Na Shomari Binda, Musoma
WAJUMBE wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, wamewataka Watanzania kuikataa Katiba inayopendekezwa kwa kuwa haikuzingatia masilahi ya Watanzania.
Waliyasema hayo juzi katika ukumbi wa MCC, mjini Musoma kwenye mdahalo wa kujadili na kuelimisha wananchi kuhusiana na mchakato wa kupata Katiba Mpya na kuwataka kupiga kura ya hapana.
Akizungumza katika mdahalo huo, aliyekuwa Mjumbe wa Tume hiyo, Joseph Butiku, alisema mchakato wa kukusanya maoni ya Katiba, haukuandaliwa kienyeji bali ulipitishwa kisheria ambapo kazi hiyo ilifanyika kwa kujali masilahi na haki za Watanzania kwa vizazi vijavyo.
“Kuipigia kura ya Ndiyo Katiba inayopendekezwa ni kuuza utu wako, Katiba hiyo haikidhi hata kidogo masilahi ya wananchi ni Katiba inayoandaliwa kwa ajili ya masilahi ya watu fulani fulani,” alisema Butiku.
Alisema Tume yao haikupindisha maoni ya wananchi ila baada ya kuikabidhi tu, wapo wajanja kwa sababu zao waliweka mambo yao kwa kupindisha baadhi ya vipengele wanavyotaka wao huku wakitupilia mbali maoni halisi ya wananchi.
Alisema baada ya baadhi ya wajumbe walipoanza kupiga kelele kutetea maoni ya wananchi, walianza kupewa vitisho na lawama nyingi.
Butiku aliwataka Watanzania kuchukua uamuzi ulio huru na kujiamini kwa kuwa wao si wakimbizi bali ni Watanzania halali na mchakato huo si wa vyama vya siasa wala watu binafsi.
“Kwa watu walio na mawazo ya kuipigia kura ya ndiyo, ni sawa na kuisusia nchi,” alisema.
Mjumbe mwingine wa Tume kutoka Zanzibar, Ally Salehe, alisema Rasimu ya Warioba ilikuwa Katiba iliyotazama mbele zaidi na iliyokuwa na manufaa kwa Watanzania wote bara na visiwani, lakini cha kushangaza ilitupiliwa mbali.
Alisema maoni ya wananchi yalipuuzwa na mchakato mzima wa Katiba ulighubikwa na wanasiasa ambapo kuna mambo ambayo yanapungua na hivyo kuchangia muungano usiwe na nguvu.
Alisema Bunge la Tanzania hujadili masuala ya Muungano japo hayana masilahi ya kimuungano kwani Zanzibar kuna Bunge la kujadili masuala ya Zanzibar na kwenye maoni ya wananchi kulikuwa na vifungu vizuri vilivyokuwa bayana juu ya suala hilo lakini vimeondolewa.
Mjumbe mwingine, Humphrey Polepole, aliwaeleza wananchi kuwa Katiba inayopendekezwa kwa sasa inatazama Uchaguzi Mkuu mmoja tu ujao badala ya kutazama chaguzi zaidi ya 100 zijazo kwa masilahi ya vizazi vijavyo.
Aidha, aliwataka wananchi kupiga kura ya maoni ya kupitisha Katiba Mpya kwa uelewa na kutambua nini wanafanya na kwa faida gani ili kuondokana na Katiba ambayo itakuwa mzigo na msalaba mkubwa kwao.
Polepole, alisema lengo lao ni kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mchakato wa kupata Katiba Mpya na si kwamba wana njama na Serikali.
“Ni ukweli usiopingika kuwa Katiba iliyopo kwenye mchakato haiwafai Watanzania walio na akili timamu na walio na shauku ya kupata haki sawa na si kuwa na taifa la matabaka
“Misingi yote iliyokuwa imepitishwa na Tume ya Warioba kama tunu ya Katiba Mpya iliondolewa ambayo ni uzalendo, uwajibikaji, uadilifu na umoja. Na badala yake wameingiza tunu nyingine bila kujua nini maana ya tunu,” alisema Polepole.
Februari mwaka huu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), itaanza uandikishaji wapiga kuwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na baadaye Machi mwaka huu kampeni zitaanza na kuhitimishwa na kazi ya upigaji kura Aprili 30, mwaka huu.
Pamoja na hali hiyo, yameibuka makundi na taasisi kadhaa za kiraia zikitaka mchakato huo uahirishwe mwaka huu ili kupisha Uchaguzi Mkuu.
Hata hivyo, Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wametangaza kutoshiriki katika mchakato wa kura ya maoni ya Katiba inayopendekezwa kwa kuitaka Serikali iahirishe mchakato huo hadi mwaka 2016.