23.8 C
Dar es Salaam
Sunday, October 13, 2024

Contact us: [email protected]

MBOWE: WATUMISHI KAMBI YA UPINZANI WAMEFUKUZWA

Fredy Azzah Na Ramadhani Hassan-Dodoma


Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, amesema Bunge limewafukuza watumishi wa kambi hiyo waliokuwa wanaandaa hotuba zao na kufanya tafiti mbalimbali, hivyo hakutakuwa na hotuba za kambi hiyo hadi watakaporejeshwa.

Alisema hata watumishi hao watakaporejeshwa, hawatakuwa tayari kupeleka hotuba zao kwa Katibu wa Bunge ili achague nini cha kusoma bungeni na nini cha kuacha na kwamba Bunge liking’ang’ania kufanya hivyo, hawatasoma hotuba hizo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana baada ya kikao kifupi cha kambi hiyo, alisema amefuatilia kwa muda mrefu suala la watumishi, lakini Katibu wa Bunge amekuwa akikataa kuwarudisha na badala yake anataka kumpa watumishi wa Serikali ili wafanye kazi ya kuandaa hotuba zao.

“Kigaigai (Katibu wa Bunge, Dk. Stephen Kagaigai) anasema atanipa watumishi wa umma waje kufanya kazi za kambi, hivi kweli watupe watumishi wao waje kuandika hotuba za upinzani.

“Ikibidi hata ofisi yenyewe tutaifunga, kwahiyo hakutakuwa na hotuba yoyote ya kambi ya upinzani mpaka pale watumishi wa ofisi yetu watakaporejeshwa.

“Na wakirejeshwa hatutakubali hotuba yetu ipelekwe kwa Katibu wa Bunge kuanza kusema futa hii, futa hii, wakifanya hivyo hotuba hatutaisoma, lakini hatutasusa Bunge.

“Nasisitiza hakuna mpango wa kususa Bunge kwa sasa, leo nilishindwa kufika mapema kwa sababu tulitoka Dar es Salaam kwa mambo mengine ya kitaifa,” alisema Mbowe.

Mbowe alisema watumishi hao wapo kikanuni na kisheria na huu ni mfululizo wa matukio ndani ya kambi yao kwani yeye alinyang’anywa gari la Serikali na dereva ambaye kisheria anatakiwa kuwa naye.

Kuhusu kunyang’anywa gari alisema: “Mimi mwenyewe kuanzia Januari sina dereva wala gari la Serikali licha ya kuwa ni haki yangu, lakini mimi sijililii mimi, ninayo magari mengi nitatumia na hata nikikosa, wabunge hapa watanipa gari la kutembelea,” alisema.

Hata hivyo hakueleza sababu ya kunyang’anywa gari na dereva.

Alisema kanuni ya 16 (4) ya Bunge inataka vyama vya siasa vyenye uwakilishi bungeni vitunge kanuni za vyama kwa uendeshaji wa vyama hivyo bungeni.

“Kanuni hii imezaa kanuni za Kambi Rasmi ya Bungeni na zimeandaliwa na kambi kwa kushirikiana na ofisi ya Katibu wa Bunge,” alisema.

Mbowe alisema kanuni hizo zinatambua Kambi ya Upinzani ni idara ambayo ina watumishi wa aina mbalimbali, wakiwamo wa Bunge na wale wa mikataba ambao ni sehemu ya Sekretarieti ya Bunge.

Alisema watumishi hao hulipwa na Bunge, lakini hutokana na mapendekezo ya Kambi ya Upinzani na huajiriwa kwa mikataba ya miaka miwili miwili.

Mbowe alisema waliunda sekretarieti yao tangu Bunge la 10 na lile la 11 lilipoanza pia waliunda.

“Bunge la 11 tuliunda tena sekretarieti, wajibu ni kuandika hotuba za mawaziri vivuli na hoja zote za kambi, tulikuwa na watumishi wanne tu wanasimamia zaidi ya wizara 30.

“Tumekuwa tukiomba waongezwe angalau wawe 12, Bunge lenyewe lina watumishi zaidi ya 400, kutoa watumishi wanne wawe wakuhutubia kambi ni kuhujumu kambi.

“Katika Bunge hili la 11, watumishi hawa waliingia mkataba na Bunge ambao ulikuwa unaisha Desemba mwaka jana.

“Mikataba ya kuwaajiri hawa inatokana na mapendekezo yetu, Novemba 7, mwaka jana niliandika dokezo kwa Spika na Katibu wa Bunge, kwamba Desemba mikataba inaisha kwahiyo nikapendekeza wapewe tena mikataba walewale waliokuwepo.

“Lakini tangu Desemba hiyo, mpaka leo hakuna majibu ya barua yangu, kwenye Bunge la Januari ofisi ya katibu iliamuru watumishi wote wa kambi waondoke kwenye ofisi za Bunge, walifukuzwa kwenye ofisi za umma kama vibaka.

“Nilishangaa Katibu wa Bunge anapata wapi kiburi cha kufukuza watu kwenye ofisi zangu bila hata kuniambia. Unapowatimua unadhani utafiti wa sheria, masuala mengine kama kupitia randama za Serikali na kuandika hotuba atafanya nani?

“Katibu aliniambia anafanya kazi kwa kanuni na mwenye uwezo wa kufanya maamuzi mengine ni Spika ambaye yupo nje kwenye matibabu.

“Mtu wa kuandaa hotuba, kufanya utafiti wa marandama hayupo, leo (jana) Tulia (Naibu Spika Dk. Tulia Ackson) anasema hakuna hotuba, anataka itoke wapi, alitaka niiandalie Segerea ama?” alihoji Mbowe.

Alisema licha ya watumishi hao wa Kambi ya Upinzani kufukuzwa, wale wa kambi ya CCM ambao pia mikataba yao iliisha Desemba na wengine wa miakataba, bado wapo kazini.

Mbowe alisema ofisi yake ilifanya mazungumzo na Spika Job Ndugai, akiwa kwenye matibabu nchini India na kutaka wapewe watumishi 12, lakini akasema atatoa watatu tu.

Alisema kwa sasa ameelezwa kuwa Spika Ndugai ataitisha kikao wiki ijayo ambacho kinaweza kujadili suala hilo.

Kwa habari zaidi jipatie nakala ya gazeti la MTANZANIA.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles