Mwandishi Wetu, Dodoma
Bunge limeridhia kutofanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, kutokana na kauli yake kuwa bunge ni dhaifu, hatua iliyolidhalilisha bunge.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Emmanuel Mwakasaka ametoa mapendekezo hayo bungeni leo Jumanne Aprili 2, wakati akisoma taarifa ya kamati hiyo iliyomhoji CAG kutokana na kauli yake hiyo ambapo ilimtia hatiani.
“Kamati ilimuuliza CAG Assad kama ataacha kulitumia neno dhaifu akasisitiza ataendelea kulitumia, hakuomba msamaha wala kujutia na akasisitiza ataendelea kulitumia neno hilo,” amesema Mwakasaka.
Aidha, baada ya kusoma taarifa hiyo, Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, aliwahoji wabunge kama wanakubaliana na mapendekezo hayo ambapo walikubaliana na uamuzi huo huku wengine wakipinga.
Katika hatua nyingine, kamati hiyo pia imependekeza Bunge kumsimamisha Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), kuhudhuria mikutano miwili ya Bunge kutokana na kuunga mkono kauli ya CAG.