30.3 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

BoT yapongeza Mfumo wa Majaribio ya Suluhishi za Kidijitali NMB

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

BENKI ya NMB imezindua Mfumo wa Majaribio ya Suluhishi za Kidijitali (Sandbox Environment), ikiutengea Sh Bilioni 1 za kusaidia bunifu zitakazopita, Mfumo ambao umepongezwa na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dk. Bernard Kibesse, na kutaka Taasisi za Fedha nchini kuiiga NMB katika kuleta njia mbadala za kutoa suluhu za kibenki ambazo ni rahisi, haraka na salama.

Naibu Gavana wa Benki Kuu, Dk. Bernard Kibese akifurahi na Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa Benki ya NMB, Dk. Edwin Mhede (kulia) na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna baada ya uzinduzi wa Mfumo wa NMB wa Majaribio ya Kitekinolojia (SANDBOX) uliofanyika jana Dar es Salaam unaotoa fursa kwa wajasiliamali wa tekinolojia kujaribu ugunduzi wao kupitia benki ya NMB. 

NMB Sandbox ni jukwaa huru la NMB linalotoa fursa kwa wabunifu wa Kidogitali na wabunifu binafsi wa Kitanzania kutumia Mifumo ya benki ya NMB kujaribu suluhishi zao kabla ya kuanza kutumika rasmi.  

Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam Alhamisi Oktoba 21, ambapo Mgeni rasmi wa tukio kilo Dk. Kibesse alisisitiza kuwa mabenki nchini hayana budi kuendana na kasi ya mabadiliko ya tekinolojia ili kutoa suluhishi za huduma za kibenki, hasa katika nyakati hizi, ambazo tekinolojia  imetanua wigo wa kuhudumia.

“Uzinduzi huu wa Sandbox Environment, unafungua fursa kwa Kampuni changa na wabunifu binafsi kuonyesha ujuzi wao na kubuni suluhishi zitakazopunguza gharama za kibenki kwa watu wote, sambamba na kutengeneza ajira kwa vijana wa Kitanzania.

“BoT inatambua changamoto zinazo wakabili wateja wanapotumia huduma za kibenki, zikiwemo upatikanaji hafifu wa huduma hizo, ufinyu wa njia za kufikisha, gharama na uelewa mdogo walionao katika masuala ya fedha. 

“Serikali kupitia BoT imechukua hatua mbalimbali kumaliza changamoto hizo na uzinduzi huu unaashiria kuwa NMB inaunga mkono jitihada hizo, Kama ilivyofanya kutenga Sh Bilioni 100 za mikopo nafuu kwa wakulima, wafugaji na wavuvi,” alisema Dk. Kibese, akiahidi kuwa BoT itaendelea kushirikiana na NMB katika kuboresha sera zinazotoa mwongozo na kurahisisha ufanyaji wa biashara kwenye sekta ya kibenki.

Naibu Gavana wa Benki Kuu, Dk. Bernard Kibese akiagana na Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa Benki ya NMB, Dk. Edwin Mhede (kushoto) baada ya hafla ya uzinduzi wa Mfumo wa Majaribio ya Kitekinolojia(SADNDBOX) uliofanyika Dar es Salaam. Kulia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna.

Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB (CEO), Ruth Zaipuna, alisema benki yake imejidhatiti na kujipambanua kuendana na kasi ya tekinolojia kwa kuleta suluhishi mpya zinazorahisisha  huduma za kibenki kwa mteja mmoja mmoja na wafanya biashara wadogo na wa kati, na kwambabenki yake imetenga kiasi cha Sh Bilioni 1 kwa ajili ya kuziwezesha suluhishi zitakazopita katika majaribio hayo.

Zaipuna alimhakikishia Dk. Kibese kuwa, licha ya kwamba utatumika kwa majaribio, lakini Sanbox Environment hautoathiri kwa namna yoyote usalama wa taarifa, amana na faragha za wateja wao na kwamba baadhi ya tuzo za miaka ya karibuni ilizopata benki hiyo zimetokana na uwekezaji mkubwa waliofanya katika mifumo ya Kidijitali. 

“Hivi karibuni tumeshinda Tuzo ya Benki Bora ya Ubunifu ya wateja binafsi kutoka Jarida la Kimataifa la International Banker, huku tukiendelea kuongoza sokoni katika kutoa huduma za kibenki kidijitali na kuongeza bunifu Kama hizi za kuwaleta karibu wateja wetu kupitia mifumo ya kiteknolojia.

“Tunaahidi kuendelea kuongeza juhudi za kuhakikisha tunafikisha na kuchagiza matumizi ya huduma za kifedha miongoni mwa Watanzania bila kujali walipo, yote yakiwezeshwa na bunifu hizi za Kidijitali,” alisema Zaipuna na kubainisha kuwa Sandbox Environment ni jukwaa muafaka kwa Kampuni za Ubunifu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), kufanya majaribio ya bunifu zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles