* Bajeti ya Waziri Mkuu yapunga kwa bil 46/-, Bunge kicheko, laongezewa bil. 3.8/-
Na Fredy Azzah-Dodoma
BUNGE limeiagiza Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kutosita kufuta chama chochote cha siasa kinachokiuka sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa vyama vya siasa.
Hayo yalisemwa jana bungeni mjini hapa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mohamed Mchengerwa, alipokuwa akisoma maoni ya kamati yake, kuhusu utekelezaji wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2018/19.
“Kamati inashauri na kusisitiza kwamba Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ihakikishe kunakuwepo na usimamizi wa karibu kwa kufuatilia na kuchunguza mienendo inayoharibu sifa na vigezo vya vyama vya siasa nchini.
“Na kwamba Msajili asisite kufuta usajili wa chama chochote cha siasa kitakachokiuka sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa vyama vya siasa,” alisema Mchengerwa katika hotuba yake ya kamati aliyowasilisha bungeni.
Alisema pia kamati hiyo inaishauri ofisi hiyo ifanye ufuatiliaji na ukaguzi wa matumizi ya ruzuku kwa vyama vya siasa ili kuhakikisha yanazingatia madhumuni yaliyokusudiwa.
“Ikibainika ruzuku hizo zinatumika tofauti na madhumuni hayo, chama husika kisipewe ruzuku ili kutoa fundisho kwa vyama vyote kuzingatia matumizi stahiki ya fedha za wananchi,” alisema Mchengerwa.
Ushauri wa kufuta vyama vya siasa, umekuja ikiwa ni takribani mwezi mmoja tangu Msajili wa Vyama vya Siasa kuitaka Chadema kueleza kwanini isichukuliwe hatua kutokana na kufanya maandamano yaliyo kinyume na sheria wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo Jimbo la Kinondoni, Dar es Salaam, Februari 16, mwaka huu.
Hadi sasa tayari Msajili amekiandikia barua mbili chama hicho kuhusu suala hilo.
Chadema ilijibu barua hizo, lakini bado hatua ya mwisho ya Msajili juu ya chama hicho hadi sasa haijajulikana.
Kuhusu Chama cha CUF, kamati hiyo imemshauri Msajili kuchukua jitihada za kutosha kusuluhisha mgogoro wake.
“Kamati inashauri Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuchukua jitihada za kutosha kusuluhisha migogoro kwenye Chama cha Wananchi CUF ili kuepusha athari kubwa zinazoweza kujitokeza katika Muungano,” alisema Mchengerwa.
Mbali na masuala hayo, kamati hiyo pia imetoa wito kwa Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge, kuhakikisha kamati hiyo inafanya ziara ya kikazi kukagua hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa makazi ya Waziri Mkuu ili kujiridhisha na uthamani wake na kiasi cha fedha kilichotumika.
Kuhusu Tume ya Taifa ya Uchaguzi, kamati iliitaka kuendelea kuchukua jitihada za kutosha kuboresha daftari la wapigakura.
“Hatua hizo zijumuishe utoaji elimu ya uraia, hususan uandikishaji wapigakura kwa vijana, waweze kutumia haki yao ya kikatiba ya kupiga au kupigiwa kura.
“Hali hii itaongeza idadi ya Watanzania wengi zaidi wenye sifa na vigezo vya kupiga kura katika chaguzi mbalimbali zinazokuja,” alisema.
Mchengerwa alieleza kuwa tume inapaswa kujitahidi kufanya kazi kwa uweledi ili kuendelea kuaminika kwa wadau wa uchaguzi.
Alisema inapaswa kuhakikisha inawashirikisha wadau wa uchaguzi wakati wa uhuishaji wa daftari la wapigakura, kuepuka migogoro isiyokuwa na tija kwa taifa.
“Kamati inashauri tume ihakikishe inawafuatilia wasimamizi wake wa uchaguzi na kuwawajibisha pale wanapofanya uzembe unaosababisha madhara yanayoweza kudhibitiwa,” alisema.
KAMATI YA BUNGE YA UKIMWI
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ukimwi, Oscar Mukassa, akiwasilisha maoni ya kamati yake kwenye ofisi hiyo ya Waziri Mkuu, alisema matumizi ya dawa za kulevya ni tatizo linaloongezeka kwa kiasi kikubwa.
Alisema Serikali inapaswa kuchukua hatua za haraka kuhakikisha mamlaka na wadau wanatoa elimu ya kutosha kwa jamii kufahamu madhara ya dawa za kulevya.
Mukassa alisema kamati yake inaishauri Serikali kuwa halmashauri zote zitenge asilimia moja ya mapato ya ndani kutoka asilimia 10 iliyokwishatengwa kwa mfuko wa maendeleo ya jamii.
Kwa habari zaidi jipatie nakala ya gazeti la MTANZANIA.