29.9 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

CAG mpya aahidi makubwa

Profesa Mussa Juma Assad
Profesa Mussa Juma Assad

NA KULWA KAREDIA, DAR ES SALAAM

RAIS Jakaya Kikwete, amemteua Profesa Mussa Juma Assad kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, imesema uteuzi wa Assad ulianza Novemba 5, mwaka huu.

Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Profesa Assad alisema hatamwangusha Rais Kikwete na Watanzania kutokana na imani iliyoonyeshwa kwake.

“Sitamwangusha rais ambaye ameonyesha imani kubwa kwangu, nategemea kufanya kazi kwa kufuata misingi na sheria… hii ni nafasi ya kitaaluma zaidi.

“Kama rais ameona naweza kwanini nimwangushe? Utaalamu na uzoefu mkubwa ninao, nitafanya kazi zangu kwa waledi kabisa,” alisema Profesa Assad.

Alisema amekuwa na uzoefu mkubwa kutokana na kufanya kazi ndani na nje ya nchi na anachotaka kwa wafanyakazi wa ofisi yake ni kumpa ushirikiano wa kutosha.

“Mtu mmoja huwezi kufanya kazi, jambo linalotakiwa ni ofisi nzima kushirikiana ili kufikia malengo,” alisema.

Alisema atahakikisha anaendeleza kazi nzuri iliyofanywa na mtangulizi wake, Utouh ambaye amestaafu miezi michache iliyopita.

Kabla ya uteuzi huo, Assad alikuwa Profesa Mshiriki, Idara ya Uhasibu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na anachukua nafasi ya mtangulizi wake, Ludovick Utouh ambaye amestaafu kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma.

Profesa Assad ni msomi mwenye weledi, ujuzi na uzoefu mkubwa wa uhasibu na udhibiti wa fedha ambaye ana Shahada ya Uzamivu wa Uhasibu (PHD in Accounting) aliyoipata Chuo Kikuu cha Southampton, Uingereza mwaka 2001 na Shahada ya Uzamivu katika Udhibiti wa Fedha (MA in Financial Accounting) kutoka Chuo Kikuu cha Dublin City, Jamhuri ya Ireland mwaka 1991.

Pia ana Stashahada ya Kitaaluma ya Uhasibu (Professional Diploma in Accounting) kutoka Chuo Kikuu cha Dublin City mwaka 1990 na Shahada ya Biashara (Bachelor of Commerce) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1988.

Pamoja na uzoefu wa kitaaluma, Profesa Assad anao pia uzoefu katika eneo la uhasibu na ukaguzi. Alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi (NBAA) kwa miaka saba (2007 – 2014); ni Rais na Mjumbe wa Chama cha Wahasibu Afrika (Pan African Federation of Accountants) tangu mwaka 2012 na mjumbe wa bodi kadhaa za wakurugenzi nchini.

“Katika kumteua Profesa Assad kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, rais anayo imani kubwa kuwa elimu, weledi, ujuzi na uzoefu vitamwezesha kutekeleza vema majukumu ya nafasi hii muhimu katika utawala bora wa nchi yetu,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imesema Profesa Assad ataapishwa leo saa nne asubuhi, Ikulu, Dar es Salaam.

ZITTO

Akizungumzia uteuzi huo, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), alisema imani ya uwajibikaji imeongezeka baada ya uteuzi wa Profesa Assad.

“Imani yangu katika kuimarisha uwajibikaji wa kifedha nchini imeongezeka kwa mara nyingine baada ya uteuzi wa Profesa Assad kuwa CAG mpya.

“Kutokana na kiwango cha usimamizi na matumizi mabaya ya fedha za umma, ikiwamo ufisadi, Tanzania inahitaji mtu asiye na mzaha, msafi na aliyejikita katika sheria na kanuni,” alisema Zitto.

Alisema Profesa Assad anajulikana kwa kutokuwa karibu na vyombo vya habari, lakini anamini ubora wa kazi yake utajieleza wenyewe.

“Nikiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, naamini ataipeleka ofisi katika kiwango kingine kutoka pale Utouh alipoiacha. Nakaribisha uteuzi wa Profesa Assad na ninamuahidi ushirikiano kutoka kwenye kamati yangu,” alisema Zitto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles