25.3 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Brela yashauri namna bora kusajili viwanda

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) umewataka wadau wa biashara kuzingatia maelekezo ya kusajili viwanda ili kuepuka kuchanganya leseni za biashara na zile za usajili wa viwanda.

Sheria ya Taifa ya Utoaji wa Leseni na Usajili wa Viwanda Sura ya 46 ya mwaka 1967 inaelekeza mtu anapofanya shughuli za kiwanda nchini lazima akisajili na kama ni kiwanda kidogo atapata cheti cha usajili na ikiwa ni kikubwa atapata leseni ya kiwanda.

Akizungumza Januari 27,2024 katika Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea katika viwanja vya Mnazi Mmoja Dar es Salaam, Ofisa Leseni Brela, Ndeyanka Mbowe, amesema wanapokwenda kufanya ukaguzi wamebaini baadhi ya wananchi wana leseni za biashara lakini hawana za kiwanda.

“Ni kosa kuendesha shughuli za kiwanda pasipo kukisajili, wananchi mara nyingi wanachanganya kati ya leseni za biashara na leseni za viwanda…akishapata leseni ya biashara anahisi kashasajili kiwanda,” amesema Mbowe.

Amesema wanaopata cheti cha usajili yaani viwanda vidogo mtaji hauzidi Sh milioni 100 na wanaopata leseni ya kiwanda kwa viwanda vya kati na vikubwa mtaji ni kuanzia Sh milioni 100 na kuendelea.

Amesema pia wanao mfumo wa usajili kwa njia ya mtandao (ORS) ambao unawezesha kupata cheti cha usajili wa kiwanda kidogo au leseni ya kiwanda, alama za biashara na huduma.

Mbowe amesema wanatumia maonesho hayo kutoa huduma za usaidizi kwa wadau waliopata changamoto katika shughuli za biashara na waliokwama kujisajili kwa njia ya mtandao.

Aidha amesema wanatoa huduma za papo kama vile za usajili wa majina ya biashara, kampuni, utoaji wa leseni za biashara kundi A na usajili wa viwanda.

“Sisi ni wadau muhimu katika maonesho haya kwa sababu tunasimamia sheria sita, tunasajili makampuni, majina ya biashara, tunatoa leseni za biashara, viwanda na cheti cha usajili wa viwanda.

“Wateja wetu wengi ni wananchi wanaotaka kufanya biashara au kuanzisha kampuni, wanapokuja tunawaelimisha namna ya kusajili kampuni, faida na hasara za kusajili kampuni hivyo, wananchi watumie fursa ya maonesho haya kuja kujifunza na kupata usaidizi katika changamoto mbalimbali zinazowakabili,” amesema Mbowe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles