26.7 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

Bunge kuburuzwa mahakamani

Bunge
Bunge

NA ABRAHAM GWANDU, ARUSHA

HATIMA ya Bunge Maalumu la Katiba kuendelea na vikao vyake imezidi kuwa shakani baada ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kutangaza kusudio la kwenda mahakamani kesho.

Uamuzi wa TLS umetolewa siku moja baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema kutangaza mkakati mbadala wa kukwamua mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya.

TLS inataka kuiomba mahakama kuzuia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba hadi muafaka wa taifa utakapopatikana ili kupata Katiba bora kwa ajili ya wananchi.

Uamuzi wa kuzuia kuendelea vikao hivyo unatokana na TLS kutangaza kusudio la kupeleka mahakamani maombi ya zuio chini ya hati ya dharura ikiitaka Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam kutoa uamuzi juu ya usahihi wa kuendelea kwa vikao vya Bunge hilo.

Rais wa TLS, Charles Rwechungura, alitoa msimamo huo Arusha jana mwishoni mwa mkutano maalumu wa wanachama uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC).

Tayari TLS imeunda kamati maalumu ya wanasheria waliobobea wakiongozwa na mwanasheria Mpare Mpoki ambao kesho watawasilisha madai hayo katika Mahakama Kuu ya Tanzania na ile ya Zanzibar.

Katika madai yao, TLS imesema sababu ya kulifikisha suala hilo mahakamani ni mvutano na mitizamo tofauti inayotolewa na kila kundi hasa kuhusu kifungu cha 25 cha sheria ya mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2012.

Wadaiwa katika shauri hilo kwa mujibu wa Rwechungura watatajwa baadaye, lakini hadi sasa aliyetajwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, na huenda Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta akajumuishwa.

“Huu ni uamuzi wa wanachama wote wa TLS bila kujali wako katika Bunge Maalumu la Katiba wanaendelea na vikao au wale waliotoka na kususia vikao…hatuko upande wowote tunachotaka ni uamuzi wa mahakama hasa katika kifungu cha 25 cha sheria ya mabadiliko ya Katiba inayohusu theluthi mbili ya wajumbe wanaoweza kuamua.

“Ni vizuri mahakama ikatoa ufafanuzi na tunaamini itafanya hivyo tujue na wananchi wajue pia kama kweli Katiba bora itapatikana bila kuwapo maridhiano na kama haiwezekani basi mahakama isimamishe mchakato wote hadi maridhiano yatakapopatikana kwa manufaa ya Watanzania,” alisema Rwechungura.

Alisema wanachama waliandaa rasimu shauri na kuikabidhi kamati iliyoundwa ili ipate muda wa kupitia baadhi ya vifungu katika rasimu hiyo na kuviboresha kabla ya kuviwasilisha mahakamani.

Wakati kesi ya msingi itakapoanza kusikilizwa, TLS imeazimia kuwasilisha mahakamani shauri dogo la kuzuiwa kwa vikao vya Bunge Maalumu la Katiba (kamati) vinavyoendelea mjini Dodoma hadi hapo uamuzi wa kesi ya msingi utakapotolewa na mahakama.

Wakati TLS ikichukua hatua hiyo, Jaji Werema tayari ameonyesha wasiwasi wake kuhusu theluthi mbili ya wajumbe wa kupitisha Katiba inayopendekezwa.

Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki, Jaji Werema alisema kama itashindikana kufikiwa basi Katiba ya sasa ya mwaka 1977 itafanyiwa marekebisho ya 15 kuruhusu uchaguzi ujao uweze kufanyika.

“Kwa sasa akidi kwenye kamati inatosha, tukifikia Bunge kuja na Katiba inayopendekezwa na kama hakuna theluthi mbili tutarudi kwenye Bunge la kawaida (Bunge la Jamhuri ya Muungano) na kukubaliana mambo yaliyokuwa hayana ubishi tutayaweka na kuyatumia kwenye Katiba ya sasa, likiwamo suala la mgombea binafsi.

Alisema suala la maridhiano ni la demokrasia na lazima lifanyike ingawa wasuluhishi watakuwa wananchi kutokana na Bunge kuwa na kazi tatu tu, ikiwamo kujadili rasimu, kutoa Katiba na kutunga masharti ya mpito.

- Advertisement -

Related Articles

2 COMMENTS

  1. Ni vema ingawaje mmechelewa kusoma alama za nyakatil. Lakini nawaomba mkomae, msijebaadaye mkaanza kulegea kwa jina la Rushwa, au posho.Katiba ya mabavu ya CCM, si katiba ya nchi. Kwa kweli Tanzania imejiletea aibu ya ajabu dunia nzima, lakini utafiti unaonyesha kwamba siasa za maji taka sasa wasomi lazima waamke kusaidia ustawi wa nchi. Hongereni sana na Mungu awabariki sana.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles