ALGIERS, ALGERIA
KATIKA kile kinachoonekana kama jaribio la kupunguza shinikizo la maandamano ya kumpinga Rais Abdelaziz Bouteflika, kiongozi huyo ameahidi hatahudumu kwa muhula mzima iwapo atachaguliwa tena kama rais katika uchaguzi utakaofanyika mwezi ujao.
Maandamano hayo yalikuwa yanapinga harakati zake za kuongeza muda kwenye miaka 20 aliyotawala.
Kituo cha televisheni cha Ennahar kilisema kuwa Rais Bouteflika ameahidi kuachia ngazi baada ya mwaka mmoja iwapo atachaguliwa.
Tangazo hilo lililosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wake wa kampeni, Abdelghani Zaalane lilisema rais huyo amepanga kuandaa uchaguzi mpya wa mapema.
“Uchaguzi mpya wa urais utafanyika tena. Tutaufanya baada ya mkutano wa kitaifa. Naahidi sitagombea tena urais katika uchaguzi huo.
“Lengo la uchaguzi huo ni kuhakikisha makabidhiano ya madaraka kwa njia ya amani na mazingira yaliyo huru na wazi. Mkutano wa kitaifa ndio utakaoamua tarehe ya uchaguzi,” lilisema tangazo hilo.
Tangazo hilo la Bouteflika huenda ikaonekana kama mbinu ya kutaka kuwaridhisha wale walioandamana kwa siku 10 kupinga hatua yake ya kugombea tena urais.