Samia: Mchango wa mwanamke utambulike kiuchumi

0
979
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan (kushoto), Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya TPB, Dk. Edmund Mndolwa na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Sabasaba Moshingi, wakifurahia jambo baada ya kuzindua akaunti ya Tabasamu kwa wanawake, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki
  • Sera ziangalie mchango wao, aisifu TPB kwa akaunti Tabasamu

MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

TANZANIA ni moja ya nchi barani Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa kasi. Tangu mwaka 2017 kasi ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania ni asilimia 7.

Moja ya chachu ya kasi hiyo ni biashara ndogondogo ambazo kwa kiasi kikubwa zinamilikiwa na wanawake.

Takwimu za usawa wa kijinsia katika ajira zinaonyesha kwamba kufikia mwaka 2014 Watanzania milioni 2.1 walikuwa wameajiriwa katika sekta rasmi, ikiwa ni pamoja na serikalini na sekta binafsi, kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu nchini.

Hatahivyo takwimu rasmi za serikali zinaonyesha pia kwamba zaidi ya asilimia 60 ya wanawake walio kati ya umri wa miaka 18 hadi 24 yaani milioni 13.9 wanajishughulisha na shughuli zisizo rasmi yaani biashara ndogondogo na kilimo.

Hii maana yake ni kwamba ni asilimia 0.75 tu ya wanawake walioko katika umri wa kufanya kazi ndio wapo katika sekta rasmi. Kwa maneno mengine, idadi kubwa ya wanawake walioko katika umri wa kufanya kazi nchini ni wajasiriamali.

Licha ya kuwa na idadi kubwa ya wanawake wenye ujasiri wa kubuni na kuendesha biashara, kasi ya ukuaji wa mitaji yao bado ni finyu na duni.

Chanzo kikuu cha mitaji karibuni duniani kote ni mikopo ya benki rasmi ya kibiashara. Hata hivyo, tafiti zinaonesha kuwa wanawake wengi wajasiriamali kutoka nchi zinazoinukia  uchumi ikiwemo Tanzania hawana mikopo kutoka benki na taasisi rasmi za kifedha.

Kutokana na hatua hiyo  inamfanya Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, kuona umuhimu kwa sasa sera za uchumi wa nchi zitambue mchango wa mwanamke kwenye uzalishaji mali na ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Akizindua akaunti maalumu ya Tabasamu kwa ajili ya wanawake wote nchini, chini ya ubunifu wa Benki ya TPB, anasema hatua hiyo inatokana na kuwa wanawake wengi wamekuwa wakishiriki kujenga uchumi kupitia sekta isiyo rasmi lakini bado wamekuwa hawatambuliki kwenye sera.

Anasema kuwa hatua ya kuzinduliwa kwa mkakati huo ni njia mahsusi ya kumuwezesha mwanamke ili aweze kufikia malengo yake.

Mama Samia anasema kuwa Rais Dk. John Magufuli, amekuwa akiwathamini wanawake na ndio maana hata ilipofika hatua ya kufunga baadhi ya benki za serikali ambazo zilikuwa zinajiendesha kwa hasara  aliamua iliyokuwa Benki ya Wanawake Tanzania ihamishiwe Benki ya TPB ili kuenzi na kupata usimamizi mzuri wa masuala ya wanawake ikiwamo kuwa na huduma maalumu zinazowahusu.

“Benki ya TPB ipo imara na ndio maana katika utekelezaji wa agizo la serikali wamehakikisha huduma zote zilizokuwa zinatolewa na Benki ya wanawake sasa tunazikuta huku. Na kufunguliwa kwa akanti maalumu ya Tabasamu ni sehemu ya kuenzi mchango wa wanawake nchini.

“Tunajua kwamba wanawake ndio wazalishaji wakubwa na ndio wenye kumiliki viwanda vidogo na vya kati lakini bado mchango wao hautambuliki kwenye ukuaji wa uchumi. Na hili linaweza kuwa kwenye hata kwenye sera zetu, sasa wakati umefika Mheshimiwa Naibu Waziri Dk. Ashatu Kijaji, anzeni sasa kufanya marebisho ya sera hizo ili kuweza kutambua mchango huu,” anasema Samia

Anasema kwamba wanawake ndio wazalishaji wakubwa na wengi wao wanamiliki viwanda vidogo na vya kati lakini bado mchango wao hautambuliki kwenye ukuaji wa uchumi.

Anasema Benki ya TPB ina matawi takriban 80, ATM 54, mtandao wa Umoja Switch takriban 200 na mawakala 150 kupitia Shirika la Posta huku ameitaka benki hiyo kuwafikia wanawake wengi haswa vijijini na kuhakikisha wanapata huduma na elimu ya masuala ya kifedha.

“Wanawake ni nguzo kuu ya uchumi wetu, kwani wao ndiyo wazalishaji wakuu kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa. Mbali ya kulea familia, huwezi kuwakosa wanawake kwenye sekta yoyote ya uzalishaji mali, na hivyo siyo upendeleo kuanzisha akaunti maalumu ya Tabasamu kwa wanawake, bali ni haki yao ya msingi kama ilivyofanya Benki ya TPB,” anasema

Kutokana na hali hiyo Makamu wa Rais ameitaka TPB ishirikiane na makampuni ya simu kuhakikisha kuwa wanawake hawa si tu wanapata taarifa za kibenki hata ikiwezekana kuweza kupata huduma za kibenki kama mikopo kupitia simu zao za mikononi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TPB, Sabasaba Moshingi, anasema kuwa katika kutambua umuhimu wa changamoto za kujiwekea akiba ambazo watu wengi hukutana nazo, Benki ya TPB imelazimika kuanzisha akaunti hiyo maalumu ya Tabasabu ili kuwezesha akina mama, dada waweze kijiwekea akiba na kujikwamua kiuchumi.

“Madhumuni ya akaunti hii ya kina mama na dada ni kujikwamua kiuchumi kwa kufungua akaunti ya Tabasamu ili kujiwekea akina na hatimaye waweze kuboresha maisha yao ya kila siku kwa kuongeza mitaji ya biashara zao au kuanzisha shughuli mbalimbali za kiuchumi.

“Walengwa wa akaunti hii mahsusi kwa akina mama  au akina dada wanaojishughulisha na shughuli za kiuchumi za aina yoyote ya biashara,” anasema Moshingi

Anasema iwapo muhusika atafungua akaunti ya Tabasamu itampa fursa mwenye akaunti kuchukua mkopo hasi asilimia 50 ya akiba yake hata atakapohitaji kufanya hivyo.

Lakini pia anasema akaunti hiyo inatoa faida nono kwa mwaka na inampa mwenye akaunti kinga za bima ya afya na bima ya maisha.

“Akaunti ya Tabasamu inatumika kama dhamana endapo mwenye akaunti anahitaji mkopo,” anasema Moshingi

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya TPB, Dk. Edmund Mndolwa, anasema kuwa benki hiyo imefanya mabadiliko makubwa katika huduma ikiwamo kuwa na akaunti maalumu ikiwamo ya Tabasamu kwa lengo la kusogeza huduma bora kwa jamii.

“Kuzinduliwa kwa akaunti hii ya Tabasabu sasa kunakwenda kumfanya mwanamke kuwa sehemu ya uchumi wa nchi yetu kwa kuweza kupata huduma mbalimbali ikiwamo mikopo ya gharama nafuu na hili sasa linakwenda kuondoa fikra potofu kwa jamii,” anasema Dk. Mndolwa

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here