* Kessy, Kakolanya, Mahadhi, Dante kuivaa Mo Bejaia
NA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM
MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga wameendelea kuwazidi kete wapinzani wao, Mo Bejaia, kuelekea kwenye mchezo wao unaotarajiwa kuchezwa Jumapili baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuwaruhusu kuwatumia wachezaji wapya wanne kwenye mchezo huo.
Uamuzi wa CAF kuwapitisha wachezaji wapya kipa, Benno Kakolanya, Hassan Ramadhan ‘Kessy’, Vincent Andrew ‘Dante’ na Juma Mahadhi, unatarajiwa kuongeza nguvu na hamasa ya ushindi kwenye kikosi cha timu hiyo hasa kwa Kessy kuziba nafasi ya Juma Abdul aliyebaki nchini kutokana na majeruhi ya kifundo cha mguu ‘enka’ yanayomsumbua.
Yanga ambayo iliweka kambi katika Hoteli ya Rui mjini Antalya, Uturuki tangu Jumapili iliyopita inatarajia kutua Jiji la Bejaia leo vilipo viwanja vya Unite Maghrebine nchini Algeria kwa ajili ya mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Baraka Deosdedit, alisema uamuzi wa CAF wa kuwapitisha wachezaji hao unamaana kubwa kwenye kikosi chao ambacho kitashuka dimbani Jumapili hii kukabiliana na wapinzani wao, Mo Bejaia.
“Kwa sasa tunakila sababu ya kushinda si mchezo huo wa Jumapili pekee, bali michezo yote ya Shirikisho iliyopo mbele yetu kutokana na kikosi chetu kuongeza nguvu mpya.
“Wachezaji wote wapo salama na wanatarajia kesho (leo) kutua Algeria kwa ajili ya mchezo huo ambao utachezwa usiku,” alisema Deosdedit.
Naye Ofisa Habari wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas, alisema kwamba leseni za wachezaji hao ili kucheza michuano hiyo ziliwasili juzi kutoka CAF.
“CAF imetuma leseni za wachezaji hao wanne wapya wa Yanga na maana yake sasa wako huru kucheza Kombe la Shirikisho.
“Wachezaji hao wanaweza kutumika kwenye mchezo huo na mingine ya Shirikisho kutokana na leseni hizo kuwaruhusu,” alisema Lucas.
Taarifa kutoka nchini Algeria zinadai kwamba mchezo huo unatarajiwa kuchezwa usiku saa 22:15, huku tiketi zikianza kuuzwa siku hiyo ya mchezo saa 11:00 asubuhi.
“Mashabiki wataanza kuingia saa 2:30 usiku kwa kiingilio cha Sh 5,830 fedha za Kitanzania kwa jukwaa la kawaida, huku jukwaa la kati wakilipa Sh 9,718 , fedha za Tanzania,” ilisema taarifa hiyo.
Baada ya mchezo huo, Yanga imepanga kurudi tena nchini Uturuki kuendelea na mazoezi tayari kujiandaa na mchezo wake dhidi ya TP Mzembe ya DR Congo kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam Juni 28 mwaka huu.