26.9 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

Cameron arudi Downing Street kwa kishindo

david-cameron-and-wife-pic-dm-1043869LONDON, Uingereza
WAZIRI Mkuu wa Uingereza, David Cameron, anatarajia kuunda Serikali ya chama chake cha Conservative bila kuhitaji muungano au ushirikiano na vyama vingine tofauti na Serikali aliyokuwa akiiongoza kabla ya uchaguzi huu uliompa ushindi wa kishindo.
Hadi kufikia jana mchana matokeo yalikuwa yakionyesha kuwa chama chake kilikuwa kimeshinda viti 331 kati ya 635 ya matokeo yaliyokwisha patikana. Jumla ya viti vyote ni 650 na ili chama kiweze kuunda Serikali peke yake kinahitaji kuwa na viti 326.
Kwa matokeo hayo, Chama cha Conservative kimekiangusha Chama cha Labour ambacho kimejipatia viti 232 kati ya idadi hiyo.
Katika viti hivyo 331 ambavyo Conservative imejipatia, 29 vimeongezeka zaidi ukilinganisha na uchaguzi uliopita wakati Labour kikipoteza viti 24, Chama cha Liberal Democrat kikiambulia viti 8 na kupoteza 48, chama kikuu cha Scotland- Scottish National-SNP, kimefanikiwa kupata viti 58 na hivyo kupoteza kiti kimoja tu.
Conservative kinatarajia kupata asilimia 50 ya kura zote, Labour 31%, UKIP 13%, Lib 8%, SNP 5%, Green Party 4% na Plaid Cymru 1%. Tayari Lib Dems kina kura 8, SNP 56, Plaid Cymru 3, UKIP 1 na Greens 1.
Ushindi huo utamfanya Cameron kuunda Serikali ya chama chake pekee tofauti na utawala uliopita ambao ulikuwa na Serikali ya mseto na chama cha Liberal Democrat.
Cameron alinukuliwa akisema ataunda Serikali ya kihafidhina huku akimshukuru aliyekuwa Naibu wake katika Serikali iliyopita, Nick Clegg wa Chama cha Liberal Democrat, pamoja na Ed Miliband, aliyempigia simu asubuhi akimpongeza kwa ushindi huo.
Pia alisema suala la kura ya maoni juu ya kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya litaendelea.
Serikali itakayoongozwa na Conservative, itaendeleza shinikizo lake la kutaka Uingereza kuitisha kura ya maoni ya kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya ifikapo mwaka 2017.
Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa jana na gazeti la Daily Mail mtandaoni, Cameron alikwenda Buckingham kwa ajili ya kuonana na Malkia kabla ya kurudi Downing Street.
Aidha, Cameron ameibuka mshindi katika Jimbo la Oxfordshire. Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Cameron alisema ushindi huo umeufanya usiku kuwa mzuri kwa chama chake cha Conservative.
Wakati huo huo, kiongozi wa Chama cha Labour, Ed Miliband na mwenzake, Nick Clegg, walitangaza kujiuzulu nafasi zao ndani ya vyama vyao baada ya kushindwa katika uchaguzi huo.
Akizungumza baada ya kushinda katika jimbo la Doncaster, Kaskazini mwa Uingereza, Miliband amesema usiku wa kuamkia leo umekuwa mbaya kwa chama cha Labour, zaidi alisema chama chake kimesikitishwa na matokeo hayo.
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa nchini humo wamezungumzia ushindi wa chama cha Conservative kuwa pamoja na mambo mengine pia kwa kiasi fulani umechangiwa na mbinu ya kukigombanisha chama cha Labour na Wascotland.
Taarifa katika mitandao mbalimbali ya habari ukiwemo ule wa Daily mail na BBC zinaeleza kuwa Waingereza wengi wamepigwa na mshangao kwa matokeo hayo kwani yamekuwa tafauti na kura za maoni zilizofanyika kabla ya uchaguzi.
Kabla ya Waingereza kwenda kupiga kura Alhamisi, uchunguzi ulieleza hakuna chama kinachoweza kupata ushindi huku tumaini likiwa kwa chama cha upinzani cha Labour kuweza kupata ushindi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles