Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital
Katika kuhakikisha kuwa inadhibiti vishoka na kuondoa migogoro kwenye kampuni mbalimbali hapa nchini, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imezindua ‘Wiki ya Suluhisha na Brela‘ ambayo ni maalumu kwa ajili ya kukutana na wamiliki wa kampuni kutoa kero zao ikiwamo migogoro.
Uzinduzi huo umefanyika leo Jumatatu Juni 13, 2022 katika Vinjwa vya Makubusho ya Taifa, Posta jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Kampuni na Majina ya Biashara (BRELA), Meinrad Rweyemamu amesema kumekuwa na wamiliki wa kampuni kutaifishwa sambamba na kuwepo kwa migogoro kwenye kampuni zao nakwamba kupitia wiki ya suluhisha na Brela wataweza kupata suluhisho la migogoro hiyo.
“kumekuwa na changamoto nyingi ambazo zimekuwa zikizikijitokeza katika kampuni nyingi hasa pale ambapo mwenye hisa anapofariki dunia huku ndugu wakiwa hawafahamu kinachoendelea ndani ya kampuni.
“Hawafahamu zile hisa za marehemu ni mali kama mali zingine ambazo zinagawiwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine, hivyo wakifika hapa ndani ya kampeni hii ya wiki moja tutaweza kutoa elimu na kusuluhisha changamoto za namna hii na kutoa elimu kuhusu haki ya mtu ni ipi,” amesema Rweyemamu.
Rweyemamu ameongeza kuwa: “Tutakaa na wamiliki pamoja na wahusika kujadiliana na kupeana elimu mwisho wa siku kila mtu apate haki yake na kuondokana na migogoro ambayo imekuwa ikitokea kwenye kampuni mbalimbali kila kukicha,” amesema.
Wiki hiyo ya Suluhisha na Brela imeanza leo Juni 13, ambapo inatarajiwa kuhitimishwa Jumapili ya Juni 19, 2022.