25.3 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Burundi hakukaliki

Na Waandishi Wetu, Bujumbura na Dar
WAKATI askari wakijaribu kuzuia maandamano yaliyoanza upya jana tangu Rais Pierre Nkurunzinza arejee nyumbani baada ya kushindwa jaribio la kumpindua wiki iliyopita, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amemtaka kiongozi huyo kuahirisha uchaguzi mkuu nchini humo uliopangwa kufanyika mwezi ujao.
Msemaji wa Rais Kenyatta, Manoah Esipisu alisema viongozi hao wawili wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) walizungumza juzi kwa simu.
Espisu alisema viongozi wengine wa nchi za ukanda huo wana mtizamo sawa na Kenyatta. Wote wanataka uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Juni 26 uahirishwe kwa misingi kuwa hakuna mazingira mazuri ya kuuendesha kipindi hicho.
Hayo yametokea huku askari mjini Bujumbura wakirusha juu risasi kuwatawanya waandamanaji ambao walikuwa wakitawanyika na kukusanyika tena mahali kwingine.
Vilevile, vijana wengi walionekana wakifunga barabara wakati wa maandamano hayo katika sehemu tofauti za Bujumbura.
Licha ya onyo lililotolewa na serikali, waandamanaji hao walimimikika mitaani wakipuliza filimbi na kuimba nyimbo za kumtaka Rais Nkurunziza aachane na mipango yake ya kugombea urais kwa muhula wa tatu.
“Tukomeshe hofu, turudie kasi yetu,” alisema Pacifique Nininahazwe, kiongozi wa maandamano hayo huku akitoa mwito wa kufanyika maandamano ya ‘amani, bila matusi wala kurusha mawe.’
“Tutasimama polisi wakitukabili, tutaketi chini na kuinua mikono juu, kisha tuendelee kutembea,” alisema kwenye ujumbe uliosambazwa katika mitandao ya jamii, baada ya vituo vinne mashuhuri vya redio kufungwa na serikali.
Mawaziri wafukuzwa
Wakati hayo yakiendelea Rais Nkurunziza amewafukuza kazi mawaziri wake watatu waandamizi wa ulinzi, mambo ya nje na biashara.
Hatua hiyo ilichukuliwa huku wanamgambo wa kundi la al-Shabaab wakisema kiongozi huyo ni mwongo kwa kujaribu kuwahusisha na mpango wa kuishambulia nchi hiyo.
Katika mabadiliko yaliyotajwa jana, Emmanuel Ntahonvukiye ambaye ni raia ameteuliwa kuwa waziri wa ulinzi akichukua nafasi ya Pontian Gaciyubwenge, huku Alain Aime Nyamitwe akiteuliwa kuwa waziri wa mambo ya nje kumrithi Laurent Kavakure, alisema Msemaji wa Rais, Gervais Abayeho.
“Rais ana mamlaka chini ya katiba ikiwamo kubadili serikali. Anaamini kwamba wakati umefika na ni wajibu wake kufanya mabadiliko,” alisema Abayeho.
Nyamitwe ni balozi wa zamani katika Umoja wa Afrika (AU) huku Ntahonvukiye akiwa mwanasheria ambaye aliongoza mahakama ya kupambana na rushwa, anayekuwa raia wa kwanza kuwa waziri wa ulinzi katika kipindi cha miaka 50.
Waziri wa Biashara, Virginia Ciza naye ameondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Irina Inantore.
Al Shabaab waibuka
Akizungumza hadharani kwa mara ya kwanza tangu arejee nyumbani kutoka Tanzania kufuatia jaribio la wiki iliyopita la kutaka kumpindua, Rais Nkurunzinza alidai nchi yake imejidhatiti kukabiliana na vitisho vipya vya al-Shabaab dhidi ya nchi hiyo na nyingine zenye majeshi Somalia.
Akitoa taarifa hiyo juzi, Nkurunziza katika hali isiyotarajiwa hakugusia chochote kuhusu jaribio la mapinduzi ya serikali yake
Lakini Msemaji wa Al-Shabab, Sheikh Ali Mahamud Rage alisema kauli ya Nkurunzinza ni uongo mtupu na ni wazi imelenga kuihadaa dunia ili ‘ibadili mwelekeo kutoka kwake’.
Askari wa Burundi wanapigana dhidi ya al-Shaba, kama sehemu ya majeshi ya Umoja wa Afrika nchini Somalia
Meya wa Bujumbura
Awali Meya wa Bujumbura, Juma Saidi, alionya kupitia kituo cha taifa cha televisheni kuwa waandamanaji watahesabiwa kuwa wahusika wa mapinduzi na maofisa wa usalama wameagizwa kuwakabili kama wapinduaji.”
Vipeperushi mitaani
Kabla ya kufanyika kwa maandamano hayo katika mitaa mbalimbali ya mji wa Bujumbura vilisambazwa vipeperushi na waandamaji vinavyopinga hatua ya Rais Nkurunziza, kuwania uongozi wa nchi hiyo kwa muhula wa tatu.
Vurugu zasambaa
Wakizungumza na MTANZANIA mjini Bujumbura baadhi ya wananchi walisema hali ya amani nchini humo inazidi kuwa tete baada ya vurugu kuendelea kuenea kaskazini mwa Burundi.
“Hali imekuwa si nzuri sana hasa kwa asubuhi lakini kwa jioni hii tunashukuru Mungu tumeweza hata kuendesha magari … ingawa kwa sasa hali ya maandamano inaendelea upande wa Kaskazini mwa nchi.
“… kwa sasa kazi kubwa ni kupambana na makundi haya ambayo yana lengo la kutaka kuundwa Serikali ya mpito,” alisema mmoja wa Serikali
Nkurunziza ameshutumiwa kwa kuanzisha kampeni za kukandamiza wapinzani wake na kunyamazisha vyombo huru vya habari tangu viongozi wa mapinduzi walipokiri kushindwa Ijumaa iliyopita, baada ya kupigana vikali na wanajeshi wanaounga mkono serikali.
Jumamosi iliyopita, watu 18 wanaodaiwa kupanga mapinduzi hayo walifikishwa mahakamani, akiwamo waziri wa zamani wa ulinzi na makamishna wawili wakuu wa polisi, wakikabiliwa na mashtaka ya ‘kujaribu kuipindua serikali’.
Vyama vya upinzani na mashirika ya kutetea haki za binadamu yamesisitiza nia ya Nkurunziza kutaka kuongoza kwa muhula wa tatu ni kinyume na katiba na makubaliano ya amani ya Arusha yaliyowezesha kusimamishwa vita mwaka 2005.
Raia wa Marekani waondolewa
Wakati huo huo, Marekani imeondoa raia wake na wa nchi nyingine kutoka Burundi baada ya nchi hiyo kukumbwa na ghasia kufuatia maandamano ya wiki kadhaa na jaribio la mapinduzi dhidi ya Rais Nkurunziza.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Jeff Rathke amesema mbali na Wamarekani 20 waliosafiri kwa ndege hadi Kigali, Rwanda juzi, Marekani iliwasaidia raia wanne wa Canada na raia wa mataifa mengine huku ikiwa imeshaufunga ubalozi wake mjini Bujumbura tangu Ijumaa iliyopita.
Kauli ya CNDD
Akizungumza na MTANZANIA jana mjini Bujumbura, Msemaji wa CNDD-FDD, Ndabirabe Gelose, alisema machafuko nchini humo yanaendelea kudhibitiwa licha ya makundi ya watu kuendelea kuhamasisha maandamano.
“Ni kweli hali ya usalama hasa kwa siku ya leo (jana), haikuwa nzuri hasa kwa asubuhi lakini baada ya muda ilitulia na sasa raia wote wako na shughuli zao kama kawaida hapa Bujumbura.
“Hatufurahishwi na hali inayoendelea na sisi kama chama kinachotawala tumekuwa na kazi kubwa ya kwenda kwa Warundi na kuwataka warejeshe amani chini kwetu,” alisema Gelose.
Warioba kuongoza jopo
Wakati huohuo, Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba, anatarajiwa kuongoza jopo la waangalizi wa Uchaguzi wa Burundi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Waangalizi hao wametakiwa kwenda nchini humo kufanya majadiliano na pande zote mbili zinazosigana na kutoa taarifa kwa wakuu wa nchi za EAC.
Jaji Warioba atafuatana na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa nchi za EAC, Dk. Harrison Mwakwembe, pamoja na Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Dk. Richard Tsezibera kutathmini hali halisi.
Akizungumza na waandishi wa habari Arusha jana, Dk. Tsezibera, alisema hayo ni maazimio yaliyofikiwa kwenye kikao cha dharura cha Baraza la Mawaziri wa EAC, kilichokutana jana chini ya uenyekiti wa Dk. Mwakyembe.
Alisema waangalizi hao kutoka EAC watashirikiana na Baraza la Wazee wa Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika (COMESA) na baadaye kutoa ushauri kwenye kikao cha wakuu wa EAC.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles