22.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Waliojitoa mhanga IPTL wafunguka

mtanzania011214Na Fredy AZZAH

KUHITIMISHWA kwa mjadala wa kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 kwenye akaunti ya Tegeta Escrow bungeni, kumeacha taifa na baadhi ya watu wanaoweza kujipambanua kuwa vinara wa kupinga wizi na wengine wakiwa kwenye mtandao wa kuutetea.

Hatua hiyo ilijidhihirisha kwenye mjadala wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), iliyowasilishwa bungeni na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).

Baadhi ya wabunge waliosimamia kuchukuliwa hatua kwa waliotajwa kuhusika katika kashfa hiyo, wameeleza jinsi ambavyo walitishwa maisha, kujaribiwa kuhongwa na kupata pia mitihani kwenye familia zao.

FILIKUNJOMBE

Mmoja wa waliopitia majaribu makubwa ni Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe ambaye ameiambia MTANZANIA kuwa akiwa kama mbunge wa chama tawala – CCM, kusimamia mapendekezo ya kumwondoa Waziri Mkuu Mizengo Pinda ulikuwa mtihani mkubwa.

Filikunjombe ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa PAC, alisema pia baadhi ya watu waliopendekeza wachukuliwe hatua kutokana na kashfa hii ni marafiki na ndugu zao, hivyo halikuwa jambo rahisi.

“Baadhi ya watu ambao tuliazimia wawajibishwe ni rafiki zetu kabisa, mtu kama Maswi (Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi), ni rafiki yangu na ameoa ndugu yangu.

“Unaweza kuona unakuwa na presha ya namna gani, mke wake anavyokupigia simu akikuambia chonde chonde nisaidie, presha hiyo pia aliipata Kangi (Mbunge wa Mwibara Kangi Lugola), Kangi alishindwa kuongea siku ile kwa sababu, kwanza PM (Waziri Mkuu) alishamuomba sana wakakaa na kumaliza, lakini angalia shangazi yake Kangi, yaani dada yake na baba yake Kangi, ameolewa na kaka yake Profesa Sospeter Muhongo (Waziri wa Nishati na Madini).

“Kaka yule kafariki, kwahiyo anayemtunza leo yule shangazi yake Kangi ni Muhongo, yule shangazi alimpigia Kangi simu akalia kwa saa zima, unaniua, unanimaliza, ukimuondoa Sospeter umeniua, kwahiyo Kangi alipoteza ‘truck’,” alisema Filikunjombe.

Alisema presha nyingine ilikuwa kupendekeza waziri mkuu aondoke. “Ndiyo maana  wakati nasoma maazimio, nilipofika kwenye kipengele cha Waziri Mkuu ilibidi ninywe maji kwanza.

“Wakati ukisoma waziri mkuu mwenyewe yupo nyuma unamsikia anahema, kufika mahali unapendekeza waziri mkuu wako awajibike ni jambo linalotaka moyo sana,” alisema.

Filikunjombe alisema hata hivyo, CCM ilipaswa kujivunia ripoti ya PAC, kwa sababu uamuzi huo unachukuliwa na kamati ambayo wajumbe 19 wanatoka CCM na watano tu wanatoka upinzani.

“Kwenye kamati yale maazimio tuliyapitisha wote, hakuna aliyepinga, hii ni kwa sababu kwenye kamati yetu vyama huwa tunaviacha mlangoni, sisi huwa hatuchuji kitu kabisa.

“Kwahiyo ilipaswa wabunge wa CCM waishike ile ripoti na kuisimamia siyo kuiona ni ya upinzani,” alisema.

Filikunjombe alidai katika kuwakatisha tamaa, watu waliohusika kwa namna moja au nyingine katika kashfa hiyo waliwahonga baadhi ya wabunge wawatukane.

“Tulizomewa, tukapigwa madongo.. wapo watu walipewa hela watuseme vibaya. Hawa watu walitumia vizuri ule msemo wa penye udhia, penyeza rupia,” alisema.

Alisema rushwa ilisababisha Bunge kukosa mwelekeo, huku spika naye akiwa na presha kutoka kwenye mhimili mwingine.

“Ule ni wizi wa wakubwa, kwahiyo mambo hayawezi kuwa rahisi, mimi kuna mtu kati ya waliotajwa alinifuata akaniambia sema unataka nini ili usiniweke kwenye hiyo ripoti.

“Nikamwambia siyo yangu, ripoti ni ya kamati, wala siandiki mimi. Sasa mtu anakufuata anasema umwambie unataka nini, ilikuwa ni shida kwelikweli, walimchafua mwenyekiti wetu (Zitto) kwa sababu wanajua anajua vitu vingi.

“Wakaja kwangu wakasema nimepewa hela, lengo kutugawa, lakini walishindwa, nawashukuru sana wenzetu kwa maana walisimama kidete,” alisema.

Filikunjombe alisema kupambana na mtu mwenye hela ni ngumu sana.

“Ile fedha ilikuwa ni EPA mara tatu, Richmond ilikuwa kashfa lakini hakuna hela iliyoliwa.

“Hii hela ilikuwa inatembea, angalia ilivyokuwa ngumu hata kwa Bunge kuipokea ripoti ile, Bunge liligawanyika, ilikuwa ni shida,” alisema.

Alisema hata hivyo hatua ya Bunge kuendeshwa moja kwa moja wananchi wakiwa wanatazama kupitia televisheni ilisaidia kubadilisha upepo na hali ikabadilika bungeni.

Alisema kipindi chote wakiwa bungeni kula na kunywa ilikuwa ya shaka kubwa, wakiwa na hofu ya kuchezewa mchezo mchafu.

“Siku ile hata yale maji niliyokunywa wakati nasoma ripoti niliingia nayo mimi, nilipofika bungeni nilimpa msaidizi ninayemwamini nikamwambia asiyafungue na nikisimama pale kusoma ripoti ndiyo aniletee.

“Tulifiklia kwenye hatua ya kutoaminiana, Zitto pia hakugusa ile glasi ya maji pale mezani wakati akisoma ripoti yake, tumekuwa tukijificha sehemu za kula. Tumekuwa tukilala kwa kuhamahama,” alisema.

Filikunjombe alisema tatizo aliloliona ni kwamba Serikali haipendi kusimamiwa.

“Serikali haipendi kusimamiwa, inapenda kushauriwa, na bahati mbaya Spika na yeye hakubali hilo, ile nayo ni presha ya kijinga,” alisema.

Kuhusu usalama wa ripoti yao, alisema Serikali haikuiona hadi ilipofika bungeni.

“Ripoti yetu tuliificha sana, tulikuwa tunafanya uchambuzi na kuandika ripoti kisha tunaiweka kwenye ‘flash’, mimi nakaa nayo kwenye ‘flash’ hadi ile siku ya mwisho tulimaliza kuandaa ripoti na kuichapa saa tisa alfajiri na ikabidi bado tuilinde hadi tunaingia nayo bungeni.

“Hata Serikali haikuwa nayo, tumefanya uchambuzi siku zote tunatoka na ‘flash’, tulijua haya maazimio  wakiyaona watatulazimisha tuyaondoe.

“Tuliyalinda hadi baada ya kuwekwa mezani ndiyo na Serikali ikayaona. Tulijua yakishafika pale kwenye meza ya spika huwezi tena kuyabadili.

“Kuna waziri mmoja aliangaika sana, alikuwa anaitafuta ripoti yetu, ikabidi tuagize askari polisi kuwa akija tena safari hii akamatwe.

“Mara nyingi ripoti zikivuja Serikali inalazimisha kujadiliwa kwake kuahirishwe, ndiyo maana baada ya kuiwasilisha spika akaahirisha Bunge ili Serikali ikayasome na ijipange,” alisema.

Zitto Kabwe

Kwa upande wake Zitto, alisema kitu kikubwa alichopitia wakati akisimamia kashfa ya IPTL ni vitisho vya aina mbalimbali.

“Nilitishwa kwamba nitavuliwa nguo hadharani, kwamba waziri na Serikali wana uchafu wangu mwingi na hivyo watasema bungeni iwapo nitaandika ukweli. Sikujali vitisho hivyo kwani naamini katika ukweli na niliwaambia waweke wazi huo uchafu.

“Siku moja kabla ya hotuba yangu watu walio karibu na Waziri wa Nishati na Madini (Profesa Muhongo) na Katibu Mkuu wake (Maswi) walikamatwa wakisambaza ripoti ya kughushi ya CAG na vipeperushi vinavyonikashifu kwa kila mbunge,” alisema.

Akizungumzia kuondolewa kwa Pinda katika orodha ya waliopaswa kuwajibishwa, alisema ni matokeo ya mazungumzo kati ya CCM na vyama vya upinzani.

“Wao walikubaliana na sisi PAC, na kwa kuwa tulitaka taarifa yetu ipite tulikubali,” alisema.

Kwa upande wa usalama wa kula na kunywa, alisema ilikuwa ni sehemu ya tahadhari na kuwa ilifika hatua ya kumwita dada yake aende Dodoma ili awe anampikia chakula.

“Sikunywa maji wakati wa kusoma hotuba kwa sababu sikuwa na imani nayo maana mtandao wa wizi wa Escrow ulikuwa mkubwa sana, nilichukua tahadhari tu,” alisema.

Alisema kulikuwa na vitisho vya kuuawa, lakini hakuvitilia maanani kwani watu walikuwa wanasema sema tu na ndiyo maana alipuuza hakwenda polisi.

“Kubwa kwangu ilikuwa ni kuchafuliwa kwenye mitandao na kutukanwa, lakini kwa kuwa nilikuwa najua nafanya nini sikujali. Nguvu yangu kubwa ilikuwa ni PAC, wajumbe walisimama kidete, hawakujali vyama vyao,” alisema.

Alisema ushauri wake alioutoa kwamba wote waliotajwa kwenye mapendekezo yao ya awali wajadiliwe na mamlaka zao za uteuzi, ulikuwa unamfunga hadi Pinda kwani suala hilo lingekubalika lingeonyesha kuwa Bunge halina imani na waziri mkuu.

“Ungepita maana yake ni kwamba waziri mkuu angekuwa amekosa imani ya Bunge, ilikuwa ni mkakatI,” alisema.

Alisema pia kuwa, Spika Anne Makinda alikuwa msaada mkubwa  na alionyesha uvumilivu mkubwa. “Tulishauriana mara kwa mara mpaka mwisho. Spika alifanya wajibu wake vizuri,” alisema.

Kafulila

Naye Mbunge wa Kigoma Kaskazini, David Kafulila ambaye ndiyo mwanzilishi wa hoja hiyo bungeni, alisema tangu kuanza kwa suala hilo ametukanwa sana, lakini sasa ukweli uko wazi.

“Nilitukanwa sana na wabunge waliokuwa wanatumiwa na mafisadi na mafisadi wenyewe, nilitishwa na hata kubadilisha hoteli mara kadhaa na kuripoti polisi mara mbili Dodoma, nilikuwa nakunywa kwa ungalifu sana hasa nikiwa Dodoma ingawa hata Dar nilichukua tahadhari.

“Ninachoweza kusisitiza ni kwamba ufisadi huu ni mkubwa sana. Hatua tulizochukua kama Bunge zinaweza kuonekana kutosha kwa Bunge change, lakini  kwa mabunge yaliyokomaa sakata hili lilitosha kuingiza nchi kwenye uchaguzi mkuu,” alisema Kafulila.

Mbali na viongozi hao, Profesa Mark Mwandosya ambaye ni Waziri wa Nchi (Kazi Maalum) Ofisi ya Rais, na Stephen Wasira ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu),  Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Mwigulu Nchemba na Mbunge wa Nzega, Dk Hamisi Kigwangalla ni kati ya wanaoweza kuhesabika kuwa ni mashujaa katika kashfa hii.

Viongozi hawa bila kujali vyama vyao, walisimama na kusema suala hili lina harufu ya rushwa na ni lazima hatua zichukuliwe.

WALIOITETEA IPTL

Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde, alisema kamwe viongozi waliotajwa hawawezi kuwajibika kwani hakuna sehemu ambapo ripoti ya CAG imewataja kuhusika na uchotwaji wa fedha hizo.

“Hapa hakuna mtu kujiuzulu wala nini, mheshimiwa waziri mkuu endelea na mambo yako kimyakimya, hakuna kujiuzulu hapa.

“Huyu Zitto ni mmoja wa watu ninaowaheshimu sana, na huwa sipendi kumshambulia bila sababu, lakini ninataka aliambie Bunge hili hizi fedha alizotuma watu kuzichukua kwa Singh zilikuwa za kazi gani,” alisema Lusinde.

Mbunge wa Magomeni, Zanzibar, Muhamad Chombo (CCM), alisema: “Unajua kuna watu wana ashki majununi, inakuwaje umma unaambiwa kitu sicho, fedha za IPTL si za umma, naomba hili litambulike na je katika hili Waziri Mkuu anaingiaje?”

Mbunge wa Viti Maalumu, Mariam Kisangi (CCM), alisema IPTL ilifuata utaratibu wote ikiwamo hukumu ya mahakama.

“Barua ziliandikwa mara nne na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, sasa hili linatoka wapi, wote tunajua katika hili la IPTL zile fedha ni zao, je, inakuwaje ajiuzulu Waziri Mkuu au Muhongo?” alisema Kisangi.

Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa (CCM) alisema: “IPTL tunaambiwa kampuni feki, je, na umeme wao mbona tunautumia? Hili hapana.”

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. katika maelezo yote sijaona ushahidi kuwa peza katika escrow akaunti ni maili ya Umma, ila imeonyesha ni mali ya IPTL na Tanesco au umma kama madaiwa.
    Sasa iweje pesa iliyotengwa kulipa deni inakuwa mali ya mdaiwa?
    IPTL, na kwa maana hiyo Bwana Tugemalilra na asimilia zake 30 ndio wamiliki..sasa kama Rugenlalira aliamua kugawa pesa kama karanga, ni juu yake..
    uongo mkubwa hapa ni kusema kuwa Umma una miliki pesa hilo.
    Taarifa ya CAG na PAC imeonyesha kuwa Tanesco alilalama kuhusu invoice ya malipo na wakili wake Mkono wakaishauri mahakama pesa ya madeni iweke kando katika akaunti maalumu hadi muafaka upatikane, sasa pesa iliyotakiwa kulipwa itakuwaje mali ya Umma au Tanseco tena kama sio wizi wa umma kwa watu na kampuni binafsi?

    Omuburi

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles