulizwa swala la umalkia mara nyingi, Camilla hutabasamu na kusema; “Huwezi jua.”
Hata hivyo, ukweli ni kwamba ni sheria ya Bunge pekee ndiyo itakayozuia Camilla asitawazwe umalkia siku ile inakuja!.