25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Bulaya amstaafisha Wassira siasa

katuni-oct-28

Na SHOMARI BINDA

-MUSOMA

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Mwanza iliyoketi mjini Musoma, imemthibitisha Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Esther Bulaya, kuwa mshindi halali wa uchaguzi wa Oktoba, mwaka jana.

Hukumu hiyo imetafsiriwa na baadhi kuwa ni sawa na kumstaafisha siasa kutokana na umri wake, Steven Wassira ambaye alipambana naye katika kinyang’anyiro cha ubunge katika Jimbo la Bunda, wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

Ushindi wa Bulaya ulipingwa mahakamani hapo na wapiga kura wa Jimbo hilo, wakidai haukuwa halali.

Hata hivyo, hukumu ya mahakama hiyo iliyosomwa jana kwa zaidi ya saa nne iliamua kwamba maombi hayo hayana msingi na yametupiliwa mbali kwa gharama.

Akitoa hukumu hiyo pasipo uwepo wa Bulaya, Wakili wake, Tundu Lissu  na Wasira, Jaji wa Mahakama Kuu, Noel Chocha, alisema maombi yaliyoletwa na walalamikaji yakiitaka mahakama hiyo itengue matokeo ya Bulaya hayakuwa na msingi wa kubatilishwa kwa matokeo hayo.

“Nimepitia ushahidi wote ulioletwa hapa mahakamani, nimejiridhisha kwamba ushahidi wa waleta maombi haujitoshelezi na hauwezi kutengua matokeo yaliyompa ushindi Bulaya,” alisema.

Jaji Chocha alisema licha ya kutoridhishwa na ushahidi, lakini pia madhara ya kurudia uchaguzi ni makubwa kuliko manufaa, ukizingatia kwamba Wilaya ya Bunda ni moja ya wilaya masikini nchini, hivyo ni vyema kujielekeza zaidi katika kusukuma mbele maendeleo ya wilaya hiyo.

“Uchaguzi wa Bunda ukirudiwa hautaathiri tu wananchi Bunda, bali hata wananchi wote wa Tanzania kwa kuwa itapaswa kutafutwa fedha kwa ajili ya uchaguzi badala ya kuzielekeza kwenye shughuli nyingine za kimaendeleo.

“Nikiufuta uchaguzi hata mimi nitaathirika, maana sehemu ya fedha za mshahara wangu zitaingizwa na kuelekezwa kwenye uchaguzi huu,” alisema Jaji Chocha.

Shauri hilo namba 1/2015,

Jaji Chocha alisisitiza kuwa mifumo ya uchaguzi iliyopo ndiyo inayoamua kama uchaguzi haukuwa huru na haki na kudai sheria zilizopo zinaonyesha mifumo ni mizuri na kwamba chaguzi duniani kote kasoro haziwezi kuepukika na si kila kasoro inaweza kupelekea kufikia maamuzi ya kufuta matokeo ya uchaguzi.

Jaji amuita “jipu”

wakala wa Wasira

 

Katika hali iliyoibua kicheko mahakamani wakati wa usomwaji wa hukumu hiyo, ni pale Jaji Chocha alipomuita mleta maombi wa tatu, Janes Ezekiel, ambaye alikuwa wakala wa Wassira kuwa ni ‘jipu’, anayestahili kutumbuliwa kwa kuwa hakumsaidia kusimamia vizuri kura za mteja wake.

Alisema Wassira hapaswi kumlaumu mtu kwa kile kilichomsibu kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, kwa kuwa wakala aliyemuamini alikuwa na majukumu mengi, ikiwemo kuhakikisha anawasimamia wanafunzi kupata elimu na kusimamia masuala ya siasa.

Jaji Chocha alisema wakala huyo aliieleza mahakama kuwa, ni mtumishi wa umma kwa nafasi ya ualimu na katika kipindi cha uchaguzi kulikuwa na jukumu lingine la mitihani kwa wanafunzi, hivyo hakuweza kusimamia mambo mawili kwa wakati mmoja.

“Huyu hana tofauti na watumishi ambao kwa msemo wa sasa wanaitwa “majipu”, maana kuna mambo makubwa ambayo yeye mwenyewe alipaswa kuyasimamia, lakini inaonekana alishindwa kusimamia majukumu yake.

“Unaweza kutafuta mchawi Mahakamani wakati mchawi ni wewe mwenyewe,,nashauri katika hili mzee Wasira asije akamlaumu mtu, kuna mtu muhimu kwenye shauri hili kama Katibu wa CCM Wilaya ya Bunda alipaswa kuja mahakamani kusaidia katika shauri hili,” alisema Jaji huyo.

Mara baada ya kumalizika kusomwa kwa hukumu hiyo,  wakili wa waleta maombi alikataa kuzungumza chochote ambapo alipanda gari na kuondoka eneo la mahakama.

Naye wakili wa wajibu maombi, Paul Kipeja, alisema walitegemea ushindi kwenye kesi hiyo kwa kuwa msingi wa kesi ulikuwa umevunjwa na maombi ya wapiga kura yametupiliwa mbali kwa gharama na watakutana na mteja wake kufanya utaratibu wa  kuomba gharama za kesi hiyo.

Baada ya hukumu hiyo kuliibuka shangwe kubwa nje ya mahakama  kutoka kwa wananchi na wafuasi waliofurika kusikiliza hukumu hiyo, ambapo walidai mahakama imetenda haki.

Shauri hilo namba 1/2015 lililetwa mahakamani hapo na wapiga kura wanne wa Jimbo la Bunda Mjini, ambao ni Magambo Masatu, Matwiga Matwiga, Janes Ezekiel na Asetic Malagila, wakidai uchaguzi huo haukuwa huru na kuiomba Mahakama kuyafuta matokeo yaliyompa ushindi Esther Bulaya.

Wassira, ambaye ana umri wa miaka 71, alizaliwa wilayani Bunda, Mkoa wa Mara na kwa mara ya kwanza alishinda kiti cha ubunge wa Mwibara mwaka 1970 akiwa na miaka 25 kupitia chama cha Tanu, wakati wa utawala wa Mwalimu Julius Nyerere.

Kwa muda wote huo alikuwa akiitumikia Serikali katika nyadhifa mbalimbali,  ikiwemo uwaziri na ukuu wa mkoa.

Wassira pia nyakati fulani alipata kuwa mpinzani kabla ya kurudi tena CCM.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles