27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

BUKUKU AZIKWA DODOMA, NYALANDU AMLILIA

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA


pg-2

MWILI wa aliyekuwa mpigapicha wa Kampuni ya The Guardian Ltd, Mpoki Bukuku, umehifadhiwa katika nyumba yake ya milele jana katika eneo la Msalato  mkoani hapa, huku Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu (CCM) akieleza urafiki wake na marehemu.

Mbali na Nyalandu, wengine waliohudhuria mazishi hayo ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira Vijana na Walemavu, Antony Mavunde na waandishi mbalimbali wa habari wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Dodoma (CPC), Habel Chidawali.

Alipopewa nafasi ya kuzungumza, Nyalandu alisema alijenga urafiki wa karibu na marehemu Bukuku kutokana na uaminifu mkubwa aliokuwa nao wakati wa uhai wake.

Nyalandu ambaye amewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii katika Serikali ya awamu ya nne, alisema alikutana na Bukuku kipindi ambacho alialikwa kwenda nchini Rwanda kukutana na Rais wa nchi hiyo, Paul Kagame.

Alisema ingawa aliambatana na baadhi ya wabunge na waandishi wa habari, lakini hakutaka habari hiyo iandikwe mahali popote.

“Kweli hakuna sehemu ambapo ‘story’ hiyo ilitoka, hivyo kuanzia siku hiyo nikajenga uaminifu kwa marehemu na kuendelea kufanya naye kazi.
“Tukio ambalo sitalisahau ni katika kipindi cha kampeni mwaka jana, tukiwa katika uwanja wa ndege wa Loliondo ambapo rubani wa ndege tuliyokuwa nayo aliomba mtu mmoja ashuke ndipo walipotaka kushuka watu wawili, msaidizi wangu na Mpoki.

“Tulikubaliana ashuke Mpoki na kweli alishuka, tukiwa njiani ndege ikakorofisha, yule msaidizi wangu jasho lilimtoka mwili mzima, lakini tulifika Dar es Salaam salama na tulipokuja kuonana na Mpoki alimwambia kauli ambayo hadi leo ipo katika kichwa changu kuwa mkiona nateremka na nyie teremkeni,’’ alisema.

Pia Nyalandu alitoa ahadi ya kumlipia ada mtoto wa marehemu, Junior ambaye mwakani anaingia kidato cha nne.

“Kutokana na mazingira hayo ambayo Mpoki ameyaacha, mimi rambirambi yangu ni kumlipia ada ya Sh milioni 3.5 kwa mwaka,’’ alisema Nyalandu.

Naye Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Mtwivila mkoani  Iringa, Naftal Ng’amillo, katika mahubiri yake wakati wa kuaga mwili wa Bukuku alisema kifo cha mtu ni funzo kwa watu walio hai.

Mwenyekiti wa CPC, Chidawali, alisema tasnia ya habari itamkumbuka marehemu kwa mambo matatu ambayo ni kuipenda kazi yake, uvumilivu na kuishi na watu vizuri.

Bukuku alifariki Desemba 23, mwaka huu kwa ajali ya gari jijini Dar es Salaam. Ameacha mke na watoto watano.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles