rio de janeiro, brazil
RAIS mteule wa Brazil, Jair Bolsonaro, ametangaza kuwa nchi yake itaiga mfano wa Marekani kwa kuhamisha ubalozi wao ulioko nchini Israel kutoka mjini Tel Aviv kwenda Jerusalem nchini humo.
Bolsonaro amesema hayo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Twitter, ambapo amefichua kuwa wanapanga kuhamisha ubalozi huo kutoka Tel Aviv hadi Jerusalem, akiongeza kuwa, Israel ni taifa huru na wanaheshimu hilo.
Marekani iliuhamisha ubalozi wake Israel kutoka Tel Aviv hadi Jerusalem mnamo Mei mwaka huu, hatua iliyowaghadhabisha Wapalestina na viongozi wakuu wa Kiislamu.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amelikaribisha tangazo hilo kwa mikono miwili.
Netanyahu, akiandika kwenye ukurasa wake wa Twitter, amempongeza Bolsonaro kwa nia yake akisema ni ya kihistoria, iliyo sawa na inayopendeza.