Spika wa Bunge, Job Ndugai, ameonyesha kukerwa na kauli ya Bunge halina meno ambayo amedai imelenga kumchonganisha na wananchi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Bunge, Mjini Dodoma leo Jumatatu Septemba 20, hivi karibuni kumeibuka upotoshaji, kashfa na matusi ambavyo vinalenga kumshambulia na kumdhalilisha Spika na Bunge.
“Wanasiasa na wananchi kulishambulia Bunge na viongozi wake kwa kutoa maelezo potofu kwamba Bunge la 11 halina meno, halitekelezi wajibu wake ipasavyo na kwamba Bunge limetekwa na serikali hivyo linaendeshwa kwa kufuata maelekezo kutoka serikalini, aidha kwa kutumia lugha za kejeli,” imesema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imesema, chanzo cha kashfa hizo ni maelezo ya Spika aliyoyatoa kwa nyakati tofauti kufafanua utaratibu wa matibabu kwa wabunge, kauli na vitendo vya baadhi ya wabunge vinavyovunja Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge na utekelezaji wa shughuli za Bunge.
“Bunge linachukua fursa hii kufafanua kwamba, Ibara ya 100 na 101 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 imetoa uhuru kwa wabunge kujadili hoja mbalimbali bungeni na kufikia uamuzi,” amesema Ndugai katika taarifa hiyo.