29.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

BOT YATOA AHUENI KWA BENKI, WAKOPAJI

NA MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imetangaza neema kwa benki nchini kwa kuziongezea uwezo wa kukopesha kwa riba nafuu.

Hiyo inatokana na kupunguza kiwango cha akiba ambacho taasisi hizo zinapaswa kwa mujibu wa sheria kukihifadhi BoT kutoka asilimia 10 hadi asilimia 8.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Idara ya Uhusiano na Itifaki ya BoT, uamuzi huo utaanza kutekelezwa kuanzia Aprili 20, na unategemewa kuongeza uwezo wa benki za biashara kukopesha.

Kutokana na hali hiyo, Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu, alitoa tangazo hilo kupitia barua yake ya Machi 21, mwaka huu kwa benki, kuhusu marekebisho ya kifungu Na. 2.1 cha waraka Na. 1 kwa benki uliotolewa Desemba 2,  mwaka jana.

“Hii ni ni taarifa kwa benki zote zinazopokea amana Tanzania Bara na Zanzibar, kuwa Benki Kuu imepunguza kiwango cha akiba ambayo ni sehemu ya amana za wateja, kinachopaswa kuwekwa Benki Kuu kisheria kutoka asilimia 10 hadi asilimia 8,” alisema Profesa Ndulu.

Uamuzi huo umefanyika kulingana na kifungu namba 44 cha Sheria ya Benki ya Tanzania ya mwaka  2006. 

Sehemu ya kifungu hicho kinasema kwamba Benki Kuu inaweza kuagiza benki na taasisi za kifedha kuweka kiasi cha fedha Benki Kuu kama akiba dhidi ya amana za wateja wa benki hizo na taasisi za kifedha.

Aidha, taarifa hiyo ilieleza kuwa kisheria benki zinatakiwa kuweka kiasi cha fedha Benki Kuu kama akiba, ambayo hupatikana kwa kukokotoa asilimia ya amana za wateja kwa kila benki.

Mapema Machi 2017, Benki Kuu ilipunguza kiwango cha riba ya mikopo inayotoa kwa benki kutoka asilimia 16 hadi 12, hatua ambayo ilisifiwa na wadau katika tasnia ya benki kama hatua muhimu ya kuendeleza ukuaji mikopo (credit) kwa sekta binafsi.

Mikakati hiyo inalenga kuongeza upatikanaji wa fedha kwa benki ambazo zitapanua uwezo wao wa kukopesha na kuchangia ukuaji wa mikopo itakayotolewa kwa sekta binafsi.

Inatarajiwa kuwa benki zitatumia nyongeza hiyo ya fedha kutoa mikopo zaidi na kwa riba za chini kwa shughuli mbalimbali  za kiuchumi na hivyo kuchangia ukuaji wa uchumi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles