Ofisi ya Bunge na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wamevurugana kuhusu Sh milioni 43 zilizochangwa na wabunge kwa ajili ya kusaidia matibabu Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu anayetibiwa Nairobi, nchini Kenya.
Wakati Ofisi ya Bunge ikidai fedha hizo tayari zimetumwa katika Akaunti ya Hospitali ya Nairobi Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amewaambia waandishi wa habari kuwa fedha hizo hawajazipata hadi leo licha ya kutuma barua pepe Ofisi ya Bunge lakini haikujibiwa.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Spika leo, imesema fedha hizo zimetumwa Septemba 20, mwaka huu kupitia Benki ya Barclays, Tawi la Hurlringham, Akaunti Namba 0451155318 yenye jina la Kenya Hospital Association.
“Katika mkutano wake na waandishi wa habari Mbowe alinukuliwa akisema mpaka sasa fedha ambazo wabunge walitoa nusu ya posho zao Spika wa Bunge amezitia mfukoni, pamoja na kwamba aliomba Akaunti ya Hospitali aziingize lakini mpaka leo Spika hajaziingiza hizo fedha ambazo Wabunge walitoa kwa ajili ya matibabu ya Tundu Lissu…
“Fedha hizo zingeweza kutumwa mapema zaidi isipokuwa mawasiliano yalikuwa yanafanyika kupata Namba ya Akaunti ya kutuma fedha hizo na taratibu nyingine za malipo nje ya nchi,” imesema taarifa hiyo.