24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Chadema yaachiwa jimbo moja Z’bar

NA SARAH MOSSI, ZANZIBAR
UMOJA wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umeridhia Chama cha Wananchi (CUF) kusimamisha wagombea wake wa nafasi ya ubunge katika majimbo yote ya uchaguzi visiwani Zanzibar, isipokuwa katika Jimbo la Kikwajuni.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Makao Makuu ya CUF, Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Uchaguzi wa CUF, Omar Ali Sheikh, alisema Ukawa wamekubaliana katika Jimbo la Kikwajuni watasimamisha mgombea ubunge kutoka Chadema ambaye ni Salum Mwalimu.
Mwalimu ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), ambaye hata hivyo tangu ateuliwe amekuwa akifanya kazi zake Tanzania Bara.
Jimbo la Kikwajuni linaunganisha wakazi wa maeneo ya Kikwajuni Juu na Chini, Kisimamajongoo, Kilimani, Miembeni, Magereza na sehemu ya eneo la Michenzani.
Uamuzi wa Mwalimu kusimama kuwania ubunge Jimbo la Kikwajuni kupitia Chadema, umepokewa kwa hisia tofauti miongoni mwa wachambuzi wa siasa ndani ya jimbo hilo huku wakionesha uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Oktoba 30 huenda utaleta changamoto kubwa kwa CCM.
Changamoto kubwa inayoonekana kwa CCM ni kwamba, Mwalimu amezaliwa na anatoka katika familia yenye makazi katika eneo maarufu la Kisimamajongoo ambalo lilikuwa ni kitovu cha harakati za siasa za Chama cha Afro Shiraz (ASP).
Wachambuzi wanasema kwa namna moja ama nyingine familia ya Mwalimu nayo ilishiriki kinagaubaga katika harakati za kudai ukombozi kwa Mzanzibari zilizofanywa na hayati Mzee Karume.
Eneo la Kisimamajongoo ndilo lilikuwa kitovu cha harakati za ASP kudai uhuru wa Mzanzibari kutoka kwa Sultani na Wanamapinduzi walikuwa wakikutana katika eneo hilo kupanga mikakati yao wakiongozwa na hayati Mzee Karume katika nyumba yake aliyoipa jina la ‘Ndiyo’.
Hata hivyo, zilipokuja siasa za ushindani, baadhi ya wakazi wake wakagawanyika na kujiunga na Chama cha Wananchi (CUF).
Wakazi wa eneo la Kisimamajongoo wanaaminika ni ndugu wa damu na hilo ndilo linasemwa huenda likawa ni moja ya jambo litakalowavutia wananchi wa jimbo hilo kuweka kando tofauti zao za kisiasa na kuamua kumpa uongozi Mwalimu wakiamini ni kijana wao na hatowaangusha.
Mwalimu licha ya kuwa amezaliwa katika eneo la Kisimamajongoo, lakini wachambuzi wanasema pia katika uchaguzi huo atabebwa sana na umaarufu wa mama yake mzazi ambaye ni mtangazaji maarufu nchini, Faudhiyat Ismail Aboud.
Kwa sasa Jimbo la Kikwajuni kwa nafasi ya ubunge linaongozwa na Hamad Yussuf Massauni (CCM), ambaye pia ni mzaliwa wa eneo la Kisimamajongoo na hata katika uchaguzi wa mwaka 2010 alibebwa na turufu hiyo.
Inaaminika katika uchaguzi huo wananchi wote wa Jimbo la Kikwajuni kwa pamoja wakiongozwa na kampeni zilizofanywa na wakazi wa eneo la Kisimamajongoo, waliamua kumpa kura Hamad wakiamini kuwa ni kijana wao.
Wachambuzi wanasema uamuzi wa Ukawa kumsimamisha Salum Mwalimu, umefanywa kiutafiti zaidi wakiamini utaamsha ushindani mkubwa katika jimbo hilo ambalo limekuwa chini ya mikono ya CCM miaka yote.
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Mji Mkongwe, Ibrahim Sanya, anatarajiwa kusimama tena kutetea nafasi yake katika uchaguzi ujao akichuana na Mwanahabari Maarufu, Ally Saleh ambaye ameshatangaza nia.
Katika nafasi ya Uwakilishi, CUF imemteua Ismail Jussa Ladhu kuwania nafasi hiyo akiwa ndiye mgombea pekee kutoka chama hicho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles